Wiki hii tunajifunza kwenye kitabu kinachoitwa LETTERS from a SELF-MADE MERCHANT to his SON. Kitabu hiki kimeandikwa na George Horace. Kitabu hiki kinahusu barua za Mfanyabiashara ambazo alikua akiziandika kwenda kwa mwanae. Tajiri huyu alikua akimwandikia mwanae toka akiwa chuoni hadi alipokua anafanya kazi na hata alipokua akipitia mambo kadha wa kadha. Barua hizo zilikua zina mafunzo mengi sana na zimegusa maeneo mengi sana ya maisha.

BARUA ZA MFANYABIASHARA TAJIRI KWA KIJANA WAKE.

 
Karibu sana tujifunze machache katika barua hizo.
1. Njia pekee ya uhakika ya mtu kupata utajiri wa haraka, ni kuupewa au utajiri wa kurithi toka kwa wazazi au ndugu. Mbali na hapo hakuna njia nyingine ya halali ya kupata utajiri wa haraka. Lazima ujiandae kufanya kazi kwa bidii, na ukubali kuanzia chini au pale ulipo. Matajiri kama kina Billgate, Warren Buffet, Mengi, Bharesa na wengine, imewachukua miaka zaidi ya 20 kufikia hapo walipo toka walipoanza kuwaza kwa habari ya kua matajiri. Utakavyoanza mapema kuweka mipango na kuitekeleza, usipofanya hivyo mwenzako anafanya hivyo na baada ya muda kutakua na tofauti kubwa na mwishowe utaanza kumuonea wivu.
2. Kuna sehemu mbili ya elimu ya chuo mtu anapata. Sehemu ya kwanza ni ile unayopata darasani kutoka kwa maprofesa, na nyingine ni ile unayopata kutoka kwa watu wanaokuzunguka, ambayo ndiyo ya muhimu zaidi. For the first can only make you a scholar, while the second can make you a man.
3. Ni rahisi kuonekana mwenye hekima kuliko kuongea hekima. Sikiliza zaidi kuliko kua mwongeaji, waache wengine wawe waongeaji zaidi, wewe sikiliza zaidi. Unapomuonyesha mtu kua unamsikiliza kwa makini, ni rahisi kukwambia kila kitu anachokijua.
4. Pesa inaongea ila tu kama mmiliki wake atakua na ulimi mlegevu wa kuongea ongea na mara zote matokeo yake hua sio mazuri. Umasikini pia unaongea japo hakuna mtu anayetaka kuusikia unasema nini.
5. Njia rahisi ya kutengeneza maadui hapa duniani ni kuajiri marafiki. Aidha kwenye biashara au hata kwenye uongozi wa kisiasa. Usiingize urafiki kwenye biashara, bishara ibaki biashara na urafiki ubakie urafiki. Usimwajiri mtu kwa kumuonea haya kamba ni rafiki yako, hii itakua ni kujitengenezea uadui. Maana kwa kawaida marafiki wanatamani wawe kwenye level sawa, na pale unapoanza kupiga hatua mbele, urafiki wenu unaanza kushika dosari. Na kwa vile anakujua ataleta kujuana kwingi kwenye kazi, na ukitaka awajibike kazini kama wengine ataanza kukuona mbaya.
SOMA; Kama Utashindwa Kufanya Chochote Utakachojifunza, Basi Fanya Hiki Kimoja Tu, Na Maisha Yako Yatagusa Wengine.
6. Usioe binti maskini aliyekuzwa kama tajiri. Mabinti kama hawa ni wale wanaotaka maisha ya matanuzi bila kujua zinatafutwa namna gani. Mfano binti anajua kipato chako, anaanza kukwambia hicho ni kidogo hakinitoshi, akipata mwenye kipato cha juu, ndio hutamuona tena. Wanataka kuishi maisha Fulani hivi, ili waonekane, fedha za kununulia cheni za dhahabu, kununulia mapambo ya dhamani, aende saluni za ghali ili tu awazidi wenziwe. Kwa ufupi ni kwamba hawana nidhamu ya matumizi ya fedha
7. Chuo hakitengenezi wajinga bali kinawaendeleza, pia chuo hakitengezi watu makini, bali kinawaendeleza tu. Mjinga atabaki kua mjinga hata akienda shule, japo akitoka atakua aina nyingine ya mjinga. Shule zinaendeleza kile ulichonacho. Lakini kukosekana kwa elimu ya chuo hakupunguzi wajinga, ila kuwepo kwa elimu kwa elimu ya chuo kunainua pia watu makini.
8. Wauzaji wazuri ni wale wenye uwezo wa kutengeneza hamu ya kula kwa wanunuzi hata kama hawana njaa. Umeshawahi kujiuliza kwa nini hua unanunua vitu hata kama ulikua huna ratiba ya kununua? Wafanya biashara wazuri wanajua jinsi ya kutengeneza hamu ya kununua hata kama ulikua huna mpango wa kununua.
9. Njia mpya ni nzuri kuliko za zamani. Katika nyanja yoyote teknolojia mpya zinarahisisha utendaji wa kazi na ufanisi, nakupelekea matokeo makubwa na ya uhakika. Mfano kwenye kilimo mkulima anayetumia jembe la mkono hawezi kupata sawa na anayetumia zana za kisasa kama trekta, na vifaa vya umwagiliaji. Ukiendelea kufanya kitu kwa njia ile ile miaka nenda rudi, utapata matokeo yaleyale. Wanaotumia njia za zamani mara zote huwatumikia wanaotumia njia mpya.
10. Mwonekano wa nje hudanganya, Shati chafu laweza kuficha moyo safi, lakini ni nadra sana kufunika ngozi safi. Ukiwa umevaa nguo zenye dosari, watu wengi wanakwenda kwenye hitimisho, kwamba hata akili yako haiwezi kua na mawazo mazuri. Watu wanaangalia smartness ya akili ya mtu kwa kuangalia amevaaje. Wakati mwingine sio kweli, mavazi ya nje hayana uhusiano na akili. Mfano tajiri wa Facebook Mr. Mark mara nyingi anavaa T-shirt, kwa mtazamo wa jamii ya sasa tungetegemea awe anapiga suti kali kila siku maana hela anayo.
11. Ulimi unaweza kusema uongo lakini macho yatasema ukweli. Mara nyingi mtu anayesema uongo ukimwangalia machoni utagundua, maana anakosa ujasiri wa kukutazama usoni.
12. Ajiri kwa taratibu na fukuza haraka (Be slow to hire and quick to fire. Katika kuajiri usifanye haraka, tumia muda kuchunguza sifa za mtu unayemtaka. Unapogundua kwamba umeajiri mtu ambaye sio sahihi fukuza mara moja. Kama sheria ya kazi inavyotaka, mlipe mshahara wake wa mwezi mmoja zaidi na haki zake nyingine kulingana na matakwa ya sheria, halafu aondoke. There are no exceptions to this rule, because there are no exceptions to human nature.
SOMA; Hiki Ndio Kinachokuzuia Wewe Kupata Kile Unachotaka Kwenye Maisha Yako.
13. Katika shughuli zako zote, kumbuka LEO ndio fursa yako, na kesho ni fursa ya mwenzako. Ukiwa na mtazamo huo utatumia vizuri muda ulionao kwa wakati huo Maana ni rahisi kuahirisha shughuli kwamba utafanya kesho. Weka juhudi katika kufanikisha shughuli zako leo bila kusubiri kesho, maana kesho sio fursa yako tena bali ni ya mwingine.
14. Mtu anakua mzuri au bora kutokana na anavyojiboresha, lakini hakuna mtu anakua bora kwa sababu babu yake alikua bora. Kwa vile baba au babu yako alifanikiwa katika maisha haina maana na wewe utafikiwa tu. Lazima uchukue jukumu la kuboresha maisha yako wewe mwenyewe.
15. Ukifanikiwa watu watasema ni bahati au umefanikiwa kama ajali (accident) ila pia ukishindwa watu watatoa unabii kwamba tulijua atashindwa tu, yaani sisi tulimwambia akajifanya mjuaji. Kwa hiyo ufanikiwe au ushindwe lazima watu watazungumza mabaya tu. Hakuna mtu atakayetambua juhudi ambazo unazifanya kufikia mafanikio.
16. Njia nzuri ya kutosheleza ladha ya mandhari ni kupanda mlima. Unapopanda mlima hua kuna njia ndefu na njia za mkato. Njia ndefu huchukua muda kufika kileleni lakini ndio salama. Ila njia ya mkato mara nyingi zinapita sehemu za hatari zenye maporomoko, kuna uwezekano ukaanguka na kufika chini mara moja. Vivyohivyo Njia ya kufika kilele cha mafanikio sio fupi lakini ndio njia salama. Hufiki juu kwa haraka, lakini pia haushuki kwa haraka. Pita njia sahihi achana na njia za mkato.
17. Usiishi leo kwa kipato/mshahara wa kesho, bali ishi leo kwa mshahara/kipato cha jana. Unapokua na matumizi makubwa kuliko kipato chako ina maana unatumia kipato cha kesho, mwishowe unajikuta unalimbikiza madeni kibao, kwa hiyo kipato cha kesho utatumia kulipa madeni ya gharama ulizotumia kuishi leo.
18. Ukikosea kuoa, itakugharimu maisha yako yote. Hili ni kosa ambalo utaishi nalo kwa kipindi chote cha maisha yako.
SOMA; Ukiendelea Na Maisha Haya Watu Watakunyanyasa Sana…
19. Mke ana nguvu kubwa sana ya kumtengeneza mwanaume kuliko hata wazazi. Mwanaume anapokua mdogo wazazi wanakua na nguvu kubwa kwake katika kum-shape, lakini akishakua mtu mzima inakua ngumu sana wazazi kumrekebisha, ila mwanaume huyo akipata mke mwema its easier keep him in order.
20. Unapokua mfanyakazi, fanya kazi vizuri sana, kiasi kwamba bosi wako ashindwe kufanya kazi bila wewe, ila wewe uwe na uwezo wa kufanya kazi hata yeye asipokuwepo. Mfano kama wewe ni meneja msaidizi, fanya kazi vizuri kiasi kwamba meneja wako atashindwa kuongoza idara yenu pasipo wewe, lakini wewe utakua unaweza kuongoza idara hata pasipo yeye. Hii ni kwakufanya kazi zako vizuri, lakini pia zile anazofanya yeye unajifunza na kuzifanya vizuri pia. Tahadhari ni kwamba usifanye kwa kuonesha unataka kushindana naye. Fanya kwa kuonyesha unataka kumsaidia ili asiwe na majukumu mengi.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe
daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com