Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukwepa Tafrani Katika Maisha Yako.

Mara nyingi huwa inatokea ghafla na pengine bila mtu kujua, ila ndivyo tunavyojiambia tunapofanya jambo ambalo baadaye tunagundua kwamba, hatukupaswa kulifanya. Nijuavyo mimi ni kwamba, hatupaswi kutojua lile tunalofanya bila kujali mazingira yanasemaje. Sisi binadamu ni zaidi ya mazingira, lakini huwa tunajiweka chini ya mazingira. Huwa tunataka na kuhusudu sana kuwa watumwa wa mazingira.

Tunahusudu kwa sababu, hatujipi nafasi ya kukua kwa kutumia miili yetu, akili zetu, roho zetu, hisia na utambuzi wetu. Tumejifunga mahali pamoja tu, tunaamini sisi ni miili na hisia, basi. Nami ni mwanafunzi wa darasa la utambuzi (Personal Growth) na nilidhani ni suala la kufikiri tu kwamba, naweza kudhibiti hisia zangu nikitaka, kumbe ilikuwa ni zaidi ya hivyo. Ilikuwa ni kutenda zaidi kuliko kufikiri.

Siku moja nilisafiri na dalala jijini Dar es salaam na niliposhuka baada ya kufika kituoni, nilishtushwa na ujio wa kondakta wa daladala ile. Alikuja ghafla sana mbele yangu na kunizuia njia. Halafu aliniambia nimrudishie fedha zake kwa madai kwamba, alikuwa amenipa chenji ya ziada. Ukweli ni kwamba, hakuwa amenipa chenji ya ziada, bali huenda alimpa abiria mwingine, akawa amechanganya.

Bila kufikiri haraka, nilipoona anataka kunikunja shati, nilimshika na kumpiga ngwala ambapo, alianguka. Kwa bahati nzuri, dereva wake aliona tukio lile. Alimpigia kondakta wake kelele kwamba, abiria aliyemzidishia chenji sikuwa mimi. Yule kondakta aliinuka akaanza upya kumtafuta huyo abiria asiye na huruma. Baada ya tukio lile nilijiuliza kama nimekomaa au bado.


Nilijiambia kuwa bado sijakomaa. Kwa nini? Nilishindwa kutumia kwa vitendo nafasi inayokuwepo siku zote kati ya tukio na uamuzi wetu. Kati ya tukio na hatua tunayoamua kuchukua kuhusu tukio hilo, kuna nafasi kubwa. Tunapoitumia nafasi hiyo vizuri, tunajiweka katika mazingira ya kujisaidia na kujiokoa na tunapoitumia vibaya, huwa tunapalilia maumivu kuja upande wetu.

Yule kondakta hakuja kwangu akiwa ananichukia au akitaka kunionea ama akitaka kunionyesha kwamba, yeye ni mbabe. Alikuja kwangu akiamini kabisa kwamba, ameniongezea chenji. Hivyo, alikuja akiwa mtu mwema tu aliyeamini kwamba, amenipa chenji ya ziada. Kama ningeingia kweye viatu vyake, yaani ningejibainisha naye, ningeelewa hilo vizuri.

Ningejua kwamba, nisingeweza kumzuia kufikiri kwamba, ni mimi aliyeniongezea chenji. Kwa kufikiri hivyo kwanza, ningemsaidia kujua kwamba, alikuwa amekosea kunifuata mimi. Kutaka kunikunja shati pia ilikuwa naye ni majibu yake ya mazoea, siyo ya kufikiri. Ningepaswa kujua hilo kwanza, kwa sababu yeye hajui, mimi ninajua. (Soma pia njia tatu zinazoweza kukusaidia ujiamini zaidi)

