Mawazo 8 Muhimu Unayotakiwa Kuwanayo, Ili Kuboresha Biashara Yako.

Kuna wakati unaweza ukawa unajiuliza ufanye nini, utumie njia gani ama mbinu zipi? ili uweze kuboresha biashara yako na kuiona ikiwa na mafanikio makubwa kama unavyotaka iwe. Hii ni kiu kubwa ambayo wewe mwenyewe huwa unakuwa nayo yakutamani kuona mafanikio makubwa katika biashara yako.

Lakini, tatizo kubwa ambalo huwa unakutana nalo ni nani wa kumuuliza ama atakaye kupa ushauri bora kama unaoutaka na ambao utaweza kukusaidia katika biashara yako, hapo ndipo shida huwa inapoanzia ukizingatia suala la ushauri katika jamii zetu huwa ni nadra kidogo hususani ushauri wa kibiashara.
Wengi kutokana na kukosa ushauri muhimu juu ya biashara zao hujikuta ni watu wa kuendesha biashara zao kiholela tu na matokeo yake huwa ni mabaya kwa biashara kushindwa kufanya vizuri. Katika makala hii, tutakwenda kuangalia mawazo muhimu unayotakiwa kuwa nayo ili kuboresha biashara yako na kuwa ya mafanikio makubwa. Ni mawazo yapi hayo?
Haya Ndiyo  Mawazo 8 Muhimu Unayotakiwa Kuwanayo, Ili Kuboresha Biashara Yako.
1. Fikiria kuwa mbunifu zaidi katika biashara yako.
Ili biashara yako iweze kukua na kufikia mafanikio makubwa unayoyataka kwa vyovyote vile unalazimika kuwa mbunifu kwa kazi unayoifanya. Unapokuwa mbunifu inakuwa inakusaidia kuweza kujua ni kitu gani na wakati gani wateja wako wanahitaji kitu hicho, hivyo inakuwa ni rahisi sana kwako kuweza kuwasogea huduma hiyo wanayoitaka kwa ukaribu zaidi.
Kwa kawaida wateja wengi huwa wanapenda kujaliwa na kusikilizwa zaidi. Kwa kutumia wazo la kuwasogezea huduma karibu na kuwasikiliza ni nini wanahitaji na kitu hawahitaji huo tayari ni ubunifu na hiyo itapelekea wao kuzidi kufurahia huduma yako na itakusaidia wewe zaidi kukupa mafanikio makubwa katika biashara yako. 
  
