Na: Meshack Maganga- Iringa.
Ndugu zangu, awali ya yote napenda kutuoa shukrani zangu za dhati kwa wasomaji walioniandikia na kunipigia simu na jumbe fupi nyingi sana nilipoandika makala ya mwezi wa 4/2014 niliyoipa kichwa cha ‘Unaweza kujiajiri kupitia kilimo cha vitunguu’ (kama hukuisoma bonyeza hayo maandishi kuisoma). Nilipokuwa nina andika makala ile ofisini kwangu Iringa, niliona nikama niandika mambo ya kawaida tu, maana mimi ni mzoefu, kumbe yalikuwa mambo mhimu sana na yaliyo wasaidia watanzania wengi, nilisafiri kwenda Kyela nilipokuwa ndani ya gari nilipokea jumbe fupi 442 na email nyingi sana zaidi 56, nilipigiwa simu nyingi, nilijitahidi kujibu email, kuna baadhi ya jumbe fupi zilinigusa sana, Msomaji mmoja alinitumia ujumbe huu “ Ni furaha gani niliyojawa baada ya kusoma maelezo yako ya kilimo, mi ninasema umeletwa na Mungu ili mimi nifanikiwe…” Nimejifunza sana na kupata marafiki wengi sana na baadhi yao wamechukua hatua za kuanza kulima kilimo cha vitunguu na baadhi yao wameanza kuwekeza kwenye kilimo cha miti.
Kwa kifupi sana leo nitaongelea umuhimu wa kuzichangamkia fursa za mafanikio zilipo ndani ya nchi yetu yenye amani na kila aina ya fursa, hii ni kwa sababu wengi wetu ama kwa kufanya uzembe na kujipa moyo kwamba muda bado upo, tumekuwa tukipoteza fursa hizo. Ama wengi wetu tumezikosa fursa hizo kwa visingizio lukuki, ama wengi wetu hatuna taarifa sahihi ya kile tunachokitaka, na wengi wetu tumekuwa na mipango mingi sana na wengine tumepoteza fursa kwakuwa ‘bize’ na ndoto za wenzetu na kushabikia kila kinachotoea mtaani kwetu.
Dunia hii na nchi yetu kwa ujumla wake imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na hivyo kuwezesha fursa za kila aina kuwa wazi, kwa sasa kilimo kimeajiri watu wa kada zote waliosoma na wasiosoma, ongezeko la watu mjini na vijijini imesabaisha uhitaji mkubwa sana wa chakula, kila utakacho amua kukifanya kwenye sekta ya kilimo kitakuletea pesa, utajiajiri na kupata pesa ya kutosha. Lakini unapoisikia fursa ya kilimo nenda ukaifanye ama ujifunze, uamue kuifanya ama kutoifanya, uamue kufanikiwa ama kushindwa, ama uendelee kupiga kelele na kutoa lawama kila siku.
Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani wanaweza. Siyo dunia ya kufuata mkumbo wala upepo na matukio ya kijamii. Wapo wanaopenda kuwa madaktari, wapo wanaopenda kuwa waimbaji nk. Kila mtu ana kitu anachopenda kinachomfanya acheke akiwa duniani. Tafuta kitu unachokipenda na kiendeleze, kitakuletea mafanikio, usisubiri umalize masomo yako, ama ukifikisha umri wa kuacha kazi ndio uaanze kutafuta nini cha kufanya utajuta hapo baadae.
Ukitaka kutembea na kuishi kimafanikio kuwa na njaa ya fursa na mfanikio kila kila siku. Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta maarifa kwa kusoma vitabu, kuuliza na kujifunza, na hata kuhudhuria mafunzo ya kuwaendeleza mara kwa mara. Mwaka huu mwezi wa tatu, nilikutana na mjasirimali Paul Masatu akanipatia Elimu ya jinsi ya kubadili mtazamo, imenisaidia sana kubadilisha mtazamo wangu na nimefanikiwa kujenga mtazamo wangu kwa kiasi kikubwa.
Na ndivyo ilivyo unapotafuta fursa, huwezi kutafuta fursa kwa kusoma mambo yasiyoendana na fursa unayoitaka, kwa mfano kama wewe ni binti uliyehitimu chuo na ndoto yako ni kwa mjasiriamali kwenye kipengele cha saluni, nenda ukawatafute wenye saluni kaa nao ujifunze kwao, unataka kulima vitunguu watafute walima vitunguu wakupatie mbinu. Huwezi kuwa na ndoto ya kuanzisha mgahawa halafu ukataka ushauri kwa mfugaji huenda akakukatisha tamaa na ndoto yako ikapotea kabisa.
Nimesoma Kitabu cha Mwalim Mwakasege amesema kwamba, “watu wengi wamekuwa wakifikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyewapangia kuwa maskini. Na hata wakristo wengine kudiriki hata kuuona umaskini kama sehemu ya utakatifu na unyenyekevu”. Ina maana mpaka sasa kuna watu wanaofikiri kwamba umaskini ni kama sifa fulani hii ni hatari.
Achana na mawazo yatakayo kukatisha tamaa, ni mpango wa Mungu ni kukuona wewe ukishi maisha ya furaha, maisha ya utele na mafanikio katika Nyanja zote za kiuchumi na kijamii. Ninawatakia mafanikio mema .
SISI WOTE NI WASHINDI.
Mawasiliano; 071348636 email meshackmaganga@gmail.com https://www.facebook.com/pages/Fresh-Farms-Trading