Ningemsaidia kirahisi kwa kumwambia kwamba, sikuwa mimi na kumwomba anikague mifukoni kama angekuta hizo fedha. Ukweli ni kwamba, sikuwa na fedha alizodai amemwongezea huyo abiria. Ni wazi angegundua kwamba, sikuwa mimi. Lakini hata kabla hajagundua, dereva wake alimpigia kelele kama alivyofanya kwamba, sikuwa mimi huyo mdaiwa.
Kutumia nafasi iliyoko kati ya tukio na hatua tuanyochukua baada ya tukio, kunataka mazoea, kunataka kuizoesha akili na ufahamu wetu, kujua kwamba, tupo. Ni pale ambapo muda wote tunakuwepo, ndipo ambapo tunaweza kujiuliza kabla ya kuchukua hatua.  Kuwepo maana yake ni kuwa na utambuzi na kila kinachoenda kutuzunguka na ndani mwetu.

Hebu fikiria, pengine dereva wa basi lile naye angeamini kwamba mimi ndiye niliyekuwa nimeongezewa chenji, ni wazi angekuja na supana na kunipiga nayo. Huenda ningeumia na kulazwa hospitalini. Huenda ningekaa sana hospitali na kazi zangu nyingi zinge simama. Huenda kwa kushindwa kufanya kazi kwa muda familia yangu ingepata shida sana kutokana na kosa la siku moja.

Kumbuka hapa nazungumzia kushindwa kutumia nafasi ndogo sana kumaliza kila kitu kwa amani. Nazungumzia matokeo ya kufikiri kwamba, jambo lile lilitokea ghafla kiasi kwamba, sikuweza kujiuliza. Kushindwa kutumia nafasi hiyo ndogo kungeweza pengine kuniuwa au kuisambaratisha familia yangu, ambayo nayo ingezidi kuuchafua ulimwengu kwa kupanda nguvu hasi za aina mbalimbali.

Nimejifunza sasa, kwamba, hakuna kitu kinachoitwa, “nilikosea kwa sababu, jambo lilitokea ghafla, nikashindwa kuamua kwa busara na hekima”zaidi na mara nyingi kuna, kufikiri na kutenda kwa mujibu wa mazoea. Kondakta aliponisimamia mbele yangu, mazoea yaliniambia kwamba, amenidhalilisha, ameniona kibaka, ameniona dhaifu. Na mazoea yakaniambia, ‘ mwoneshe kwamba, wewe siyo dhaifu’

Kila siku au mara kwa mara huwa ni watu wa kujiambia ‘ ningejua nisingeamua vile ‘ ningejua nisingefanya makosa yale, ‘ au ningejua ningefikiri kwanza’. Ndivyo ilivyo, huwa tunagundua baada ya maumivu kwamba, tulikuwa na nafasi, lakini tukaitumia vibaya, hii yote inatokana na pengine wengi wetu kushindwa kuiona nafasi hiyo mapema na kuitumia vizuri.

Kila mtu ana nafasi ya kutumia sekunde hata moja kabla hajafanya uamuzi pale anapotokewa na jambo. Kila mmoja wetu ana uamuzi pale anapotokewa na jambo. Kila mmoja wetu ana uwezo wa kuachana na mazingira na kuwa yeye. Hatupigani na mtu aliyetutukana kwa sababu tumeshindwa kuvumilia kwa sababu katuvunjia heshima, hapana. Ni kwa sababu tumeshindwa kutumia nafasi iliyo kati ya tukio na uamuzi wetu.

Ni mara ngapi umejikuta ukijiingiza kwenye mzozo au ugomvi usio na  kwa sababu ya kushindwa kuchukua maamuzi yaliyo sahihi? Hayo ndiyo mazoea yetu, tuliyozoeshwa tangu utotoni ingawa sasa hatutakiwi kuyaendeleza tena. Tunatakiwa kuwa watu wa kufikiri kwanza ili kukwepa tafrani zisizo za lazima katika maisha yetu, na hiyo itakusaidia kuishi kwa amani na furaha.

Hivyo ndiyo unavyoweza kukwepa tafrani zisizo na lazima katika maisha yako. Tunakutakia maisha mema yenye furaha na endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza kila siku.

DAIMA TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU,
Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: