Kama zilivyo kanuni zingine za maumbile zinazofanya kazi kila siku katika maisha yetu na kuleta matokeo makubwa, pia ipo kanuni muhimu ya pesa ambayo ni muhimu sana kwako wewe kuijua na kuitumia kila siku ili uwe tajiri. Kuijua kanuni hii, kutakusaidia wewe kuweza kuelewa na kutumia uwezo mkubwa ulionao kukufanikisha katika maisha yako.
 

Kanuni hii inafanya kazi kwa mtu yeyote, endapo tu ataiamini na kuifanyia kazi katika maisha yake. Ni kanuni ambayo inaweza ikampa mamilioni ya fedha, hata kwa mtu Yule unayemwona ni mjinga. Kwani huenda kwa mtu yeyote Yule anayeamini akilini mwake kwamba anastahili kuzipata fedha.
Hakuna bahati au bahati mbaya, Baraka au nuksi kwenye suala zima la kupata fedha kama wengi wanavyofikiri mara kwa mara. Kuna kanuni muhimu unayoweza kuitumia kupata pesa. Kanuni hii ni kanuni ya kuamini kwamba unaweza kupata fedha. Hii ndiyo kanuni muhimu ya pesa unayotakiwa kuijua na kuitumia kila siku ili uwe tajiri.
Nadharia au kanuni hii inasema wazi kwamba, kupata fedha sio tatizo kama watu wengi wanavyofikiri. Lakini ugumu uko kwenye mawazo yetu, ambayo yamefundishwa kwamba, kupata fedha ni kazi. Kwa kuamini kwamba, kupata fedha ni kazi sana tunajikuta tunakwama mara nyingi kila tunapotafuta fedha. Kwa kutumia kanuni hii, ukiamini kuwa utapata fedha, utapata tu.

Kwa kadiri utakavyoielewa kanuni hii na kuitumia katika maisha yako, itakusaidia kujua kwamba kila mtu anauwezo wa kuwa na fedha, ikiwa mtu huyo atachukua hatua kwa vitendo kwa kujiamini yeye mwenyewe na kuamini kuwa ana uwezo wa kupata fedha. ( Soma, Hii Ndiyo Imani Unayotakiwa Kuwa Nayo Ili kufanikiwa
Kama nilivyosema mwanzo, kanuni hii anaitumia mtu yeyote hata Yule unayemwona wewe ni mjinga na kumfanikisha. Hebu fikiria, kuna wakati unaweza kusikia kwenye vyombo vya habari. ‘Fulani ametoa milioni kadhaa ili washabiki wamziki waingie ukumbini bure’. Pengine unajiuliza, hivi wenzetu fedha hizi za kuwafurahisha watu kwa dakika kadhaa tu wanazitoa wapi?

 

Kinachotumika hapa na kuwafanikisha watu hawa si kingine ni kanuni ya kuamini wana uwezo wa kutengeneza pesa upya hata wakizitumia. Kuwa na fedha nyingi hakuhitaji wewe uwe na elimu kubwa sana unachohitaji ni ufahamu sahihi juu ya pesa tu hapo utajiri ni wako.( Unaweza kusoma pia Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Pesa Zako Na kuwa Tajiri )
Kumbuka fedha haimkatai mtu hata kwa mjinga huenda tu, kama utaamini uwezo wa kupata fedha unao kweli utazipata. Kikubwa uwe tayari kuishi kwa kufata malengo na mipango yako, ili utimize ndoto zako za kuwa huru kifedha. Acha kuwa na fikra potofu za kufanya chochote ilimradi tu upate pesa hata kama kinawaumiza wengine.
Jenga ufahamu mkubwa wa fedha, jiamini na tumia kanuni hii utafanikiwa na kufika mbali katika maisha yako. Acha visingizio sasa, chukua hatua na ubadili maisha yako. Kuwa na fedha nyingi sio tatizo, tatizo ni wewe mwenyewe unajiwekea vizuizi vingi bila kujua na mwisho unajikuta unashindwa kufanikiwa na kutimiza ndoto zako.
Narudia tena, fedha siyo sababu uwezo wa kuwa nazo nyingi unao, hata mtoka kamasi anaweza kuwa nazo kama anatumia kanuni ya kumfanikisha kupata pesa. Ndiyo maana kuna watu kibao wenye fedha tele, lakini wanalewa hadi wanabebwa kama mizoga. Wengine wanahangaika kutafuta wanawake kama wamepagawa na kuwa na vurugu na uozo mwingi.
Ukiwaona nje unaweza kudhani nje ni watu wa maana. Lakini ndani mwao wameoza, wananuka. Kwao siyo maisha ya furaha kama unavyodhani wanayaona hivyo. Kwao maisha ni vurugu, hofu, mashaka na mtiririko wa kukosa ridhiko. Lakini wanapesa kwa sababu ya kuamini wanauwezo wa kuwa na pesa na kweli wamezipata.
Kwa vyovyote maisha yako yalivyo uwezo wa kuwa na pesa za kutosha na hatimaye kuwa tajiri unao, endapo utatumia kanuni hii muhimu ya pesa kukutoa pale ulipo. Hiyo ndiyo kanuni muhimu ya pesa unayotakiwa kuijua ili kuwa tajiri.
Nakutakia mafanikio mema katika safari yako ya uhuru wa kifedha, endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza zaidi.
TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0713048035/ingwangwalu@gmail.com