Habari za leo rafiki?
Karibu kwenye mazungumzo yetu ya leo kama ulivyo utaratibu wetu kila siku ya jumanne na alhamisi.
Naamini unaendelea vizuri, na unafanyia kazi yale yote ambayo unajifunza. Vizuri sana kwa hilo.
Leo nataka tuzungumzie kitu kimoja ambacho nimekuwa nakiona kwa watu wengi ninaofanya nao kazi.
Watu wengi tumekuwa tukitumia muda mwingi kutafuta sababu kwa nini hatuwezi kufanya kitu fulani, badala ya kutumia muda huo kutafuta njia ya kufanya kitu hiko.
Tumekuwa watu wa kutafuta sababu za kutetea uvivu wetu au kushindwa kwetu kujituma. Na kwa sababu binadamu tunapenda kujilinganisha na wengine, tabia hii ya kutafuta sababu imekuwa inawarudisha watu wengi sana nyuma.
Nakumbuka siku nyingi kidogo rafiki yangu mmoja alikuwa anamaliza masomo yake ya chuo kikuu na aliomba tuonane ili tushauriane ni kitu gani anaweza kufanya. Tulikutana na tulizungumza mengi ambayo anaweza kuyafanyia kazi na mwishoni nikampa mfano wa rafiki yetu mwingine jinsi ambavyo anapambana na hatua kubwa aliyopiga. Baada ya kumwambia vile alinijibu yule kaweza vile kwa sababu kwao wana uwezo mkubwa na hivyo wazazi wake watakuwa wamemsaidia mtaji. Nilimuuliza una uhakika, akasema lazima itakuwa hivyo. Ambacho rafiki yangu huyu hakujua ni kwamba yule aliyedhani anafanikiwa kutokana na uwezo wa familia yake, alikuwa akifanya biashara kwa mtaji ambao alikuwa amekusanya kwa watu, na mimi nilikuwa mmoja wa watu ambao nilikuwa nimemchangia mtaji kwa makubaliano ya kulipa na riba kila baada ya muda fulani.
Ni rahisi sana kuona wengine wameweza kwa sababu fulani ambayo wewe huna, lakini nataka nikuhakikishie kitu kimoja, kama ndio unavyofikiri hivyo unajidanganya sana.
Mara nyingine nikiwa nashauri watu huwa nawapa mambo magumu kidogo kufanya, na wengine husema ni rahisi wewe kufanya hivyo kwa sababu huna majukumu ambayo ninayo mimi. Lakini ukweli ni kwamba unakuta nina majukumu mengi kuliko aliyonayo yeye au huenda majukumu yetu yanaendana.
Akili zetu ni nyepesi sana kutafuta sababu ya kujiridhisha. Na wakati mwingine tunajiridhisha kwa mambo ya kijinga sana. Kwamba yule ameweza vile kwa sababu ana hiki au kile. Mtu anaweza kusema yule anaweza kufanya biashara vizuri kwa sababu yeye ni mchaga! Na mimi siwezi kwa sababu sio mchaga. Hii ni sababu ya hovyo sana, lakini kuna wengi wanajiridhisha nayo na kuendelea kuwa na maisha mabovu.
Kitu kikubwa sana nilichojifunza ni kwamba unapomwambia mtu kitu, yule ambaye anaanza na swali nitaweza kufanyaje, ndio ambao wamekuwa wakifanya vitu vikubwa na hata ukiangalia walikotoka kuna vitu vya tofauti walivyofanya.
Lakini kama utamwambia mtu kitu halafu kwa haraka sana akaja na sababu kwa nini mpaka sasa hajafanya au kwa nini kwake yeye haiwezekani huwa hawachukui hatua yoyote na maisha yao yanaendelea kuwa vile yalivyokuwa.
Je wewe upo kwenye kundi lipi kati ya haya mawili? Upo kwenye kundi la kujiuliza unaanzaje kuchukua hatua au upo kwenye kundi la kutoa sababu kwa nini huwezi kuchukua hatua.
Naomba ujiulize swali hili na uchukue hatua leo. Kwa sababu kama umekuwa unasoma makala hizi kwa muda mrefu na mpaka sasa hakuna kilichobadilika kwenye maisha yako, moja kwa moja upo kwenye kundi la watafuta sababu. Kwa mfano umesoma kwamba kwenye kila kipato unachopata, asilimia kumi weka pembeni, hii ndio mbegu yako ya mafanikio. Wale wa kuelekea kwenye mafanikio haraka sana wanaanza kuweka pembeni, haijalishi kipato chao ni kiasi gani. Ila wale wa kushindwa sasa wanaanza risala, mimi nina kipato kidogo, mimi nina majukumu makubwa, mimi nikipata shida nitatumia hiyo ninayoweka pembeni, mimi wazazi wangu huko kijijini wananitegemea, mimi ndugu zangu wote wananiangalia, mimi….. watakupa sababu nzuri mno, ambazo zinaweza hata kukutoa machozi. Lakini hii haibadili ukweli kwamba wanajichimbia kaburi la umasikini wao wenyewe. Hakuna mtu amewahi kutajirika kwa kutegemea kipato kimoja ambacho nacho kinaishia kwenye matumizi.
