Kuna wakati katika maisha yako unaweza ukajikuta ni mtu kulaumu ndugu, jamaa na watu wengine wengi kuwa hao ndio wamechangia kukukwamisha na kukurudisha nyuma sana katika maisha yako. Ingawa ni ukweli kwamba adui mkubwa wa kwanza wa maisha yako, anayefanya mipango na malengo yako mingi isitumia mara kwa mara katika maisha yako ni wewe mwenyewe na sio mtu mwingine.

Mara nyingi tumekuwa ni watu wa kujikwamisha na kujirudisha nyuma sisi wenyewe, lakini pasipo kujua tumekuwa tukiutupia mzigo huo wa lawama kwa watu wengine kuwa ndio wamesababisha maisha yetu yawe hivyo. Kwa vyovyote vile utakavyolaumu, lakini mtu pekee anayewajibika na maisha yako ni wewe mwenyewe. Umekuwa ukijikwamisha na kujirudisha nyuma kutokana na mienendo ama maisha unayoishi. Kivipi?

Haya Ndiyo  Mambo 6 Yanayokukwamisha  Na Kukurudisha Nyuma Sana Katika Maisha Yako.

1. Kukumbuka sana mambo  yaliyopita.

Kuendelea kuweka sana kumbukumbu kwa mambo ama makosa uliyofanya na kuendelea kuumia hiyo ni sawa na kupoteza muda, pia ni moja ya jambo  linalokukwamisha na kukurudisha nyuma katika maisha yako. Nguvu nyingi ambazo unatumia kukumbuka makosa hayo ungetakiwa kuziwekeza katika kugundua nini na wapi kitu gani ufanye kipya ambacho kingeweza kukuletea mafanikio makubwa katika maisha yako. Kama unataka kuleta mabadiliko katika maisha yako, acha kushikilia na kukumbuka sana mambo yaliyopita yatakukwamisha.

SOMA; Kama unaogopa kushindwa, tayari umeshashindwa.

 
 
2. Kuendelea kuwa na mawazo hasi sana.

Mara nyingi wengi wetu huwa ni watu wa kuwa na mawazo hasi sana kwa yale tunayoyafanya na hata kwa wenzetu pia. Unapokuwa na mawazo hasi kwamba siwezi kufanya kitu hiki kwa sababu hii, ama ukawa na chuki, kisirani, choyo bila sababu yoyote, suala la kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako kitakuwa ni kitu kigumu.  Hii yote ni kwa sababu mawazo mengi hasi uliyonayo yatakuwa yanakukwamisha na kukurudisha nyuma bila kujijua. Ili kufikia mafanikio makubwa unayoyataka, achana na mawazo hasi uliyonayo kwani ni adui mkubwa wa mafanikio yako.

SOMA; Hizi ndizo fikra zinazokuzuia kufikia viwango bora vya mafanikio.

3. Kuendelea kusubiri muda sahihi.
Kuna watu ambao katika maisha yao wao ni watu wa kusubiri muda sahihi wa kutekeleza ndoto zao. Ni watu ambao huwa ni wa kujiambia nitafanya hili ama lile pale mambo na mipango yangu itakapokaa sawa. Kwa kukaa na kusubiri huku hujikuta zaidi ni watu wa kupoteza muda na hakuna lolote ambalo limekuwa likifanyika. Maisha yako hayawezi kuwa mazuri kama utakuwa mtu wa kusubiri sana muda sahihi. Anza kutekeleza mipango na malengo yako mapema kidogo kidogo, utayafikia mafanikio. Kama tu utakuwa mtu wa kusubiri muda sahihi, utakwama kufikia mafanikio makubwa.

4. Kuwaongelea watu wengine vibaya.
Hiki ni kitu pia ambacho kimekuwa kikikurudisha na kukwamisha sana katika maisha yako bila ya wewe kujijua. Kwa kawaida, unapokuwa umeamua kuchukua jukumu la kuanza kuwaongelea watu wengine vibaya hususani kwa mafanikio yao waliyonayo, uwe na uhakika utakuwa hufanyi kitu cha maana katika maisha yako, zaidi ya nguvu zako nyingi utakuwa unazielekeza zaidi kwenye kulaumu huko. Watu wengi wenye tabia hii ya kuwaongelea watu wengine kwa ubaya, mara nyingi ukichunguza huwa ni watu ambao hawana mafanikio makubwa sana katika maisha yao.

5. Kuwa na tabia ya kuahirisha mambo.
Kati ya tabia ambazo ni hatari na adui mkubwa wa mafanikio yako ni tabia hii ya kuahirisha mambo. Kazi yoyote ile hata kama ingekuwa nyepesi vipi lakini inapoahirishwa hugeuka na kuwa ngumu kuliko ile kawaida. Watu wengi huwa ni watu wa kujikuta wa kukwama na kurudi nyuma sana katika maisha yao kutokana na kuondekeza tabia hii mbaya, ambayo huwa inaua mipango na malengo yao mengi. Kama unataka kubadili maisha yako sasa, ni muhimu kwako kuachana na tabia hii ya kuahirisha mambo yako mara kwa mara, vinginevyo itakuwa ni ngumu kwako kufanikiwa.

6. Kuwa na mambo mengi sana kwa wakati mmoja.
Ili uweze kufanikiwa na kufikia malengo makubwa uliyojiwekea, ni lazima ujifunze kutekeleza lengo moja baada ya jingine hata kama una malengo mengi vipi. Unapokuwa unashikiria au kuwa na malengo ama mambo mengi kwa wakati mmoja hiyo takuwa ni ngumu sana kuweza kufikia ndoto na malengo yako uliyojiwekea. Hii itakuwa ni kwa sababu hakuna jambo utakaloweza kulifanya kwa uhakika zaidi. Kuwa na mambo mengi kwa wakati mmoja ni moja ya jambo ambalo limekuwa likiwarudisha watu wengi katika maisha yao.

Mara nyingi huwa yapo mengi ambayo kwa namna moja ama nyingine huwa yanaweza kutukwamisha na kuturudisha nyuma bila kujijua. Ili kuweza kufanikiwa na kutoka pale tulipo, ni jukumu letu sisi kuwa wa kwanza kuweza kuwajibika na kuachana na tabia ya kulaumu wengine kuwa ndio wameweza kusababisha ugumu katika maisha yetu. Chukua hatua sahihi na badilisha maisha yako mara moja.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, ansante kwa kuwa msomaji mzuri wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA na pia endelea kuwashirikisha wengine kujifunza mambo mazuri yanayoendelea hapa.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku, mpaka maisha yako yaimarike.

IMANI NGWANGWALU,

  • 0713 048 035,