Siku chache zilizopita rafiki yangu alinipigia simu akitaka nimshauri kama abaki dar au aende mkoani. Alikuwa njia panda kwa sababu amepata kazi dar na pia amepata kazi mkoani, kazi zote zina maslahi mazuri na ni yeye tu kuchagua. Nilimshauri abaki dar na nikampa sababu kwa nini namshauri hivyo. Nimeona huenda kuna wengine wanapata wakati mgumu kama huu na hivyo nimeona ni vyema nikatoa ushauri wa wazi kwa wote wanaofikiri ni wapi pa kuweza kufanikiwa kimaisha dar es salaam au mikoani.
Kwanza kabisa kufanikiwa kwenye maisha hakutegemei sana eneo mtu alipo ila inategemea na juhudi binafsi na malengo ya kufanikiwa. Ila tunapokuja kwenye mazingira yetu ya kitanzania kwa mtazamo wangu, DAR ES SALAAM NDIO SEHEMU PEKEE TANZANIA AMBAYO KILA MTU ANAWEZA KUFANIKIWA. Nasema kila mtu bila ya kujali kabila, dini, umri, jinsia wala kiwango cha elimu. Nitaeleza vizuri hili.
Mimi nimezaliwa moshi, nimekulia na kusomea moshi mpaka kidato cha nne. Nilikuja dar es salaam kwa mara ya kwanza miaka tisa iliyopita (mwaka 2005) na kwanzia kipindi hiko nimekuwa nikilinganisha maisha ya dar es salaam na maisha ya moshi na kuona tofauti kubwa sana.
Dar es salaam kuna fursa ya kila mtu kuweza kufanya biashara hata kwa kuanza na mtaji kidogo na akatengeneza faida kubwa.
Kwa mikoani, kwa mfano sehemu kama moshi ambapo nipafahamu vizuri ni vigumu sana kuweza kuingia kwenye biashara hasa ukiwa na mtaji kidogo, kuna watu wachache ambao wameshatawala masoko ya biashara na hivyo kuingia na mtaji kidogo ni kujipoteza.
Ni dar es salaam pekee ambapo mtu anaweza kuanzisha biashara kwa mtaji wa chini ya laki moja na akaweza kuikuza na kuwa biashara kubwa sana. Namfahamu mtu aliyeanza kufunga karanga kwa mtaji wa shilingi elfu ishirini ila sasa ameajiri vijana watatu kwenye kazi hiyo. Kuna watu wengi wanaishi dar hapa kwa biashara ndogo sana na maisha yao wanayaendesha vizuri. Watu wanauza maji na wanaishi, wanauza kahawa wanaishi, wanatembeza miwa wanaishi na hata wanaouza chenchi nao wanaishi. Ukienda sehemu kama moshi kuna watu wachache sana wanaofanya biashara za aina hii na tayari wameshatawala soko, hivyo inakuwa vigumu sana kwa mtu mpya kuingia kwenye soko la aina hii.
Ni dar ambapo mtu anaweza kuanzisha biashara bila ya kuwa na mtaji wowote na akatengeneza biashara nzuri kama anamipango mizuri. Biashara za kukusanya na kuuza makopo, vyuma chakavu, pesa mbovu, chenchi, kupiga debe zote hizi kwa mtu ambao anaweza kujipanga vizuri anaweza kufanya kwa muda mfupi na akajipatia mtaji na kuanza biashara nyingine kubwa.
Ni dar es salaam pekee ambapo mtu anaweza kuanzisha biashara ndogo ila akaingiza kipato kikubwa kushinda mshahara wa meneja wa makampuni makubwa. Namfahamu mtu ambaye alianza kuuza supu ya utumbo kwa shilingi elfu moja tu kwa sahani ila kwa miaka kama mitano sasa ameweza kununua nyumba, kutanua biashara yake na hata kuwekeza kwenye biashara nyingi zaidi, hana elimu kubwa ila ana juhudi kubwa. Namfahamu mtu ambaye alianza kuuza chipsi kwa kuchonga viazi mwenyewe, akajituma na hivi sasa ameajiri vijana sita na anabiashara nyingine nyingi zinazotokana na biashara hiyo.