Haijalishi unatoa sababu nzuri kiasi gani, haina maana yoyote, miaka mitano ijayo, sababu uliyotoa leo itakuwa ya kijinga sana, maisha yako yataendelea kuwa magumu na utazidi kujichukua.
Ufanyeje sasa kama umekuwa mtu wa sababu?
Kama umekuwa mtu wa sababu kwenye kila wazo jipya unalopata, anza kwa kubadili mtazamo wako. Anza kwa kujipa mawazo madogo madogo sana na usijipe sababu yoyote, anza kuyatekeleza mara moja. Chagua chochote kidogo sana, halafu kitekeleze haraka, bila ya kuchambua chochote. Kwa mfano tuseme unataka kuanza mazoezi, lakini umekuwa unajipa sababu, mimi sina viatu vya kukimbia, mimi muda hautoshi, mimi nitakuja kujiandikisha jimu na sababu nyingine za kijinga. Sasa badala ya sababu hizi, hebu anza kwa push up kumi, kila siku unapoamka, halafu kila siku inayofuata ongeza push up moja, baada ya mwezi utakuwa mbali sana.
Anza kuchukua hatua haraka kwenye kila wazo zuri unalopata, na unapoona sababu zinakunyemelea hamisha mawazo yako haraka sana.
Kwa kuwa huwezi kufanya kila kitu, kuwa mtu wa kusema HIKI NITAFANYA, HIKI SIFANYI. Sema hivyo tu na usiweke sababu yoyote.
Kwa mfano umepata wazo la kujiwekea akiba, jibu lako liwe, NITAANZA KUJIWEKEA AKIBA ILI MAISHA YANGU YAENDELEE KUWA BORA HATA KAMA KAZI YANGU ITAISHA. Au jibu lako liwe SITAJIWEKEA AKIBA, NIMEAMUA NIFE MASIKINI. Basi, usilete sababu yoyote kwa sababu hakuna sababu inayoweza kutetea maamuzi yoyote unayochukua.
Napenda sana kauli moja iliyowahi kutolewa na Benjamin Disraeli, anasema “Never complain and never explain.” Ukielewa hii utakuwa unafanya maamuzi yako vizuri sana na utachukua hatua ambayo utakuwa tayari kuishi nayo.
Labda utamaliza kusoma hapa na kusema, siwezi kufanyia kazi haya kwa sababu…… na kazi yangu yote ya leo itakuwa imefeli.
Nakutakia kila la kheri katika kuchukua hatua na kuboresha maisha yako. Nakutakia nguvu ya kuweza kuepuka sababu ambazo zimekuwa zinakurudisha nyuma. Uende ukawe mtu wa matendo sasa, ili maisha yako yawe bora zaidi.
MAKALA ZA KUSOMA;
- Je umekuwa kwenye ajira kwa muda mrefu na bado huoni kikubwa cha kujivunia? Soma hapa kuna mambo muhimu ya kuzingatia; USHAURI; Umekuwa Kwenye Kazi Muda Mrefu Na Huoni Mafanikio? Zingatia Mambo Haya Muhimu Sana.
- Watu wengi wamekuwa wakichanganya mawazo na fikra. Kuwa na mawazo hakukufanyi uwe unafikiria. Soma hapa ujue jinsi ya kuw ana fikra sahihi na zitakazokuletea mafanikio; Fikiria Unachofikiria….
- Hakuna kitu kinakukosesha fursa nyingi kama wewe kuwa ndio muongeaji wa kila kitu. Jifunze kusikiliza, utapata mengi sana ambayo hukuwa unayapata hapo awali. Soma hapa kujua zaidi; Kusikiliza Ni Bora Kuliko Kuongea, Mambo Sita (6) Ya Kuzingatia Ili Uwe Msikilizaji Mzuri.
- Wale wakuamini kwamba chuma ulete ndio wanawarudisha nyuma kwenye biashara, dawa ya chuma ulete iko hapa; Jinsi Ya Kudhibiti Matumizi Ya Biashara Ili Kupata Faida Kubwa.
- Kama mpaka sasa bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA unasubiria nini? Umekuwa unapitwa na mambo mengi mazuri. Hebu achana na sababu zote ambazo umekuwa unajipa na bonyeza haya maandishi, jaza fomu, tuma ada ya GOLD MEMBER na utaingia kwenye kundi zuri sana la wasap ambapo utajifunza mengi zaidi.
Hakikisha unasoma makala zote hizo, kumbuka hakuna sababu, kwamba nitasoma baadae au nikiwa na muda soma sasa. Na unaposoma ukakutana na wazo jipya, sema ninaanza kulifanyia kazi, au sitalifanyia kazi, kumbuka NEVER COMPLAIN, AND NEVER EXPLAIN.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz