Karibu kwenye kona yetu ya ushauri. Wiki hii tutashauriana nini cha kufanya pale unapoanza biashara ila baada ya muda ikafa.

Hii ni moja ya changamoto inayowakuta watu wengi sana walioko kwenye biashara na wanaoingia pia. Takwimu zinaonesha kwamba katika kila biashara kumi zinazoanzishwa ni moja tu inayoweza kukua na kuingiza faida baada ya miezi kumi na nane. Asilimia tisini ya biashara zinazoanzishwa zinakufa kabla ya muda huo na hata zile ambazo hazifi zinakuwa haziingizi faida ya kutosha kujitosheleza kusimama zenyewe.

Kabla hatujaangalia ni mambo gani unayoweza kufanya unapokutana na hali hii, tuone ujumbe wa mmoja wa wasomaji ambaye aliomba ushauri kuhusiana na changamoto hii;

Nimekutana na changamoto nilifungu biashara hata mwaka haukuisha ikafa nifanye nini maana nilichukuwa mkopo ndo nikafungua ila biashara iliisha na mkopo sikumaliza mpaka sasa sijui nifanye nini.

FAIL

Safari ya biashara au ujasiriamali sio safari rahisi, ni safari iliyojaa vikwazo na kushindwa kwingi. Lakini habari nzuri ni kwamba vikwazo na changamoto hizi zimewekwa ili kuwazuia wale ambao hawajajitoa kweli kushindwa na kuwapa nafasi wale ambao wamejitoa kweli kufanya biashara au ujasiriamali.

Hivyo kwa kiwango chochote ambacho umeshindwa kwenye biashara swala la kwanza kabisa ni kutokata tamaa. Maana pale tu unapokata tamaa unakuwa umekubali kujiondoa kwenye safari ya mafanikio katika biashara.

Baada ya kuondoa hali ya kukata tamaa kitu cha pili kufanya ni kujifunza kutokana na kikwazo ulichopitia.

Tatizo moja kubwa ambalo watu wengi wanaopata changamoto hii wanafanya ni kutumia muda mwingi kulalamika mwamba wameshindwa na kusahau kutumia muda mwingi kujifunza ni wapi walikosea. Unachotakiwa kufanya baada ya kushindwa ni kujiuliza ni wapi ulipokosea. Hata kama hali ya uchumi ni mbaya au kuna mambo yaliyo nje ya uwezo wako yaliyosababisha biashara yako kushindwa bado kuna sehemu ambapo utakuwa ulifanya makosa mpaka biashara hiyo kushindwa. Jua ni makosa gani uliyofanya wewe yaliyosababisha kushindwa kwa biashara yako.

Baada ya kujua makosa yako jua ni jinsi gani unaweza kuepuka kuyarudia tena mbeleni wakati unaendelea na biashara. Pia angalia sababu ya kushindwa kwa biashara yako na makosa uliyofanya kama yanaweza kurekebishika au unaweza kubadili baadhi ya mambo ili hali hiyo isijirudie tena. Kwa njia hii unaweza kubadili mfumo unaofanyia biashara, mbinu unazofanyia biashara au hata aina ya biashara. Usikimbilie kuacha au kubadili biashara kabla hujajua chanzo hasa cha kushindwa ni nini.

Ukishajua ni njia ipi unayochukua baada ya hapa jipange upya, weka malengo na mipango mipya ya kufanikiwa kwenye biashara na uanze kuitekeleza. Kama biashara iliyokufa ilihusisha mkopo inabidi kuzungumza na mtu au taasisi iliyokupatia mkopo juu ya kubadili muda wa kulipa mkopo. Kama itashindikana kubadili unaweza kuangalia vyanzo vingine vya fedha ili kuendelea kurudisha mkopo. Ila unapoanza tena biashara baada ya kushindwa anza kwa kutumia vitu vilivyobaki kutoka kwenye biashara iliyokufa. Kulingana na biashara uliyofanya kuna vitu vinabaki hata baada ya biashara kufa, inaweza kuwa vifaa, bidhaa, samani, au hata wateja wachache ambao walishakuwa wateja wa kudumu. Anza na vitu hivi kuanza kujenga tena biashara yako.

Wakati unaanza tena kuijenga biashara yako zijue alama za hatari. Jua ni vitu gani vikianza kuonekana biashara inakuwa inaelekea kubaya. Kwa kujua alama hizi ulizojifunza kwenye biashara itakuwa rahisi kwako kuchukua hatua kabla mambo hayajawa mabaya.

Kama biashara iliyokufa ni biashara yako ya kwanza basi nakupa hongera kwa sababu umeshafanya mtihani wa kwanza na muhimu kuelekea kwenye mafanikio. Kufaulu mtihani huu inategemea na wewe mwenyewe, kama utaendelea na biashara umefaulu na kama utakata tamaa umefeli. Kushindwa mapema kwenye biashara ni kitu kizuri kwani inakusaidia kujifunza mapema kabla biashara haijawa kubwa sana kiasi cha kukufanya upoteze kila siku.

Naamini kwa kuanza na haya machache utapata mwanga wa kuanza tena kuikuza biashara yako. Kwa ushauri zaidi wa vitendo unaweza kuwasiliana na mimi kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887

Nakutakia kila la kheri katika changamoto za kila siku za biashara.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kuyaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa mawasiliano yangu hapo juu.

Karibu sana, TUKO PAMOJA.