Tambua kuwa kufikia mafanikio makubwa katika biashara na Ujasiriamali si kazi nyepesi. Ili wewe nawe uweze kufanikiwa unahitaji kujiwekea malengo yenye kufaa, kuyafanyia kazi na utafanikiwa .

Katika kona yetu ya Ujasiriamali na biashara tutaona juu ya namna bora ya kujenga ustawi katika biashara. Lengo la kujenga ustawi katika biashara yako ni kupanga na kujenga maendeleo endelevu, kuwa na namna ya kufanya biashara isimame imara. Katika biashara mpya au iliyokomaa, ni muhimu kujiwekea utaratibu wa kupitia madhumuni hasa ya kile unachofanya, na hili linaweza kufanyika kila baada ya kipindi fulani . Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa unalenga shughuli moja au chache ulizoamua kuzifanya na kuzisimamia vizuri na kwa ufanisi. Hii itakurahisishia kuweka madhumuni na malengo unayoweza kuyatimiza na kupata matokeo tarajiwa.

Kumbuka kuwa namna bora ya kupunguza hasara ya rasilimali unazotumia katika biashara, ikiwamo matumizi ya fedha za biashara, na kila wakati jiwekee utaratibu wa kutofautisha matumizi ya fedha za biashara kwa mambo binafsi na ya biashara.

Ni wazi kuwa kwa wajasiriamali wengi wana kiu ya kuongeza kipato na rasilimali mbalimbali katika biashara zao. Kiu hii ya wajasiriamali itafikiwa tu kwa kujenga utamaduni wa kufikiria kesho. Tambua kuwa suala la kujenga ustawi katika biashara siyo suala la kulala na kuamka, unahitaji kujenga nidhamu katika biashara .Ili kujenga mazingira mazuri ya kufikiria kesho, yafaa kwa mjasiriamali kujiuliza maswali mbalimbali ambayo yatakuwa na majibu yatakayotoa mwelekeo wenye kufaa ambao utaisaidia biashara kupata ustawi, baadhi ya maswali ya kujiuliza ni kama yafuatayo:

1. Kwa nini unafanya biashara unayoifanya?

Swali hili litakupa wasaa wa kujitathmini na kupima mwelekeo wa kile unachokifanya. Kwa swali hili utapata mchanganuo wa sababu za wewe kufanya bishara husika na siyo nyingine. Swali hili litakupa majibu ya kwa nini uliamua kutumia nguvu na mali zako kufanya biashara hiyo na siyo nyinginezo. Yafaa kukumbuka wapo wajasiriamali ambao walishindwa biashara kutokana tu na kufanya yale ambayo wengine wanafanya.

Soma; Ushindani utakuondoa kwenye biashara.

2. Ungependa biashara yako iwe katika hali gani?

Usifanye mambo kimazoea, jiwekee malengo yatakayo kuwa chachu ya wewe kupata mafanikio katika biashara yako. Hili ni swali ambalo linamjenga mjasiriamli kufikiria kesho, na ili kujenga kesho yenye kuleta ustawi yafaa kujiwekea vigezo mbalimbali katika biashara ili kwa kuvisimamia vema uweze kuandaa mazingira ambayo yatakusaidia kufikia mafanikio katika biashara.

3. Unahitaji kitu gani kufikia malengo yako?

Lengo la swali hili ni kujua yale yaliyo muhimu ili uweze kujenga ustawi katika biashara unayofanya, je unahitaji vitu gani zaidi ili uweze kupata mafanikio ya kweli? Kaa chini ufikirie yale ambayo unayahitaji ili kupata mafanikio ya uhakika. Kwa mfano, yafaa kujiuliza je bidhaa au huduma unayotoa ina ubora gani, je wateja wa biashara yako ni kina nani hasa, ni kwa njia gani unaweza kuongeza idadi ya wateja wako.

4. Vikwazo gani unahitaji kuvivuka ili kufikia malengo tarajiwa?

Yafaa kukumbuka kila wakati vikwazo mbalimbali ambavyo vinaweza kuwa sababu ya wewe kurudi nyuma kibiashara. Baadhi ya vikwazo vya kujiuliza ili kujenga ustawi katika biashara yako na hatimaye kufikia malengo yako ni pamoja kutathmini udhaifu ulio nao katika kuendesha biashara yako. Kumbuka huwezi kuwa mzuri kwa kila jambo, utakuwa na mazuri na mabaya. Jipime wewe na washindani .

Pamoja na maswali haya ambayo yanaweza kutoa mwelekeo wenye kufaa wa namna bora ya kujenga ustawi katika biashara yako, yafaa pia kukumbuka baadhi ya vitu ambayo vitasaidia kujenga ustawi na kukupa mwelekeo wa mafanikio katika biashara yako. Inashauriwa kuwa na shughuli chache unazozimudu vema. Kuwa na shughuli ambazo utazimudu kwa kuzisimamia vema, wapo wajasiriamali ambao wameshindwa kufanikiwa kutokana na kuwa na shughuli nyingi na kushindwa kuzisimamia vema.

Ili kujenga ustawi katika biashara yafaa madhumuni ya biashara yako yafahamike na kueleweka vema. Na ili kujenga mwelekeo wa mafanikio katika biashara yako, yafaa kuwa na mchanganuo mzuri wa wateja wako. Yafaa kuzingatia mahitaji ya soko na andaa rasilimali zenye kufaa ili kutoa huduma bora kwa wateja. Jenga utamaduni wa biashara yako kuwa bora, wewe kama mmiliki wa biashara husika yafaa uwe mfano wa kuigwa na wengine katika biashara yako, kuwa mtu wa mfano. Jijengee mazingira ya kudumisha ubora wa biashara na bidhaa kila wakati.

Pia Tafuta namna bora ya kuwathamini wafanyakazi wako ili waweze kuelewa malengo yako vema. Lingine la kuzingatia ni kujenga utamaduni wa kusimamia vema fedha za biashara yako. fanya tathmini ya fedha kwa kuzingatia mapato,matumizi na gharama za biashara ili biashara yako iweze kuwa endelevu.weka namna bora ya kutunza kumbukumbu za biashara yako. Epuka mazoea ya kutembea na kumbukumbu kichwani mwako. Haiwezekani kuyakumbuka matukio yote.

Tunakutakia mafanikio mema ya biashara yako na TUPO PAMOJA

Makala hii imeandikwa na Geofrey Mwakatika, Unaweza kutembelea blog yake Geofrey Mwakatika(bonyeza maandishi hayo) kujifunza zaidi.

kitabu-kava-tangazo4323