Hii Biashara Inaliangamiza Taifa, Tujiepushe Nayo.

Hapo zamani, alikuwepo mfalme wa nchi moja. Mfalme huyu aliwaita watu wote wenye busara kwenye nchi yake na kuwaambia naamini nyinyi ndio mna busara sana, nataka make chini na mtengeneze falsafa ya maisha ambayo kila mtu kwenye ufalme wangu ataishi nayo na itamletea mafanikio.

Watu wale wenye busara walikwenda kukaa na baada ya muda wakarudi kwa mfalme wakiwa na vitabu 12 vilivyoelezea kila kitu kuhusu falsafa ya maisha. Mfalme aliwaambia naamini mlichoandika kwenye vitabu hivyo ni kizuri sana, lakini watu hawawezi kusoma vitabu 12, ni vingi mno. Nendeni mkapunguze ili iwe rahisi kwa watu kusoma. Watu wale waikwenda kukaa tena wakarudi na vitabu sita, mfalme aliwaambia bado ni vingi mno. Wakaenda kukaa na kurudi na kitabu kimoja, bado mfalme akawaambia ni kirefu. Wakaena kukifanyia kazi na wakarudi na sura moja, bado mfalme hakukubali, alisema ni ndefu mno. Wakaenda kukaa na kuja na aya moja, bado mfalme hakuikubali. Walirudi tena kukaa na safari hii walikuja na sentensi moja tu. Mfalme alipoipokea sentensi ile na kuisoma alitikisa kichwa kwa kukubali na kusema hii ndio falsafa ya maisha ambayo kila mwananchi kwenye ufalme wangu anapaswa kuishi nayo.

Sentensi yenyewe ilikuwa inasema HAKUNA KITU CHA BURE. Kama kila mtu angeweza kuishi kw afalsafa hii, hakika tusingekuwa na matatizo makubwa ambayo yanatusumbua sasa. Hakuna kitu cha bure, ili upate kitu ni lazima ulipe gharama.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaotafuta Ajira. Soma Hapa Uone Fursa Unazoweza Kutumia.

Sasa kwa sababu ambazo hazieleweki sasa hivi watu wanaamini kwmaba wanaweza kupata kitu bila ya kutoa kitu. Watu wanaamini kwamba wanaweza kupata fedha bila ya kufanya kazi yenye kuzalisha thamani kwa wengine.

Kuna biashara moja ambayo inakua kwa kasi sana hapa Tanzania. Biashara hii inawaoa faida wachache na kuwaumiza wengi. Biashara hii inakwenda kinyume kabisa na falsafa hiyo muhimu ya maisha kwamba hakuna kitu cha bure.

Biashara ninayozungumzia hapa ni kamari iliyohalalishwa na kupewa jina la BETING. Beting ni kamari na biashara hii au mchezo huu unaliangamiza taifa. Tunahitaji kuwa makini sana, vinginjevyo tunakwenda kutengeneza taifa la ajabu sana.

Kwa nini beting ni biashara hatari sana?

1. Hakuna thamani yoyote inayozalishwa.

Ili biashara iwe halali, inahitaji kuwa inazalisha thamani kwa watu wengine. Kwa mfano mtu analima shamba, anaweka mbegu, anapalilia, anaweka mbolea anavuna kisha anauza mazao yake, huu wote ni mzunguko wa thamani. Lakini ukija kwenye beting, mtu anabashiri kwamba mchezo kati ya arsenal na liverpool, arsenal watashinda, sasa hebu niambie wewe kusema arsenal watashinda umetengeneza thamani gani?

2. Biashara hii inatengeneza uteja.

Tatizo kubwa sana la biashara hii hasa kwa wale ambao wanabet ni kwmaba kuna uwezekano mkubwa sana wa kutengeneza uteja. Kwa mfano mtu anaweka shilingi mia tano na kutabiri michezo kumi na nne, kama akipatia yote basi anapata shilingi laki moja. Baada ya michezo hiyo 14 aliyobashiri, anapatia michezo 13 na kukosea mmoja. Mtu anaona dah, nilikuwa karibu sana kuipata laki moja, ngoja nijaribu tena najua nitashinda. Hali ya namna hii inamfanya mtu kuendelea kuwa mteja na wakati mwingine kushindwa kujizuia.

SOMA; Katika Kula Ujana Usifanye Mambo Haya Matano, Utajutia Maisha Yako Yote.

3. Vijana wameanza kuichukulia kama sehemu ya kuingiza kipato.

Sasa hivi vijana wanachukulia beting kama sehemu ya kujiingizia kipato. Kijana anaitafuta shilingi elfu mbili na kwenda kubet akijua kwamba anaweza kuondoka na fedha nyingi hata mamilioni. Hizi ni akili za ajabu sana, beting haiwezi kuwa sehemu ya kipato hata siku moja. Mtu pekee mwenye uhakika wa kuingiza kipato kupitia beting ni yule anayechezesha. Yeye anachofanya ni kukusanya fedha zenu, kuondoa gharama zake za kuendesha na faida yake kisha  kuwagawia wachache kile kinachobaki.

