Habari rafiki msomaji wa makala za kilimo katika jukwaa hili la AMKA MTANZANIA. Ni matumaini yangu waendelea vizuri katika safari hii ya mafanikio. Wiki iliyopita tulijifunza kuhusu fursa katika kilimo cha bustani, tuliweza kujua nini maana ya mazao ya bustani kwa ufupi na fursa zilizopo. Kama hukusoma makala ile isome hapa; Fursa katika Kilimo cha Bustani

Kwa bahati nzuri wiki hii nimekutana na makala kwenye gazeti la ‘The Citizen’ inayohusu kile tulichojifunza wiki iliyopita. Nikasema kabla hatujasonga mbele hebu tushirikishane ripoti hiyo. Katika makala hiyo inaonyesha ukuaji wa kilimo cha mazao ya bustani, jinsi mauzo yalivyoongezeka na kiasi cha pato la kigeni kilichopatikana kutokana na mauzo ya mazao yabustani nje ya nchi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

BUSTANI

Kutokana taarifa za mamlaka ya mapato (TRA)zinaonyesha kwamba kwa mwaka jana (2014) jumla ya dola milioni 477 ($ 477 milioni) sawa na fedha za Tanzania shilingi Bilioni 858.6 zilipatikana kutokana na mauzo ya mazao ya bustani nje ya nchi. Hizi bilioni 858.6 ni zaidi ya mara 3 ya fedha za ESCROW ama kweli kilimo kinalipa sana. Hiyo hapo haijajumuisha mauzo ya ndani ya nchi ambayo kwa kawaida ndiyo yanakua mengi zaidi kuliko yanayouzwa nje ya nchi. Kwa mwaka 2013 mauzo nje ya nchi yalikua Bilioni 675, hii ikimaanisha kwamba kwa mwaka mmoja tu kumekua na ongezeko la mauzo ya shilingi bilioni 183.6 ambalo ni ongezeko la asilimia 38.

Katika biashara hili ni ongezeko kubwa sana tena kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.Katika kuongezeka huko mazao ya mbogamboga ndio yameongoza kuuzwa kwa wingi ambapo mauzo yake ni bilioni 415.80, yakifuatiwa na viungo (Bil. 226.26), maua (Bil. 147.6), mbegu (Bil. 36) pamoja na matunda (Bil. 34.56).

SOMA; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo – 2

Wachambuzi wanasema kwamba kilimo cha bustani ndio tumaini linaloibukia katika kutupatia fedha za kigeni, kikichukua nafasi ya kahawa na pamba ambaposoko lake limeanguka. Wachambuzi wanaendelea kusema kwamba kilimo cha bustani kimekua tishio kwa kilimo cha kahawa, kwa maana wakulima wengi wa kahawa sasa wamebadilisha akili zao na kuingia kwenye kilimo cha bustani, maana kilimo cha kahawa kinachukua muda mrefu, pia bei ya kahawa inathibitiwa na soko la dunia ambapo ni tofauti na mazao ya bustani. Kwa kulima kilimo cha bustani wakulima wengi wameweza kujiongezea kipato kikubwa zaidi na kwa muda mfupi ikilinganishwa na walichokua wakipata kutoka kwenye kilimo cha kahawa.

Wakati mauzo ya mazao ya bustani yakiongezeka kwa asilimia 38, hali imekua mbaya kwa upande wa kahawa na pamba kwa kipindi hichohicho cha kutokea 2013 hadi 2014. Kwa Kahawa mauzo nje yameshuka kwa asilimia 29 wakati pamba mauzo yameshuka kwa asilimia 33, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya benki kuu ya Tanzania (BOT).

Kwanza hizi takwimu zinazidi kutufungua akili kwamba fursa ya kilimo cha bustani ndio ya kufanyia kazi kwa haraka. Taarifa hii itumike kututia hamasa kwa wale ambao tayari wamewekeza kwenye kilimo na wale wanaoanza tujue kwamba tupo kwenye mstari sahihi, tupo kwenye biashara inayolipa.

Pili nipende kutoa rai hasa kwa vijana wenzangu hebu tuichangamkie hii fursa, tuache kulia kwamba ajira hakuna, tuache kukaa vijiweni na kuanza kutoa lawama kwa serikali kwamba haitupi ajira. Hizotakwimu hapo juu usizione ni kubwa, ni ndogo sana ikilinganishwa na uwezo tulio nao. Tunayo ardhi na hali ya hewa inayoruhusu kufanya zaidi hata ya mara 10 ya hapo. Pia miundombinu kila kona ipo vizuri, hii ni kwa upande wa barabara na hata viwanja vya ndege karibu kila kanda vipo kwa fursa ya uuzaji nje ya nchi. Hata kama hatutaweza kufanya mtu mmoja mmoja, tunaweza kuungana baadhi na kuanza kufanya kitu. Kumbuka mabadiliko hayaletwi na watu wengine, wala sio hao wanasiasa tunaowafikiria. Zaidi watatumia kwa kisiasa kwa faida zao baadaye tunaachwa palepale. Na pia tusifikirie kwamba mabadiliko yanatakiwa kwenye siasa tu, mabadiliko makubwa yanahitajika kwenye fikra zetu ili tufunguke akili, tujue kwamba hatima ya maisha yetu iko mikononi mwetu, tuache kupoteza muda kwa mambo ya muda mfupi huku tukiacha mambo ya manufaa kwetu.

SOMA; Haya Ndio Mapinduzi Makubwa Tunayohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Kilimo.

“Mabadiliko hayatakuja kama tunayasubiri kutoka kwa wengine au wakati mwingine. Sisi ndio ambao tumekua tukijisubiri. Sisi ni mabadiliko ambayo tumekua tunayataka” BarackObama

Naamini tukiingia kwenye fursa hii ya kilimo cha bustani kwa dhamira ya dhati kabisa nakuhakikishia kikomo chetu kitakua anga.

Kusoma habari kwenye gazeti la The Citizen waweza kubonyeza hapa.

Nawatakia kila la kheri.

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au 0658 587029 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali ba ruapepe: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713683422. http://rumishaelnjau.wix.com/editor