Kama kuna mtu yeyote unayemfahamu amemaliza kidato cha sita mwaka huu, tafadhali sana mtumie makala hii, ITABADILI MAISHA YAKE.

Siku chache zilizopita nilikutana na kijana aliyemaliza kidato cha sita mwaka huu. Tulizungumza mambo machache kuhusiana na shule, mitihani ilikuwaje na hatimaye tukaja kwenye likizo. Kwanza aliniambia hajachaguliwa kwenda kwenye jeshi la kujenge taifa. Mimi nikamuuliza una mpango wa kufanya kitu gani kwenye likizo hii. Alinijibu kwamba anafikiria kusomea kozi ya kompyuta au kozi ya udereva. Ila akaniambia tena yeye mwenyewe kwamba kompyuta hatasoma kwa sababu amekuwa akitumia kwa muda mrefu na anajua mambo yote ya msingi. Nilimuuliza tena, kama utasomea udereva unafikiri itahitaji miezi mitano? Akaniambia hapana. Nikamuuliza atafanya nini sasa kwa muda wote huo? Mwenyewe alikiri kwamba kwa miezi mitano watakayokuwa likizo, atachoka sana maana hata kwa siku chache alizokaa nyumbani ameshaanza kuchoka.
Nilimshauri kijana huyu baadhi ya mambo anayoweza kufanya katika kipindi hiki wanachosubiri kwenda vyuo vya elimu ya juu. Nimeona niwashirikishe wengine pia kupitia mtandao huu kwa sababu najua atakayefanyia kazi hiki ninachoshauri hapa atabadili maisha yake kwa kiasi kikubwa sana.
Kama wewe ni kijana ambaye umemaliza kidato cha sita mwaka huu 2015 na unasubiri kuingia kwenye vyuo vya elimu ya juu, jambo la kwanza kabisa unalotakiwa kujua ni kwamba una likizo ya miezi mitano. Vyuo vya elimu ya juu mwaka huu 2015 havitafunguliwa mpaka uchaguzi mkuu utakapofanyika na kwa kuwa uchaguzi unafanyika mwishoni mwa mwezi oktoba, vyuo vitafunguliwa mwezi novemba. Hivyo ukihesabu kuanzia mwezi huu wa sita mpaka wa kumi unapata karibu miezi mitano. Kama hujachaguliwa kujiunga na jeshi, miezi hii mitano ni mingi sana na unaweza kubadili maisha yako kabisa.
Kwa miaka saba uliyokuwa kwenye shule ya msingi, na hii sita uliyokuwa kwenye shule ya sekondari, walimu wako wamefanya kazi nzuri sana ya kukufundisha kuhusu kuhusu ulimwengu wa kazi. Walikuambia usome kwa bidii, ufaulu vizuri na utapata kazi nzuri na kuwa na maisha bora. Lakini kwa kuwa ulikuwa ‘bize’ na masomo hukupata muda wa kuangalia hali halisi ya ajira inavyoendelea. Utafaulu na kuingia chuoni lakini ndoto ulizojengewa hazipo tena, hivyo unahitaji kuwa na mtizamo tofauti kuhusiana na ulimwengu wa kazi.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ninayokushauri ufanye wakati huu wa likizo.
1.     Jifunze kutoa thamani, hili ni hitaji namba moja la mafanikio kwenye maisha.
Katika kipindi hiki cha likizo, jifunze kutoa thamani, hakuna kitu kitakusaidia kwenye maisha yako kama hiki kimoja. Tafuta kazi yoyote unayopenda kufanya au unayoweza kufanya na omba uifanye. Utakapopata nafasi ya kuifanya, ifanye kwa moyo mmoja, weka kila kitu ulichonacho kwenye kazi hiyo na thamani yako itaonekana. Kazi yoyote utakayopata usiangalie ni kiasi gani wanakulipa, bali angalia ni thamani gani unaweza kuiongeza pale. Fanya kazi sio kwa kupata kipato, bali kwa kujifunza kuhusu kazi, kujifunza kushirikiana na watu kwenye maeneo ya kazi. Kujifunza jinsi watu wanavyofanyiana majungu kwenye maeneo ya kazi, na mengine mengi ambayo yatakuandaa na ulimwengu unaokuja mbele yako.
Najua miaka karibu 20 iliyopita mingi umeitumia darasani na ulikuwa unachukuliwa kama mtoto, ila sasa hivi unaingia kwenye utu uzima na hivyo unahitaji kujifunza mambo mengi yatakayokuwezesha kufanikiwa kwenye haya maisha.
Swali kubwa utakaouliza hapa ni utapataje hiyo kazi iwapo hata waliohitimu vyuo hawapati. Jibu langu ni kwamba kazi zipo nyingi sana hasa kwa wewe unayetaka kufanya kwa muda tu na huhitaji malipo makubwa, tena usihitaji malipo kabisa, ukipata wanaokupa nauli na chakula, shukuru zaidi. Kama utakosa kabisa mahali pa kufanya kazi kwa muda nakupa njia moja ambayo haishindikani. Kwa miaka sita uliyokuwa kwenye elimu ya sekondari umejifunza mambo mengi sana. Kwenye eneo lolote unalokaa tanzania, kuna shule ya sekondari karibu(asante kwa shule za kata) na katika shule hizi kuna uhaba wa walimu na hata yale masomo ambayo yana walimu wa kutosha bado wanafunzi wanafeli.
Moja nenda kwenye shule zote zinazokuzunguka na waombe wakupatie nafasi ya kufundisha kwa muda, onesha kwamba una kitu kikubwa unataka kuwasaidia wadogo zako.