4. Biashara hii sasa inafanyika kila mahali.

Kitu kingine kinachofanya biashara hii kuwa hatari sana ni kwamba inafanyika kila mahali mpaka kwenye mitaa ya ndani kabisa. Eneo ninaloishi mimi kuna sehemu hizi za kubet kama nne na hazipo kwenye umbali mkubwa. Hii inatoa nafasi kwa kila mtu kujiingiza kwenye mchezo huu hatarishi. Na kadiri watu wanavyosimuliana kwamba unaweza kushinda fedha nyingi, ndivyo wanavyozidi kufurika kwenye biashara hii.

Najua biashara hii sio mpya hapa Tanzania, lakini zamani ilikuwa inafanyika kwenye kumbi kubwa za starehe, Casino, na hivyo waliokuwa wanacheza hii michezo ni watu ambao wanastareheka. Ila sasa hivi imeletwa mitaani kabisa na hata asiye na uhakika wa kipato cha kesho anakwenda kubet.

SOMA; BIASHARA LEO; Usitupigie Kelele, Tupe Sababu.

5. Watoto nao wanajiingiza kwenye huu mchezo.

Ni hali ya kusikitisha sana kwamba sasa hivi hata watoto wa shule nao wanacheza mchezo huu wa kubet. Kumbuka huyu mtoto hana chanzo chochote cha kipato, ila fedha kidogo anayopewa anashawishika kwamba anaweza kuizalisha na ikawa nyingi. Sasa hatari kubwa itakuja pale ambapo watakuwa wameshakuwa wateja na wakose fedha ya kwenda kucheza, wataiba.

Hatari nyingine kwa watoto, hivi kama mtoto anafikiria kwamba anaweza kuweka mia tano, akatabiri vizuri kisha akapata laki moja au mpaka milioni, ana sababu gani ya kwenda kukaa darasani na kusoma kwa juhudi ili aweze kutengeneza kipato chake mwenyewe? Mchezo huu unaua kabisa msingi wa uwajibikaji ambao watoto wanatakiwa kujengewa. Kama mtoto atakua kwa msingi kwamba anaweza kupata fedha bila hata ya kufanya kazi, ni vigumu sana kuja kumwaminisha tofauti baadae na tunatengeneza taifa la watu wazembe kupitiliza.

Biashara hii ni hatari sana tena sana, na sababu za uhatari wake zipo nyingi sana.

SOMA; Vitu VIWILI Ambavyo Tayari Unavyo Na Vinavyoweza Kukufikisha Popote Unapotaka KWENDA.

Tufanye nini sasa ili kujiokoa na janga hili?

1. Epuka kabisa kujihusisha na biashara hii. Usibet na pia usifungue biashara ya watu kubet, utapata faida ila utaharibu taifa. Usije ukashawishika kwa namna yoyote ile kwamba unaweza kufaidika kwa kubet. Hakuna.

2. Tuwasaidie wenzetu ambao wameshaingia kwenye mchezo huu. Hii ni kazi ngumu sana lakini tusiache kuifanya. Nimekuwa nikiongea sana na vijana ninaowakuta wakibet, wengi wao wana imani kubwa sana na chochote unachomwambia kuhusu ubaya wa mchezo huu hakuamini kabisa. Huyu ni mtu ambaye amewahi kushinda mara moja au mara chache lakini ukilinganisha na idadi aliyoshindwa ni kwamba anapoteza.

3. Tupinge biashara hii. Kila mmoja wetu kwa uwezo wake, tupinge biashara hii. Tuitake serikali iondoe hii biashara mitaani na irudishwe kwenye maeneo maalumu ambayo wanaokwenda kucheza ni wale ambao wananielewa kweli. Kuiacha huku mitaani inaendelea kuharibu kabisa taifa.

Hakuna kitu cha bure, ni lazima utoe kitu ndio uweze kupata kitu. Biashara yoyote unayofikiria kufanya hakikisha inatoa thamani kwa watu wengine na kwako pia. Kinyume na hapo hiyo siyo biashara bali ni kitu hatari kinachoweza kuwaangamiza wengine.

Mafanikio hayaji kwa kukaa chini na kutabiri timu gani itashinda, mafanikio yanakuja kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuzalisha thamani. Nawatakia kila la kheri wale wote ambao wanajua kazi ndio msingi wa maendeleo. Tusikubali kuondolewa kwenye falsafa yetu hii.

TUPO PAMOJA,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

kitabu-kava-tangazo4322

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: