Karibu msomaji kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio tunayotarajia. Maisha yetu yamejaa changamoto nyingi sana, wakati mwingine kujaribu kuzitatua mwenyewe inakuwa ni tatizo kubwa. Ndio maana unapopata ushauri wa mtu mwingine halafu ukachanganya na kile unachofikiri wewe unapata jibu zuri kwenye changamoto zako.

Leo hii tutaangalia changamoto ya kufanya kilimo wakati wewe upo mbali na eneo la kilimo. Sasa hivi kilimo kinalipa sana, hii inatokana na ongezeko la mahitaji ya mazao mbalimbali ya kilimo. Ukiwa na ardhi ambayo ipo karibu na maeneo ya miji mikubwa na ukawea kulima vitu kama matunda au mazao mengine yanayohitajika kwa wingi, unaweza kupata soko kubwa sana la mazao yako.

kilimo2

SOMA; Orodha Mpya Ya Mabilionea; Mambo Kumi Ya Kuzingati Ili Na Wewe Uweze Kuingia Kwenye Orodha Hii Siku Za Baadae.

Lakini pia kilimo kina changamoto zake kubwa sana. Sio wote wanaofanya kilimo wanapata mafanikio waliyotarajia, achilia mbali kupata hata faida tu kwa kiasi cha fedha walichowekeza.

Kuna changamoto nyingi sana kwenye kilimo, na kwa bahati nzuri mimi binafsi nimefanya kilimo hivyo nina uzoefu wa moja kwa moja.

Kabla hatujaingia kujadili changamoto ya kufanya kilimo ukiwa mbali kwanza tusome maoni ya msomaji mwenzetu.

Nina eneo la ardhi ekari 100 maeneo ya Bonde la Mto Ruvu. Nia yangu ni kuendesha shughuli za kilimo cha matunda ya muda mfupi kama matikiti,Matango na mazao ya mbogamboga kama nyanya,vitungu,bamia,biringanya nk.
Tatizo:
Sina mtu wa kusimamia kwasababu mimi ni mtumishi wa serikali.
Sina uwezo wa kununua pampu na mpira wa kuvuta maji kutoka mtoni au kugharamia uchimbaji wa kisima
Sina uwezo wa kujenga walau kibanda cha kuishi mtu wa kusimamia.

Hiyo ndiyo changamoto ambayo anaipitia msomaji mwenzetu.

Kwa kusoma maelezo ya msomaji mwenzetu hapo juu ana changamoto mbili. Ya kwanza ni kukosa usimamizi kwenye kilimo anachotaka kufanya kwa kuwa yeye bado ni mfanyakazi wa serikali. Na pili ni kukosa mtaji w akuwekeza kwenye kilimo hiko anachotaka kufanya.

Anawezaje kutatua changamoto hizi ili aweze kufikia mafanikio anayotarajia?

Kwanza kabisa changamoto kubwa ni kukosa usimamizi. Hii ni hatari kubwa sana na inaweza kupelekea kupata hasara kubwa sana. Kama huwezi kuwa na usimamizi wa karibu wa kilimo unachotaka kufanya au unachofanya ni bora kuacha kabisa kilimo hiko bila ya kujali una mtaji mkubwa kiasi gani.

Watu wengi wamekuwa wanafikiri ukishakuwa na eneo la kilimo na ukawa na fedha za kuendesha kilimo hiko basi mchezo umeisha. Utachukua watu wakae shambani wakichapa kazi wakati wewe unaendelea na mambo yako mjini, hii ina changamoto kubwa sana. Vitu kama kilimo hasa cha matunda kinahitaji usimamizi mkubwa sana, watu wakikosea tu kidogo unaishia kupata hasara kubwa sana. Unahitaji usimamizi mzuri wa hatua kwa hatua ili kuweza kupata mavuno mazuri na kufikia mafanikio.

SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Hofu/ Woga

Usimamizi mzuri wa kilimo utawezekana kama wewe binafsi utakuwa sehemu ya usimamizi huo. Hata kama haupo pale moja kwa moja ila uweze kupatikana mara kwa mara hasa wakati ambao ni muhimu kama kupanda, kuweka mbolea, kumwagilia maji na hata kuweka dawa.

Usikubali kabisa kufanya kilimo kwa kuwaachia watu shambani wafanye kazi halafu wewe wanakupa taarifa kwa simu. Watakuambia mambo mazuri na wewe utafurahia na kutuma fedha ila siku utakayofika shambani utashangaa kukuta vitu ni tofauti na ulivyotarajia.