2. Jifunze biashara kila siku.
Pamoja na kuwa unafanya biashara, lakini kitu pekee kitakachoweza kuifanya biashara yako ionekane kwa utofauti na hata kuweza kufika mbali ni namna wewe utakavyoweza kujijengea hulka ya kujifunza zaidi juu ya biashara yako hiyo na sio kukaa na kubweteka. 
Kupitia kujifunza huko ndiko kutakakufanya ufikie viwango vya juu vya mafanikio. Unaweza ukajifunza kupitia vitabu, semina,  warsha au kwa wengine ili kuongeza maarifa muhimu yatakayokusaidia kuboresha biashara yako na hata kuweza kukabiliana na ushindani. Ni muhimu sana kuwa na wazo hili ili kusonga mbele zaidi.
3. Kuwa na mikakati ya baadaye Katika biashara yako.
Ni lazima uwe na wazo hili na kujiuliza mara kwa mara baada ya muda fulani utakuwa umefika wapi kibiashara. Hii itakusaidia kujua na kuweza kutambua zaidi kama unasonga mbele au unakwama mahali, ili uweze kuchukua hatua za kubadilika na kurekebisha pale unapokosea.
Hautaweza kufanikiwa sana katika biashara yako kama kweli utakuwa huna mikakati ya kujua biashara yako itakapokuwa kwa baadaye.  Hii yote inatokana na wewe, kwa kuwa utakuwa unafanya biashara yako kwa mazoea sana hali itakayopelekea ushindwe kusonga mbele. Ili kufanikiwa zaidi kibiashara ni muhimu kwako kuwa na wazo la kuweka mikakati iliyo bora.
4. Jenga fikra za kuwa king’ang’anizi.
Kitu muhimu kitakachoweza kukutoa na kukupeleka kwenye ngazi ya mafanikio unayoyataka ni kuwa king’ang’azi kwenye biashara unayoifanya na huku kusoma mazingira yanaendaje. Bila kuwa kung’ang’azi itakuwia vigumu sana kwako wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa unayoyataka.
Pamoja na kuwa kuna wakati mambo yanakuwa magumu na pengine unakuwa unakosa matumaini, jipe moyo na kusonga mbele. Acha kukata tamaa kwa chochote kile. Kwa kadri utakavyozidi kujenga nguvu ya kuwa mvumilivu na kutokukata tamaa, ndivyo utakavyojikuta unafanikiwa zaidi.
5. Kuwa na wazo la kuboresha huduma zako kila siku.
Fanya chochote kile ukifanyacho lakini tambua kuwa na huduma bora na inayopendwa na wateja ni nguzo muhimu sana kwa biashara yoyote yenye mafanikio. Unapokuwa na wazo la kuboresha huduma katika biashara yako na ukatekeleza, uwe na uhakika biashara yako itafika mbali sana.
Kampuni nyingi kubwa duniani zenye mafanikio makubwa ni zile ambazo huwa zinafanyia kazi wazo hili mara kwa mara na kupata matokeo ya kushangaza. Ni kitu hichohicho ambacho hata wewe unaweza ukafanya na kuwa na wazo la kuboresha biashara yako, ili kuleta mafanikio makubwa zaidi.
6. Kuwa na fikra chanya za kujali mteja.
Hakuna kitu kibaya kama kutokujali wateja wako ambao tena wanafanya biashara yako isimame. Wengi pengine kutokana na kutokujua huwa ni watu wa kuwapuuza wateja wao na kuwaona kama si kitu kwao. Hata kama ikatokea kuwa si mnunuzi, jaribu kumonyesha kuwa unamjali pia.
Kitendo hiki cha kutokujali wateja mara nyingi huwa kinapelekea siku hadi siku unajikuta unakosa wateja wa kutosha. Ili kuweza kuboresha hili katika biashara yako ni muhimu kujua ni lazima ujifunze kuwa na lugha tamu ambayo itakuwa kishawishi kwa wao kuja kwako tena siku nyingine.
7. Kuwa na wazo la kuifanya biashara yako ijulikane.
Usije ukajidanganya ama ukaendelea kufanya biashara yako kwa mbinu zilezile ambazo umekuwa ukizifanya siku zote, hutafika mbali. Ni muhimu kuweza kuifanya biashara yako ijulikane zaidi, ili iweze kuleta mafanikio makubwa. Na njia pekee utakayoweza kuifanya biashara yako ijulikane ni kwa kuifanyia matangazo.
Ninapozungumzia matangazo si maanishi ya redio au tv tu peke yake, hapana. Nina lenga hata kwa matangazo madogo madogo ambayo yanakuwa yapo kwenye mfumo wa vipeperushi ambayo hata kama hujiwezi sana unaweza ukayamudu. Unapofanya matangazo ni lazima biashara yako itajulikana tu. Kuwa na wazo la kuitangaza biashara yako ni kitu muhimu sana kwako.
8. Kuwa na wazo la kujali muda wa mteja pia.
Utakuwa hufanyi kitu kama utakuwa wewe ni mtu wa kuwapotezea wateja wako muda sana. Hata uwe unatoa bidhaa zako kwa ubora wa juu kama unapotezea muda wateja ni kitu kibaya sana kwa maendeleo ya biashara yako. Hebu jaribu kujiuliza unapoenda dukani kununua kitu halafu ukawa unacheleweshwa unakuwa unajisikiaje?
Kama unataka biashara yako iweze kusonga mbele zaidi ni muhimu kutambua kuwa unalazimika kuwa makini na kujali muda wa wateja sana vinginevyo utawapoteza na kuanza kujilaumu. Kutoa huduma bora ni pamoja na kujali wateja wako kwa kuwahudumia kwa muda mwafaka, hapo utaona matunda ya kile unachokifanya.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
Tunakutakia kila kheri katika safari yako ya kibiashara, iwe ya ushindi, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kujifunza zaidi kila siku.
TUPO PAMOJA,
IMANI NGWANGWALU,

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: