USHAURI; Jinsi Unavyoweza Kufanya Biashara Yenye Mafanikio Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Zaidi ya asilimia tisini ya biashara zinazoanzishwa na watu ambao bado wako kwenye ajira zinashindwa kukua au zinakufa kabisa. Hili ni tatizo kubwa sana ambalo linarudisha watu wengi nyuma na kukatisha tamaa wengine kuingia kwenye biashara kabisa. Je inawezekana kufanya biashara yenye mafanikio ukiwa bado umeajiriwa? Hebu tuone kwanza changamoto za wasomaji wenzetu wa AMKA MTANZANIA.

nafanya biashara wakati bado nimeajiriwa hnapata shida haswa kwenye ufuatiliaji”

“changamoto ni pamoja namna ya kuweka akiba, na jinsi ya kutumia muda vizuri na kwa hiyo basi ina sababisha kuwa ngumu kupata mtaji ila pia kuukuza”

“Asante ndugu kwa kunifungua mawazo na fikra kadhaa ambazo nimekuwa nikizifikiria mara nyingi sana hasa ninapokuwa naona nikitaabika na ajira na kuona kamwe sitaweza kutimiza malengo lakini kwa sasa najiona iko siku nitafikia malengo yangu.
Mimi changamoto kubwa inayonitatiza ni muda wa kuweza kufanya biashara kwani muda mrefu niko kwenye kazi za mwajiri wangu na nahisi nikifungua biashara ufuatiliaji wa hiyo biashara nitakuwa sina na nahisi nitakuwa namfaidisha mtendaji atakaekuwa anafanya hiyo biashara”.

Hawa ni baadhi ya wasomaji ambao wameniandikia kuhusiana na changamoto hii. Huenda hata wewe ni mmoja wa watu ambao wanatamani kuanzisha biashara au umeshaanzisha ila kuwepo kwenye ajira kunakuwa changamoto kubwa kwako. Leo tutaangalia jinsi ya kuweza kusimamia biashara yako na kuikuza ukiwa bado kwenye ajira.

Japokuwa ni vigumu sana kuweza kuanzisha biashara na kuikuza wakati bado umeajiriwa bado ni muhimu sana kufanya hivyo.

Ni muhimu sana kuanzisha biashara yako wakati bado unaendelea na kazi yako kwa sababu kama mtaji ulionao ni kidogo ni vigumu sana kuweza kuanza kuitegemea biashara mwanzoni. Biashara inahitaji muda kukua ndio uweze kuanza kuitegemea kwa kipato. Hivyo ukiweza kusimamia biashara yako vizuri wakati bado uko kwenye ajira itakuwa rahisi kwako kuweza kuondoka kwenye ajira pale biashara inapokomaa.

kitabu kava tangazo

Pamoja na umuhimu huu bado kuna changamoto kubwa sana ya kuweza kuendesha biashara ukiwa bado umeajiriwa. Usipokuwa na usimamizi makini unaweza kukuta unawafaidisha uliowaachia biashara waisimamie. Kama tunavyojua binadamu wanapenda kufanya kazi kidogo na kupata malipo makubwa, watu uliowapa biashara yako waisimamie wanaweza kukuingiza kwenye hasara kubwa.

Unawezaje kuepukana na changamoto hii?

Kuna mambo matatu muhimu unatakiwa kufanya wakati unaanza biashara yako ukiwa bado kwenye ajira ambayo yatasaidia biashara yako kuweza kukua. Mambo hayo ni;

1. Kuwa na matumizi mazuri ya muda.

Hili ndio jambo moja muhimu ambalo kama ukiweza kulimudu vizuri unauhakika wa zaidi ya asilimia tisini kufaulu kwenye biashara yako. Changamoto kubwa inayowapata watu wenye biashara na ajira ni jinsi ya kugawa na kutumia muda wao katika sehemu hizi mbili.

