Habari ndugu msomaji wa AMKA MTANZANIA. Leo ningependa tuangalie namna ambavyo unaweza kujijenga na kuwa na fikra chanya kila wakati bila kujali watu wanaokuzunguka au matukio ambayo yametokea na kukuvunja moyo.
Siri ya kuwa na mafanikio katika kila unalolifanya ni kuwa na fikra chanya. Ukishakuwa na fikra hasi tu, basi hata kukamilisha matamanio yako itakuwa ngumu. Ni dhahiri kuwa vile tunavyoviona nje vilianzia ndani yetu. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana kujenga fikra chanya ili kuleta matokeo mazuri ya nje/katika ulimwengu wa mwili. 

Tutaangalia baadhi ya vitu vitakavyotusaidia kutujengea fikra chanya na kama utakua na baadhi ya sababu ambazo unahisi kwako ni muhimu katika kukuongezea fikra chanya basi utaongezea na uweke katika karatasi ili kila ukiamka uzipitie, ili hali yoyote ile mbaya inapokukumba ukumbuke kuwa kuna mahala unaweza kusoma na ukarudi katika hali yako ya kawaida.
1. Kuamka mapema
Ili siku yako iende vizuri na uwe na fikra chanya ni lazima uamke mapema asubuhi. Ni vizuri kama utaamka saa kumi na moja. Muda wa alfajiri unakupa nafasi ya kupangilia mambo yako vizuri. Kama wewe ni mfanyakazi basi mpaka muda wa kwenda kazini unapofika unakua umekamilisha majukumu yako vizuri na hisia za kukimbizana kwa kuhofia kuwa utachelewa zinakuwa hazipo hivyo kukupa utulivu na hisia chanya kila wakati. Utulivu huu wa akili utakusaidia kuongeza thamani katika kile unachofanya.
SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha Ten Roads To Riches(Njia Kumi Za Kuelekea Kwenye Utajiri).
2. Kuwa na furaha
Jambo jingine la muhimu ni kuwa na furaha. Kufurahia siku yako, ratiba yako ya siku usiione kama adhabu kwako. Kuwafurahia wale wanaokuzunguka na zaidi ya yote ni kujikubali mwenyewe. Ni muhimu kufanya hivyo kwakua kama utafanya kinyume na haya utaishia kuwa na siku, wiki, mwezi na mwaka mbaya kila wakati.
3. Kukamilisha majukumu kwa wakati.
Jambo jingine muhimu ni kukamilisha majukumu yako kwa wakati. Kuna muda unaandika majukumu unayotakiwa kuyafanya lakini unajikuta kwenye shida ya kuahirisha na kuona kesho au baadaye utakuwa na muda wa kufanya shughuli ile. Tatizo ni kwamba kama hujamaliza majukumu hata ukipumzika, haupumziki kwa amani kwakua unakuwa na mawazo ya kutokamilisha lile ulilopanga. Hivyo unajikuta ukiwa na hisia mbaya na kushindwa kufanya hata shughuli nyingine. Hata kama unajisikia uvivu kiasi gani, jitahidi uanze kufanya kazi yako na kuimaliza kwa wakati. Itakupa hamasa ya kufanya mambo mengine pia utapata raha ya kupumzika na kutumia muda na wale uwapendao.
4. Kuepuka masengenyo na majungu.
Unapokuwa unajihusisha na majungu na masengenyo ni vigumu kuwa na fikra chanya. Kila unachokiona utakiona tofauti kwa kuwa akili yako imekaa katika utayari wa kubeza na kuchambua vibaya kila wakati.
5. Kulala muda wa kutosha
Tunakuwa na majukumu mengi sana kwa siku. Majukumu hayo yanatufanya tuwe na mawazo mengi sana na hivyo kuifanya akili na mwili kuchoka. Mojawapo ya vitu vinavyosababisha fikra hasi ni kuwa na uchovu na kuona kama maisha ni adhabu, majukumu ni kama utumwa na hivyo kuifanya akili kuchoka zaidi. Ni vizuri kupata muda wa kulala wa kutosha ili kuwezesha akili na mwili kupumzika na ukiamka unaanza siku ukiwa na nguvu mpya ya akili na mwili pia.
SOMA; Kama Unataka Kufanikiwa Achana Na Demokrasia Na Kuwa Dikteta.
6. Kupata muda wa kujipongeza
Mara nyingi tumekuwa tukitamani kupongezwa na watu wengine pale tunapofanya mambo mazuri. Ni jambo zuri ,lakini tumesahau kujipongeza wenyewe kwa kukamilisha majukumu yetu ya kila siku. Unapojipongeza unajihamasisha kukamilisha mambo mengine uliyojipangia. Unapojiahidi zawadi baada ya kutimiza jambo fulani unajipa hamasa ya kuzingatia kile unachokifanya. Hivyo unapata hisia chanya katika kukamilisha yale uliyojipangia.
7. Kuandika majukumu yako kwa siku na kuyafanya kwa kuzingatia muda.
Watu wengi katika ulimwengu huu tumekuwa na shughuli nyingi za kufanya kiasi kwamba unaweza kuchanganyikiwa kama ukiziorodhesha kichwani tu. Mojawapo ya njia ya kupunguza lundo la shughuli kichwani ni kuziweka katika karatasi. Andika shughuli zako katika karatasi na toa kiasi cha muda kwa kila shughuli iliyopo mbele yako. Kwa kufanya hivyo akili inakuwa katika nafasi nzuri ya kutulia na kukamilisha jukumu lililopo badala ya kufikiria juu ya shughuli ambazo bado hazijakamilika.
8. Kutotenda kinyume na imani zako/misingi yako binafsi
Kila mmoja ana imani au misingi yake binafsi ambayo ndiyo huwa chanzo cha maamuzi na matendo yake ya kila siku. Ni vizuri kufahamu ni nini misingi yako binafsi na kuisimamia ili kukufanya ujisikie vizuri kila wakati. Kama utatenda kinyume na misingi yako kwa sababu ya ushawishi wa rafiki au kikundi fulani cha watu basi lazima baada ya muda utahisi vibaya. Sio vizuri kujisaliti wewe mwenyewe kwa kufanya kinyume na vile unavyoamini kwa sababu ya msukumo kutoka kwa wengine au sababu nyingine yoyote ile.
Ni imani yangu kuwa mambo hayo yatasaidia kwa namna moja au nyingine kukujengea fikra chanya. Kumbuka kuwa fikra au hisia au mawazo huleta matokeo ya nini tufanye na vile tunavyovifanya pia hutuletea matokeo ya namna tukavyohisi/kufikiri.
Mwandishi: esther ngulwa
Mawasiliano: 0767 900 110 / 0714 900 110
estherngulwa87@gmail.com