Kila mmoja wetu ana mawazo mazuri sana ya jinsi ya kuboresha maisha yake. Inawezekana kabisa unajua maisha unayoishi hayawezi kukuletea mafanikio. Hivyo umeshapanga kwenye kichwa chako mipango mizuri ya kubadili maisha yako na kuyaboresha zaidi. Lakini pamoja na kuwa na mipango mizuri inapofika kwenye utekelezaji unashindwa kabisa kuanza. Huenda umeshakaa kwenye ajira miaka mingi hakuna unachoweza kuhesabu zaidi ya madeni na kazi inayokuchosha, umeshachoka na kuona imetosha sasa, umeshapanga kwamba utaachana na kazi hiyo na kufanya biashara au kujiajiri. Lakini miaka inaenda na bado unajikuta kwenye kazi hiyo ya mateso na kushindwa kabisa kutekeleza mipango yako?

Unajua hii yote inatokana na nini? Ngoja tuone ujumbe kutoka kwa mwenzetu ambaye aliomba ushauru kuhusiana na hili.

Changamoto inayo nikabli mimi ni jinsi ya kufanya kitu pia nakuwa na hofu pale ninapoona mtu ameanguka kwenye kile kitu ninachotaka kufanya mimi, mfano biashara.

 

Kinachomsumbua msomaji mwenzetu na kinachokusumbua wewe pia ni HOFU YA KUSHINDWA. Hii ni sumu kali sana ambayo imeua ndoto za watu wengi mno mmoja wao ukiwa wewe. Unapanga mipango mizuri sana lakini inapofika kwenye utekelezaji hofu inaingia. Kwa mfano umepanga kuachana na ajira inayokusumbua na isiyokuridhisha ili ukajiajiri au kufanya biashara, baada ya mipango yote unapofikia kwenye kutekeleza hofu inapiga hodi. Unaanza kufikiria hivi nikishindwa itakuwaje? Mbona fulani amejaribu akashindwa? Si bora hiki kidogo ninachopata cha kusogeza maisha yangu kuliko kukosa kabisa! Baada ya maswali haya unaweka mawazo yako kwenye shimo la taka na kuendelea na maisha yako magumu na yasiyo na furaha.

KUSHINDWA

Hofu ya kushindwa ni kitu cha uongo, yaani ni kitu cha kutengeneza kwenye vichwa vyetu, sio ukweli bali ni uhalisia tunaojaribu kuutengeneza. Kwa kuwa hofu hii ipo kwenye vichwa vyetu basi hata kuikabili inabidi kubadili mawazo yetu na mitazamo yetu.

Ili kuondoa au kuishinda hofu ya kushindwa jua mambo yafuatayo;

1. Kushindwa haimaanishi huwezi.

Kikubwa unachoamini kwenye hofu ya kushindwa ni kwamba pale unaposhindwa ndio uthibitisho kwamba HUWEZI. Huu ni uongo mkubwa sana ambao umekuwa unaamini kwenye maisha yako. Hakuna uhusiano wowote kati ya kushindwa na kutoweza. Kushindwa inamaanisha kuna njia mbaya za kuepuka ambazo ulikuwa hujajua na kuna njia nzuri za kufanya ambazo ulikuwa hujazijua. Hivyo unaposhindwa ni furaha! Kwa sababu gani? Kwa sababu hatimaye umejua ni njia gani ambayo haifanyi kazi na hivyo usiirudie tena kama unataka kufanikiwa.

2. Kushindwa ni kujifunza.

Hatuendi mbali sana na hoja ya kwanza. Unaposhindwa ndipo unapojifunza. Na unaposhindwa haraka ndivyo unavyojifunza haraka. Hivyo badala ya kuogopa kushindwa, jua kabisa ndio njia ya kujifunza. Na jambo kubwa la kushangaza duniani ni kwamba mambo bora kwenye maisha yetu huwa tunajifunza kwa hali ngumu. Hivyo unapojifunza kupitia kushindwa ni somo zuri sana ambalo hutolisahau kamwe kwenye maisha yako.

3. Kushindwa mwingine haimanishi na wewe utashindwa.

Sijui haya mawazo huwa tunatoa wapi lakini tunapenda sana kupima maisha yetu kwa kuyalinganisha na maisha ya watu wengine. Hata kwenye kushindwa tunaamini kama wengine wameshindwa basi na sisi tutashindwa. Nilishasema tena wewe ni wa pekee katika dunia hii, katika watu zaidi ya bilioni saba wanaoishi duniani kwa sasa. Kama kuna mwenzako amejaribu akashindwa haimaanishi na wewe utashindwa. Na hata ukishindwa tayari utakuwa na mtazamo tofauti na yeye hivyo hutokata tamaa na kuacha kama yeye alivyoacha.

4. Hakuna mtu ambaye hajawahi kushindwa.

Tunapenda kuangalia maisha ya watu waliofanikiwa baada ya kufikia mafanikio. Hatujawahi kukaa na kufuatilia ni njia gani ngumu watu hawa walizipitia mpaka kufikia walipofika leo. Na hata tukifuatilia kwa kuwauliza wao wenyewe kuna wengine watakudanganya. Ukweli wa mambo ni kwamba mtu yeyote unayemuona amefanikiwa leo jua amepitia njia ngumu sana kufika hapo alipo. Ameshindwa sana lakini kutokana na shauku kubwa ya mafanikio iliyokuwa ndani yao waliweza kufanya tena na tena na hatimaye kufanikiwa. Wale walioanza nao ila wakakata tamaa baada ya kushindwa mara moja hujawahi kuwasikia! Je na wewe unataka kuishia kimya kimya kama wao? Hii sio saizi yako, mafanikio ndio halali yako, ukishindwa jifunze kisha anza tena.

5. Haujaribu kufanya bali UNAFANYA.

Kila mara ninapopata nafasi ya kuongea au kushauriana na msomaji yoyote nimekuwa nikipata neno moja karibu kutoka kwa kila mtu. Neno hilo ni KUJARIBU. Mtu anakuambia “kutokana na changamoto nilizopitia nimeona ni bora nijaribu biashara” kwa kauli hii tu najua huyu anakwenda kushindwa na mbaya zaidi anaposhindwa ataacha kwa sababu jaribio lake litakuwa limefika mwishoni. Hata kwenye sayansi, unapofanya majaribio na yakaenda tofauti na sheria zilizopo unahitimisha kwamba jaribio hilo ni la uongo au limeshindikana. Sasa wewe tayari una mawazo kwamba kuanza kitu kipya unaweza ukashindwa, ila unajipa moyo kwamba ngoja ujaribu kufanya na huenda ukafanikiwa. Inapotokea ukashindwa ndio unakuwa mwisho wa jaribio na unahitimisha ya kwamba umeshashindwa na huwezi. Hii ni kauli ndogo sana ambayo unapenda kuitumia lakini madhara yake ni makubwa sana. Hujaribu kufanya biashara, unafanya biashara na hayo ndio yatakuwa maisha yako, ushindwe usishindwe hakuna kitakachokutoa kwenye njia hiyo. Unatakiwa kusema maneno hayo bila ya kuona aibu kama kweli unataka kufanikiwa kwenye biashara. Ila kama utaendelea na kauli zako za kujaribu utajaribu mpaka utamaliza majaribio yote na bado hutopata mafanikio.

6. Kushindwa haimaanishi ndio mwisho wa safari.

Kuna mambo mengi sana ambayo yanatokea kwenye maisha yetu ya kila siku ambayo yanaonesha kushindwa ila hauwi ndio mwisho. Ila inapotokea sisi kushindwa tunaamini ndio mwisho, jambo ambalo linashangaza kidogo.

Kwa mfano watu wanakufa kwa ajali za magari kila siku, je kuna siku umewahi kufikiria kwamba utaacha kupanda gari kutokana na ongezeke la ajali? Gari inapata ajali, wenzako wanakufa ila wewe unapelekwa hospitali kwa kutumia gari nyingine. Kwa nini usingekataa kabisha kupanda gari nyingine baada ya kupata ajali kwa gari? Hii ni kwa sababu usafiri ni kitu muhimu sana hivyo hata kama watu wanakufa bado tunaendelea kuutumia huku tukiwasihi madereva kuwa waangalifu. Sasa kwa nini usitumie mfano huu kwenye jambo lolote unalofanya! Kwamba pale unaposhindwa sio mwisho wa safari bali unahitaji kuendelea mbele ili kuweza kufikia mafanikio.

Kushindwa hasa pale unapofanya jambo jipya ni lazima, naweza kukuhakikishia hilo, ila mafanikio yako yatatokana na wewe kuweza kujifunza kutokana na kushindwa na kuboresha zaidi njia unazotumia.

Kama una wazo la kufanya biashara au jambo lolote jipya, anza kutekeleza, unaposhindwa jifunze kisha endelea kuboresha na kuimarisha. Baada ya muda, kama utakuwa na uvumilivu na ubunifu utafikia mafanikio makubwa. Usiogopeshwe na wengine kushindwa au watu wanaokukatisha tamaa. Wewe pekee ndiye unayejua uwezo mkubwa ulioko ndani yako.

Mafanikio ni haki yako utakayoipata kwa kuweka juhudi na maarifa.

Nakutakia kila la kheri katika safari hii ya mafanikio.

Kumbuka TUKO PAMOJA. 

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.