Namfahamu mtu ambaye anazoa takataka mtaani kwetu ila anaishi kwenye nyumba yake na analea familia yake. Mtaji wake ni mkokoteni tu.
Namfahamu mwanaume ambaye huwa anavaa nguo za kike na kuzunguka mtaani kuchekesha na jioni anarudi nyumbani na hela ya kutosha kuendesha familia yake.
Watu wote ninaowataja hapa ni kwenye mtaa mdogo ninaokaa Tabata, hapa hatujenda kinondoni, mwenge, tegeta, mikocheni, temeke, mbagala, gongo la mboto na kwingine kwingi. Tofauti na mikoani dar es salaam hakuna anayemiliki eneo, kama wewe unafikiri unamiliki mtaa wenu mikocheni, sinza kuna watu kibao wanafanya yao, hapo hujaenda manzese, magomeni au ukonga.
Hapa natoa mifano michache sana ila kila ninapopita mitaani naona ni jinsi gani dar imejaa fursa ambazo hata mtu ambaye hajamaliza shule ya msingi anaweza kuzitumia na kuboresha maisha yake.
Kwa nini nasema yote haya?
Siandiki haya kuwashawishi walioko mikoani kukimbila dar es salaam, la hasha, popote ulipo unaweza kutengeneza mafanikio yako. Naandika haya kuwahamasisha wale walioko dar KUAMKA na kuchangamkia fursa hizi zilizopo wazi kwa kila mtu. Kuna watu wako dar hapa lakini wanalalamika maisha magumu, hakuna kazi, hakuna mitaji na kadhalika. Ila kama wakiweza kutumia fursa nyingi zinazopatikana dar wanaweza kutengeneza mafanikio makubwa.
Ni kitu gani unaweza kufanya mikoani?
Sina uzoefu na mikoa mingi ila kwa uzoefu nilionao kwa moshi, biashara ndogo ndogo ni vigumu sana kukua.
Ila kwa mikoa mingi ya kitanzania kilimo ni kizuri sana kufanyika mikoani na hiki unaweza kuanza na mtaji kidogo. Pia unaweza kuangalia mazingira uliyopo na fursa nyingine ambazo unaweza kuanza na mitaji kidogo. Kwa kujifunza vizuri mazingira yako na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa unaweza kupata mafanikio makubwa.
Kama upo DAR na unalalamika maisha ni magumu wewe ni mzembe.
Samahani kama nimetumia neno kali na linalokuudhi lakini sina njia nyingine ya kuliremba hilo. Kwa fursa hizi ambazo zinapatikana kwenye kila kona ya jiji hili ni vigumu sana kushindwa kuzitumia.
Tatizo kubwa watu wengi wanachagua sana vitu vya kufanya wakati hawana anasa hiyo ya kuchagua. Waliopata elimu kidogo nao wanaona wana hadhi kubwa hivyo kudharau shughuli ndogo ndogo ambazo zinawaingizia watu wengi kipato kikubwa.
Kuna changamoto nyingi sana dar es salaam, foleni, miundombinu mibovu, hali ya hewa ya joto, wingi wa watu na mengine mengi. Ila ukiweza kutengeneza njia nzuri ya kukabiliana na changamoto hizi unaweza kupata faida kubwa sana ndani ya jiji hili.(Kwa mfano kukabiliana na changamoto ya foleni unaweza kufanya hivi, bonyeza hapa kusoma zaidi.)
Kwa nini wengi hawafanikiwi?
Pamoja na watu wengi niliowataja hapa bado kuna wengi sana ambao wanafanya biashara ndogo ndogo huku mitaani ila bado hawafanyi vizuri. Tatizo kubwa linatokana na kutokuwa na mipango mizuri na kukosa ubunifu. Wengi wanafanya biashara kwa kuiga, mtu anaona mwenzake anauza kahawa na yeye anaenda kuanza kuuza kahawa bila hata ya kuangalia ni jinsi gani anaweza kuitofautisha na kutengeneza soko kubwa zaidi.
Kama upo dar es salaam na unateseka kutengeneza kipato karibu tushauriane njia bora za wewe kuweza kujenga uchumi wako na kufikia mafanikio makubwa. Kwa ushauri zaidi unaweza kuwasiliana na mimi kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kuboresha maisha yako.
Kumbuka TUKO PAMOJA kwenye safari hii.