Pili kusanya watoto wa sekondari kwenye mtaa unaokaa na waambie wao au wazazi wao kwamba unafundisha tuisheni ya masomo uliyosomea wewe kidato cha tano na cha sita. Wawekee gharama ndogo wanayoweza kuimudu na hata kama ni ndogo kiasi gani wafundishe. Hapa wafundishe vizuri sana na kwa njia ambayo wataelewa vizuri kile unachowafundisha. Hii itakujenga sana kwenye kutengeneza na kutoa thamani kwa wengine. Usianze kusema mimi sijui kufundisha, mimi sina hobi ya kufundisha mimi sijui nini….. hakuna anayejua chochote, tunajifunza tunavyokwenda kwenye maisha. Na hutafanya hivi miaka yako yote, ni miezi hii mitano tu. Utakachokifanya sasa kitakusaidia sana mbeleni hata kama hakuna kikubwa unachoingiza kwa sasa.
Nakumbuka nilipomaliza kidato chasita, mtihani wa mwisho nilifanya siku ya jumanne, siku ya jumatano nilisafiri kwenda nyumbani, alhamisi nikaandika barua za kuomba kufundisha kwenye baadhi ya shule na jumatatu ya wiki iliyofuata nilianza kufundisha. Nilifundisha mpaka wiki moja kabla ya kuripoti chuoni. Nilijifunza mambo mengi sana kuhusu maisha na kazi, nilijifunza jinsi ya kutoa thamani, jinsi ya kuepuka majungu ya ofisini na mengine mengi. Na hata miaka mitatu baadae nilipopata matatizo chuoni na kusimamishwa masomo, hii ilikuwa sehemu yangu ya kwanza ya kujitengenezea kipato huku nikitafakari maisha yangu yanakwendaje.
Nakusihi sana mdogo wangu, tafuta njia yoyote ile ya kutoa thamani kwa wengine. Usiseme kwamba unahitaji kupumzika, movie unazoangalia, mitandao ya kijamii utakayoshinda unaangalia kila siku haviongezi thamani yoyote kwenye maisha yako, yaani ni sifuri.
Nilitaka nikushirikishe mengi lakini naona muda hautatutosha, nivumilie nikupe jambo jingine muhimu la pili.
2.     Soma vitabu kumi.
Katika wakati huu wa likizo, soma vitabu kumi. Yaani kumi ndio kiwango cha chini ninachokushauri, ila ukiweza endelea zaidi ya hapo. Sio kwamba nataka nikurudishe shuleni, najua ulikuwa unakesha kusoma mavitabu makubwa ili ufaulu mtihani, japo ulikuwa hupendi kusoma vitabu hivyo. Sasa nakuambia usome vitabu kumi ambavyo utavipenda na kuna mengi utakayojifunza. Vitabu hivi kumi naomba uvisome kwa utaratibu ufuatao.
Vitabu vitatu viwe vinahusiana na kile kitu ambacho unataka kusomea utakapoenda chuoni. Sio viwe vya somo, bali vinavyoelezea kuhusu kitu hiko, historia yake, umuhimu wake na hata mabadiliko yanayoendelea kuhusiana na sekta hiyo. Kama unataka kuwa daktari soma vitabu vinavyohusiana na udaktari, kama unataka kuwa mwalimu, mwanamuziki na kila aina ya kazi, tafuta vitabu vinavyohusiana na sekta hiyo na vizome. Utapata uelewa mkubwa sana wa sekta hiyo na kufikiria mara mbili kama kweli upo tayari kuingia kwenye hiyo sekta. Najua kwa sasa utakuwa umechagua sekta kwa sababu ya kufuata mkumbo au kuambiwa, ila hujapata muda wa kutosha wa kuijua vizuri sekta hiyo..
Vitabu vitatu vingine viwe ni hivi, THINK AND GROW RICH, THE RICHEST MAN INA BABYLON na RICH DAD POOR DAD. Sitatoa maelezo mengi hapa, visome vitabu hivi halafu kama utamaliza kuvisoma na kama utajali, niandikie email kwa yale uliyojifunza.
Vitabu sita tayari, vimebaki vinne.
Vitabu viwili, fikiria watu ambao unawakubali sana na siku moja ungependa kuwa kama wao. Kisha tafuta vitabu vilivyoandikwa kuhusu wao na visome. Soma vitabu hivi na jua ni changamoto gani walizipitia na jinsi gani walizivuka. Utajifunza mengi sana ambayo yatakuandaa na maisha yako ya sasa na ya baadae.
Vitabu viwili vilivyobaki soma kuhusu historia, uchumi, biashara na ujasiriamali. Kwanza tafuta kitabu kimoja kizuri sana kinachoelezea kuhusu ujasiriamali, kisome. Ni lazima utakuwa mjasiriamali kwenye maisha yako, hata kama utakuwa umeajiriwa. Tafuta kingine kinachoelezea historia ya dunia kwa ufupi, hapa nako utajifunza mambo ya msingi sana kuhusu dunia, ilipotoka na ilipo sasa.
Vitabu kumi sio vingi kwa miezi mitano, soma vitabu viwili kila mwezi, kitabu kimoja kila wiki mbili na kwa sababu vitabu vingi vina kurasa kati ya 200 mpaka 400, soma kurasa 20 mpaka 30 za kitabu kila siku na utamaliza vitabu hivyo.
Kama utapenda kujua zaidi ni vitabu gani usome, niandikie email kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Naomba kwa leo tuishie hapa, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na utajifunza mambo mengi na mazuri.
Nakutakia kila la kheri kwenye utekelezaji wa mambo haya mawili makubwa ambayo yatabadili kabisa maisha yako.
TUPO PAMOJA.