Heus amicus/amica!
Quid agis?
Hapo ni habari rafiki, unaendeleaje? Kwa kilatini, unakumbuka nilikuambia mwezi huu nitajifunza kilatini? Ndio mambo yameanza, nipigie makofi kidogo. Kama wewe ni mwanaume salamu hiyo ya kwanza ingekuwa heus amicus na kama wewe ni mwanamke salamu hiyo ingekuwa amica. Kilatini kina maneno yanayotumika kwa wanaume(masculini generis), maneno yanayotumika kwa wanawake(feminini generis) na ambayo yanatumika kwa vitu visivyo na jinsia(neutra generis).
Samahani kwa kuanza na hayo ya kilatini, unaweza kuyaruka tu amicus/amica (rafiki) na kwend akupata mazungumzo ya leo hapo chini. Kama utataka kunijibu kw akilatini, niandikie Valeo! (maana yake wewe ni mzima), na unaweza kuongezea Et tu! (ukitaka kujua hali yangu pia). Pia napenda kukujulisha kwa furaha kwamba nimepata rafiki mmoja hapa wa kujifunza naye lugha hii, hivyo nafikiri mambo yatakuwa rahisi zaidi kwa sababu baada ya muda tutakuwa tunawasiliana kwa kilatini kabisa.
Kama hayo hapo juu yamekuchanganya, niwie radhi, nilitaka kukupa mrejesho kwa sababu nilikuahidi kufanya hivyo. Sasa twende moja kwa moja kwenye mazungumzo ya leo ili tujifunze na kuhamasika.
Leo nataka tugusie mafanikio hasa ni nini, kwa sababu jibu la swali hili linaweza kukupeleka mbele au kukurudisha nyuma. Nauliza swali hili kutokana na maoni aliyoniandikia msomaji mwenzetu. Yasome hapo chini kabla hatujaendelea.
Habari yako coach Makirita? ahsante Sana kwa makala ambazo zinazidi kuboresha maisha yangu. Ila naomba unitoe hofu kwa hili; nawezaje kutuma post ya mafanikio na ikiwa bado mimi mwenyewe maisha yangu yana changamoto kubwa? Vipi kwa atakayeisoma na kuangalia maisha yangu sifanani na kile nilichoandika? Naomba uitoe hofu yangu kwa hili. Ahsante.
Rafiki yetu na msomaji mwenzetu anataka kuwa anawaandikia watu kuhusu mafanikio, ila ana hofu ya kufanya hivyo kwa sababu anaona yeye bado hana mafanikio. Kwa hiyo anaona atakuwa anawadanganya watu. Nimemwelewa vizuri sana rafiki yetu huyu na naungana naye mkono kwamba kudanganya sio kitu kizuri, kwa sababu uongo una mwisho wake.
Lakini kabla sijaendelea kukubaliana naye, nataka tujiulize wote swali hili muhimu, mafanikio ni nini hasa? Kuwa na mabilioni ya fedha? Kama hilo ndio jibu lako, basi usizungumzie tena mafanikio mpaka utakapozipata. Je ni kuwa na jumba la kifahari na magari ya kifahari? Kama hilo ndio jibu basi unaweza kuacha kuandika au kuongea kuhusu mafanikio mpaka utakapovipata.
Ukweli ni kwamba mafanikio yana maana tofauti kwa watu tofauti. Kwa mfano kwangu mimi, mafanikio ni kuwa na maisha bora leo zaidi ya niliyokuwa nayo jana. Kuweza kuboresha maeneo yote muhimu ya maisha yangu, kifamilia, kifedha, kibiashara, kiroho na hata ushirikiano na wengine. Kuweza kupanga malengo na mipango na nikaweza kuifikia hata kama ni midogo kiasi gani nahesabu kama mafanikio. Kuweza kuvuka changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye maisha yangu ya kila siku haya ni mafanikio makubwa kwangu.
Na kwa sababu najua kuna watu wengi ambao wanakazana kuboresha maisha yao kama ninavyokazana kuboresha maisha yangu, najua nikiwashirikisha kile ninachofanya na ninachojifunza kwenye maisha kila siku, kwa sababu kama kinanisaidia mimi, na wao pia kitawasaidia.
Kwa hiyo mimi nina mafanikio, tena makubwa tu kwa viwango vyangu mimi, lakini kama nitajilinganisha na Ndugu Reginald Mengi naweza kujiona sio kitu, sina haki ya kumwandikia mtu kuhusu mafanikio, kitu ambacho itakuwa ni kosa kubwa sana kwangu.
Kuona kwamba maisha yako bado yana changamoto hivyo huwezi kumwambia mtu kitu kuhusu mafanikio pia ni kosa kubwa sana kwako. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye hana changamoto. Unaweza kuona watu wanavyoishi ukatamani sana maisha yao, lakini ungepewa masaa 24 tu ya kuishi maisha yao, ungeweza kusema huyawezi. Mimi mwenyewe nina changamoto nyingi mno, ambazo nikikupa zinaweza kukushinda, kila mtu ana changamoto, hivyo zisikurudishe nyuma, badala yake zitatue halafu washirikishe watu zile njia ambazo umetumia kutatua. Kama watasoma watu 100, kuna mmoja au wawili ambao watatumia njia ile na watapata majibu mazuri, watakuwa wanakufuatilia kwa makini zaidi.
Naomba kwa ufupi sana nikushirikishe mambo kumi unayoweza kuanza kufanya leo na ukawa sehemu ya mafanikio yako mwenyewe na hata kuweza kuwashirikisha wengine.
- Anza leo kuweka asilimia 10 ya kipato chako pembeni, hiyo huigusi kabisa hata kitokee kitu gani. Nilianza kufanya hivi siku nyingi zilizopita, na ninaweza kukuhakikishia, sijawahi kuwa sina hela kabisa. Yaani kwamba nimekaa sina hata fedha kidogo kwa jambo lolote haijawahi kutokea tangu nimeanza kuweka asilimia hii kumi pembeni. Haijalishi asilimia 10 yako ni kiasi gani, hata kama ni elfu moja, iweke pembeni, na iwekeze zaidi. Mwaka jana niliandika makala kuhusu mtu kuweka elfu moja pembeni kila siku na kuiwekeza kwenye UTT, wengi walipinga na kusema haiwezekani. Lakini mimi ndio ninafanya hivyo kila mwezi, sio kwa elfu moja lakini pia sio kwa fedha nyingi sana. Lakini kwa mwaka mzima uwekezaji wangu umeongezeka kwa kiasi kikubwa sana, nina mpango wa kufanya hivi kwa miaka 30 mpaka 50 ijayo, sasa haya sio mafanikio? Naweza kukuhakikishia kwa hapa dar es salaam, hasa kwa wafanyakazi, kuna mtu anaweza kuwa ameishiwa na hana fedha kabisa, anasubiri mshahara mwingine utoke ndio aishi nao. Sasa haya ni maisha hatari sana, anza wewe kuweka elfu moja pembeni kila siku, tafuta sehemu nzuri ya kuwekeza, halafu washauri watu wa aina hii kwamba inawezekana kuondoka kwenye maisha hayo ya mishahara kuwa haikutani.
- Anza kusoma vitabu vizuri vya kuongeza maarifa, angalau kwa saa moja kila siku. Hakikisha huachi hata siku moja na washirikishe watu kile ulichojifunza. Waambie tu nimesoma kwenye kitabu fulani na naanza kulifanyia kazi.
- Watangazie watu kwamba unafanya kitu fulani na wakufuatilie. Hii itakusukuma sana. Kwa mfano mimi kila siku kabla ya saa kumi na moja asubuhi inabidi niwe nimeandika makala ya kurasa, inabidi nitume ujumbe wa kuwaamsha watu kwenye kundi la wasap la wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA. Hii inanilazimu kila siku kuamka saa kumi asubuhi. Sasa kuna siku ambazo nakuwa nimechoka kweli, nakuwa natamani japo nilale kwa leo tu, lakini kwa sababu nimeshawaahidi watu nitafanya hivyo kila siku, inanibidi niamke, na nifanye hivyo. Hii ni nidhamu kubwa sana ambayo wengi hawawezi kuifanya hivyo, watu wanapoona unafanya kile unachoahidi, wanakuamini na wao wanafanya pia, hawataki kujua kwenye benki yako una shilingi ngapi.
- Anza kuandika mawazo 20 kila siku asubuhi. Fikiria tatizo lolote unalopitia kwenye maisha yako na andika mawazo 20 ya kulitatua. Ndio hakikisha ni mawazo 20 na hata kama ni ya kitoto wewe andika tu, hakuna atakayeyaona, lakini kadiri utafanya hivyo kwa muda mrefu utakuwa unatoa mawazo bora sana.
- Amka mapema kila siku. Hakikisha kila siku unaamka mapema sana, kabla dunia haijaamka. Amka angalau saa moja kabla ya muda wako wa kawaida wa kuamka, saa kumi na moja itakuwa vizuri, saa kumi itakuwa bomba zaidi. Tumia muda huu kufanya mambo ambayo ni muhimu kwako.
- Anza kufanya meditation (tajuhudi), utabadili sana fikra zako, na utaweza kufanya mengi niliyokushauri hapo juu.
- Kila siku kabla hujalala andika vitu vitatu ambavyo unashukuru kuwa navyo kwenye maisha yako. Fanya hivi kila siku, halafu washirikishe watu majibu utakayoyapata.
- Usiangalie tv, usisome gazeti, usisikilize redio kwa wiki nzima, yaani usisikilize kabisa. Na kama nyumbani kuna watu wamekaa wanaangalia tv, wewe chukua kitabu nenda sehemu nyingine na endelea kusoma. Jaribu hivi kwa wiki moja, halafu angalia majibu yake, na washirikishe watu.