Una masaa 24 kwa siku, ondoa masaa nane ya kulala(usilale zaidi ya masaa 8) unabaki na masaa 16, Ondoa masaa nane au kumi ya kazi unabaki na masaa 6, Ondoa masaa mawili ya kupumzika na kukaa na familia au uwapendao unabaki na masaa 4. Masaa manne kila siku unaweza kuyatumia vizuri sana kufuatilia na kusimamia biashara yako. Wakati mwingine unaweza kupata zaidi ya hapo, na hata ukipata chini ya hapo bado hata masaa mawili kila siku yanakutosha sana kusimamia na kufuatilia biashara yako. Na mwisho wa wiki unapata muda mwingi zaidi ya kuwa kwenye biashara yako.

2. Badili mfumo wako wa maisha.

Tatizo jingine kubwa kwenye kufanya biashara huku bado una ajira ni kujisahau na kuendelea kuishi kama wafanyakazi wengine. Yaani wewe una biashara nje ya ajira yako lakini unataka uishi kama wanavyoishi wafanyakazi wenzako ambao hawana biashara. Kama mkiwa kazini wote mnazungumza kitu kimoja, mkitoka mnapitia sehemu za kupumzika pamoja na kustareheka pamoja, itakuwia vigumu sana kufuatilia biashara zako.

Pia inakubidi usahau baadhi ya vitu ambavyo wenzako ambao wana kazi tu wanavifanya. Kama umezoea kila siku kwenda baa baada ya kutoka kazini huwezi kuendelea kufanya hivi ukiwa kwenye ajira na ukiwa na biashara. Huna anasa ya kupoteza muda kila siku wa kufuatilia habari, mabishano, na hata michezo mbalimbali. Kuna wakati unahitaji kutoa kafara vyote hivyo ili uweze kupata muda wa kutosha kufuatilia biashara zako.

3. Ajiri kwa uangalifu mkubwa.

Kabla hujamuamini mtu na kumpa biashara yako na aiendeshe ni vyema sana kumjua mtu huyo vizuri. Usifurahie tu kumuajiri mtu ka sababu ana maneno mazuri, chukua muda wako na mfatilie historia yake ya juma bila ya yeye kujua. Jua kama ni muaminifu, mchapa kazi na mwenye kujituma. Pia jua historia yake kwa sehemu mbalimbali alizowahi kufanya kazi. Pia weka utaratibu wa kuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi kwenye biashara yako muda wowote ambao mfanyakazi/wafanyakazi hawajui kama utakuwepo. Kwa njia hii itawafanya kuwa kwenye kazi na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Kuwa muangalifu sana kama utampa ndugu yako asimamie biashara yako, historia inaonesha wengi wamepata hasara kwa kuwaamini sana ndugu zao, ba inakuwa vigumu kuwachukulia hatua za kisheria. Ajiri mtu ambae itakuwa wazi kwake kama atafanya makosa au uzembe atawajibika kisheria, hii italeta nidhamu kubwa kwenye biashara yako.

Inawezekana sana kuweza kujenga biashara yenye mafanikio ukiwa bado umeajiriwa. Kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuwa na maisha tofauti na wengine ambao hawana kazi na ajira kwa wakati mmoja. Kuwa na mipango mizuri amabyo itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa na hatimaye kuweza kuachana nautumwa(ajira) na kusimamia biashara zako vizuri zaidi. Kama unaendelea kupata changamoto kubwa ya kuweza kusimamia biashara tako ukiwa bado kwenye ajira tuwasiliane kwa mawasiliano hapo chini kisha tutajadiliana zaidi kuhusiana na changamoto yako na kupata suluhisho bora kwako.

Kumbuka kama wewe hutaweza kuilinda fedha yako hakuna atakayeweza kukusaidia kuilinda, kuwa makini sana na biashara yako hasa pale ambapo una muda kidogo wa kuifuatilia.

Nakutakia kila la kheri na mafanikio makubwa kwenye biashara yako.

TUKO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s