Watanzania tumekuwa na uaminifu mdogo sana, hasa kwenye eneo la kazi. Hivyo kwa sasa sikushauri kabisa ufanye kilimo kama huna muda wa kutosha wakukisimamia, utakuwa unajiandaa kupoteza fedha ma uje kuwa sehemu ya hadithi za kushindwa kwenye kilimo.

SOMA; UKURASA WA 67; Kama Huwezi Kufanya Miaka 50 Acha..

Changamoto ya pili ya ukosefu wa mtaji, hii wala sio kubwa kama ile ya ukosefu wa usimamizi. Kwa kifupi naweza kukushauri yafuatayo kwenye kupata mtaji wa kuweza kuanzia kilimo unachofikiria, hasa kama una muda mzuri wa kukisimamia.

Unaweza kushirikiana na mtu mwingine mwenye mawazo kama ya kwako. Wewe tayari unayo ardhi, nina hakika kuna mtu mwingine ambaye ana fedha ila hajui aziwekeze sehemu gani. Ukiweza kumpata mtu wa aina hii mnaweza kuingia ubia na mkafanya kilimo hiki kwa pamoja. Angalizo; unahitaji kumjua mtu vizuri kabla hujafanya maamuzi haya makubwa ya kufanya nae kilimo na pia kujua utayari wake wa kujitoa na hata uwezo wake wa kuvumilia hasara pale mambo yatakapokwenda vibaya.

SOMA; NENO LA LEO; Tofauti Ya Kinachowezekana NA Kisichowezekana.

Unaweza pia kujichangisha mwenyewe na ukapata mtaji wa kuanzia kilimo. Kama unafanya kazi, unaweza kuanza kujiwekea akiba kiasi fulani cha mshahara wako na ukafanya hivyo kwa mwaka mmoja au hata miwili. Ukiwa na nidhamu nzuri, ukapunguza matumizi yako na hata ukaangalia njia nyingine za kupata kipato cha ziada kupitia unachofanya unaweza kupata kiasi cha fedha cha kuanzia. Nina hakika heka hizo kumi hujazipata mwaka huu, huenda umekuwa nazo kwa muda kidogo, sasa kama kipindi chote hiko ulikuwa unajikusanya leo hii ungekuwa na pa kuanzia. Sio lazima ulime heka zote 100 kwa wakati mmoja, utahitaji mtaji mkubwa sana kuweza kuwekeza hapo. Unaweza kuanza na heka kumi halafu ukaendelea kukua kuanzaia hapo.

Cha mwisho nachoweza kukushauri kuhusu kupata mtaji ni kutumia sehemu ya eneo hilo kupata mtaji. Hapa namaabsiah katika heka 100 unazomiliki unaweza kuuza sehemu ya shamba hilo na ukapata mtaji wa kuanzia kilimo. Najua hapa kwenye kuuza unaweza usipende kabisa au kuona kama unapoteza kwa sababu thamani ya ardhi inakua kw akasi sana. Lakini kama utaendelea kukumbatia ardhi hii kubwa halafu ukashindwa kuifanyia kazi, yaani kuiendeleza unaweza kujikuta unaipoteza kwa sehemu kubwa. Kama una heka 100, hujazifanyia maendeleo yoyote na wewe upo mbali, kuna siku unaweza kwenda shambani na kukuta wenyeji wameshagawana maeneo wakidhani ni msitu, na hata kama wanajua siyo wanaweza kukusumbua sana kwa sababu mambo ya ardhi yana changamoto nyingi. Hivyo kama huna njia nyingine yoyote ya kupata kipato cha kuendeleza shamba lako, naweza kukushauri uuze sehemu ya shamba hilo ili uweze kupata fedha ya kuendeleza eneo linalobaki.

SOMA; UKURASA WA 66; Dalili Za Kuanguka, Zijue Na Jinsi Ya Kuepuka.

Hayo ndio machache ninayoweza kukushauri hapa kwa changamoto hii ya kufanya kilimo ukiwa huna usimamizi wa kutosha na pia kukosa mtaji wa kutosha. Angalia kile unachoweza kuanz akukifanyia kazi na kama kauli mbiu ya mwaka huu ilivyo, JUST DO IT. Kuwa na kitu utakachoanza kukifanya mara moja ili uweze kufikia kile unachokitaka. Muda haukusubiri.

Nakutakia kila la kheri katika kutatua changamoto zako na kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322