- Usilalamike, ndio yaani usilalamike kabisa. Kila unapojisikia kulalamika acha mara moja na fanya kitu kingine. Kwa mfano kwa sasa umeme umekuwa unakatika karibu kila siku, na mimi kazi zangu zinahusisha sana umeme. Kuna wakati najisikia kabisa kulalamika kwamba wanachofanya sio vizuri, lakini kujilalamikia mimi hakuna kinachobadilika, umeme umeshakatwa. Hivyo ninachofanya kwa sasa umeme ukikatika nachukua kitabu cha kawaida na kuanza kusoma, kuna vitabu vingi nilikuwa navyo sijawahi kusoma, sasa nakaribia kuvimaliza, na nina mawazo mengi na mazuri kuliko mwanzoni.
- Kuwa na matumizi mazuri sana ya muda wako. Karibu kila mtu ninayemjua ana changamoto ya muda, ana vitu vingi vya kufanya lakini muda ni mchache. Lakini pia karibu kila mtu ninayemjua anapoteza muda kwa baadhi ya mambo anayofanya kila siku. Jifunze mbinu za kutumia vizuri muda na washirikishe, wale watakaozifanyia kazi na zikaleta majibu mazuri watakuwa wafuatiliaji wazuri sana wa mambo yako.
Anza na mambo hayo kumi na yafanye yote, usiache hata moja. Ni mambo magumu sana, najua lakini kama utaweza kuyafanya, nakuhakikishia kila mtu ataona una mafanikio makubwa na atapenda kufanya hivyo bila ya kujali wewe una kiasi gani cha fedha benki au unatembelea gari gani. Na ukifanya hayo, maisha yako hayatabaki kama yalivyo, kila siku yataendelea kuwa bora sana.
Kikubwa ninachokusisitiza usidanganye watu, usiwaambie watu kitu ambacho wewe mwenyewe hufanyi, nafsi yako itakusuta na watu watajua tu. Kuwa mwaminifu, kuwa mwadilifu, jitume, jijengee nidhamu. Misingi hiyo itakufikisha mbali sana.
Mambo hayo kumi sio kwa msomaji aliyeuliza tu, ni kwa kila mtu ambaye anataka kuboresha maisha yake, hebu anza kuyafanya sasa. Najua mengi ni magumu, najua utafikiria unaachaje kuangalia tv, taarifa ya habari, unaachaje kusikiliza uchambuzi wa magazeti. Lakini ukiweza kuvuka hivyo, utaweza kuvuka vitu vingi sana kwenye maisha yako.
MAKALA ZA KUSOMA;
- Rafiki yetu Daudi ametuandalia uchambuzi mzuri sana wa kitabu HOW TO LIVE ON 24 HOURS A DAY. Ni kitabu kizuri sana, nashauri kila mtu akisome, mambo mengi niliyokushirikisha hapo juu yamo humu kwenye hiki kitabu. Nilipokutana nacho mara ya kwanza nilikifurahia sana, na sasa nimeshakisoma mara tatu. Na azimio langu kwa sasa ni kila siku asubuhi lazima nikisome kitabu hiki, kila ninaporudia kusoma napata kitu kingine kipya. Ni kitabu kifupi sana, lakini kina madini adimu sana, soma uchambuzi wa kitabu hiko hapa; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha How To Live On 24 Hours A Day.
- Hivi unajua kadiri unavyofanya maamuzi mengi ndivyo unavyojizuia kuchukua hatua? Soma hapa kujua nini cha kufanya; UKURASA WA 245; Uchovu Wa Maamuzi.
- Unataka kuona fursa nyingi zaidi za kibiashara? Tumia njia hizi tano; Njia Tano(5) Za Kukuwezesha Kuziona Fursa Nyingi Zaidi Za Kibiashara.
- Leo tumekuwa tunazungumzia mafanikio hapa, nimesahau kukuambia kitu kimoja muhimu sana. Kuna kanuni ya uhakika ya kufikia mafanikio, kama unataka kuijua ili uifuate, soma hapa; Hii Hapa Ndio Fomula Ya Uhakika Ya Mafanikio.
- Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, nasisitiza sana kama unapokea ujumbe huu kila ninapotuma na hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA unakosa mengi sana. Kuna makala nzuri sana za kujifunza, unapata kuwa kwenye kundi la wasap ambapo unapata maarifa na hamasa, na gharama ni ndogo sana ukilinganisha na yale unayopata, bonyeza maandishi haya kwa maelekezo zaidi na ujiunge, utume ada na uanze kupata maarifa zaidi.
Naamini umetoka na kitu cha kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi ya yalivyokuwa mwanzo, mimi pia wakati naandika hapa nimejikumbusha kitu ambacho nimekuwa sikiwekei mkazo siku za hivi karibuni. Fanyia kazi yale ambayo unanifunza.
Vale! (kila la kheri)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.
makirita@kisimachamaarifa.co.tz