Habari ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu. Karibu tena wiki hii katika mwendelezo wetu wa uchambuzi wa vitabu Wiki hii ninakukaribisha katika Kitabu kinachoitwa The Innovator’s Dilemma (Utata wa mvumbuzi). Kitabu hichi kimeandikwa na Profesa Clayton M. Christensen, huyu ni profesa wa Usimamizi wa Biashara (Business Administration) katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani, Chuo hichi ni moja ya vyuo vikuu vinavyoheshimika sana duniani kote, hapo ndipo waliposoma viongozi wengi wa marekani kama kina Barack Obama, pia ndipo waliposoma mabilionea wa dunia, japo wengine pia waliamua kuondoka bila kumaliza shule na kufuata biashara zao, mfano ni kama Bill Gates na Mark Zuckerberg mmiliki wa Facebook. Kitabu hiki kinazungumzia juu ya Utata wa uvumbuzi wa teknolojia mpya. Kinaelezea jinsi kuibuka kwa teknolojia mpya kulivyopelekea kuanguka kwa kampuni mengi makubwa. Mwandishi anaanza kwa kuonyesha historia ya tasnia mbalimbali, na jinsi mabadiliko yalivyotokea katika sekta hizo. Mwandishi pia anaelezea sababu za kuanguka kwa makampuni hayo, na anatoa njia za kuweza kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia ili kunufaika nayo. Hapa nimekuwekea mambo 20 tu, lakini yapo mengi sana ya kujifunza. 

 
Karibu tujifunze
1. Makampuni yanategemea wateja na wawekezaji kwa ajili ya Upangaji wa Rasilimali (resource allocation). Matumizi ya fedha katika kampuni ambayo hayatapelekea kuwaridhisha wateja na wale waliowekeza kwenye hiyo kampuni (Investors), ni kwamba kifo cha hiyo kampuni ndio kimewadia. Maamuzi ya wapi pakuwekeza yanaendeshwa na uhitaji wa soko. Na hii ni moja ya utata uliopo.
2. Masoko madogo hayawezi kusaidia ukuaji wa kampuni kubwa. Kampuni nyingi ambazo ni kubwa hua haziwekezi kwenye masoko madogo, zinasubiria mpaka lile soko limekua kubwa ndipo wanaliingia. Japo kanuni hii ni Dilema, kwa maana pindi wakisubiri soko likue, anayefaidika ni Yule aliyeingia kwenye hilo soko mapema tokea likiwa dogo maana anakua ameshakita mizizi, na ameshaweka mifumo mizuri. Hivyo kampuni kubwa wakati inataka kuigia kwenye soko hilo tayari wanakua wamechelewa.
3. Masoko ambayo hayapo hayawezi kufanyiwa tathimini. Ni kawaida kwa kampuni kufanya utafiti na thamini ya masoko (market research and analysis) ili kupata picha ya uhitaji wa soko, na ni kwa kiwango gani kampuni itanufaika na uwekezaji wa kwenye soko husika. Hivyo kwa masoko ambayo hayapo inakua ngumu sana kufanya tathimini, na wakati mwingine kufanya utabiri wa soko kunaweza kua si jambo rahisi. Mfano wakati computer zinavumbuliwa, wapo waliotabiri kwamba dunia nzima zitahitajika computer tano tu, hivyo watu watakao wekeza kwenye biashara hiyo wasitegemee kufika mbali, maana hakutakua na masoko ya computer kabisa. Lakini leo hii stori ni tofauti, wale waliowekeza ndio matajiri wa dunia. Mfano mzuri ni Bill Gate yeye hakusikiliza utabiri wao.
4. Kuna tofauti kati ya uwezo wa watu na uwezo wa kampuni au shirika. Mfano mtu anaweza kua mzuri sana kwenye Kampuni X, na mtu huyo huyo akashindwa kufanya vizuri kwenye kampuni Y. Hii ni changamoto hasa kwa waajiri wengi. Kuna waajiri mfano wanaamini kwa vile Fulani anafanya kwenye kampuni X ambayo inafanya vizuri basi akimchukua na kwake atafanya vizuri. Akisahau kwamba mifumo , criteria na values za kampuni X zinazomsaidia kuweka vipaumbele na kufanya maamuzi ni tofauti kabisa na za kampuni Y. Mfano mzuri ni wachezaji, unakuta mchezaji yupo timu ya Barcelona anafanya vizuri sana, lakini anapohamia Chelsea au Arsenal kiwango chake kinashuka. Systems and Values ni tofauti, hata combination ya wachezaji ni tofauti.
5. Usimamizi mzuri wa kampuni sio guarantee ya kutokufeli kwa kampuni. Kampuni inaweza kua na uongozi mzuri na bado ikaanguka kutokana na kuibuka kwa teknolojia mpya. Meneja wengi wana pambana dhidi ya teknolojia mpya badala ya kutafuta njia ya kufaidika nazo. Menejimenti nzuri inajikita katika kuhakikisha mahitaji ya sasa ya wateja yanatimizwa. Na wakati mwingine kuhakikisha kwamba haiwekezi kwenye teknolojia mpya ambayo hazitahitajika na wateja. Hii inaweza isiwe sawa maana anachohitaji mteja leo haimanishi hichohicho atakihitaji na kesho.
SOMA; Mabadiliko; Yalikuwepo, Yapo Na Yataendelea Kuwepo.
6. Ujio Teknolojia sumbufu (disruptive technology) au teknolojia mpya kwenye tasnia yeyote unaweza kua na madhara chanya au hasi. Mfano kama kampuni inahusika na kutoa huduma za intaneti kwenye internet café, ghafla inaibuka teknolojia ya laptop na matumizi ya modem kwa ajili ya inteneti, biashara ya inteneti café itaanguka maana watu watakaa nyumbani kwao nakutumia modem. Na hata Kwa kampuni inayotengeneza modem kwa hivi sasa inaanguka, maana mtu mwenye smart phone anaweza kujiunganisha na internet kwa kutumia Tethering.
7. Sababu kuu ya kuanguka kwa kampuni kubwa ni kwamba walidharau baadhi ya kanuni au walipambana na kanuni hizo badala ya kuzifuata. Moja wapo ni ugawaji wa rasilimali (resource allocation) ambao ulikua ni tegemezi (resource dependence), ambapo wateja ndio walikua wakidhibiti ugawaji huo wa rasilimali. Yaani uongozi wa kampuni ulijikita tu katika kuwekeza kwenye zile bidhaa au huduma ambazo wateja wanazihitaji. Kama ni fedha zikaelekezwa kwenye kazi hizo, bila kua na jicho la mabadiliko ya teknolojia ambayo yangeweza kutokea. Ukijikita katika kutengeneza kile anachohitaji mteja kwa wakati huo, bila kutazama mbele, ni kitu gani atakuja kuhitaji wakati ujao, lazima kampuni itakumbwa na changamoto, pindi teknolojia mpya zitakapoibuka.
8. Sababu pili ya Kuanguka kwa kampuni kubwa ni kutokutilia maanani masoko madogo yanayoibukia. Kwa sababu ya ukubwa wa kampuni zililenga zaidi katika masoko makubwa, hivyo zile kampuni zilizokua zinaibukia na kuwekeza kwenye masoko madogo, ndizo ziliweza kunufaika nayo zaidi. Hivyo wakati yale makampuni makubwa yalipotaka kuja kuwekeza maana soko limeanza kuvutia, ikawa wameshachelewa.
9. Sababu ya tatu ni kwamba matumizi ya mwisho ya teknolojia hizo mpya (ultimate uses or applications) hayakuweza kufahamika mapema, kitu kilichopelekea kampuni kubwa kushindwa kujua umuhimu wake hapo baadaye.
10. Utoaji wa teknolojia unaweza usiwe sawa na uhitaji wa soko. Sifa zinazofanya teknolojia mpya kukosa mvuto kwenye masoko yaliyopo ndizo hizo hizo zinazopelekea kuwa na thamani kubwa katika masoko yanayoibukia. Hii ina maana sababu zinazopelekea bidhaa au huduma Fulani kukataliwa kwenye soko lililopo, ndizo hizo zinaifanya hiyo bidhaa au huduma kukubalika kwenye soko jipya.
11. Wakati wakutengeneza biashara ya teknolojia mpya, ni vizuri kutengeza au kutafuta masoko mapya kabisa ambayo yatakayoweza kuona thamani ya sifa za hiyo teknolojia mpya badala ya kuendelea kung’ang’ana kutafuta mpenyo kwenye masoko yaliyopo ili kuleta ushindani na teknolojia iliyopo. Mfano ujio wa teknolojia ya digitali dhidi ya analojia iliyokuwepo. Digitali ingepata changamoto kubwa kama sio serikali kuingilia kati na kuelekeza mitambo ya analojia izimwe. Teknolojia ya digitali mfano ingeanza sehemu ambayo hakuna kabisa hata analojia, ingekua rahisi kupata soko, kuliko kushindana kwenye soko lililopo.
SOMA; UNATAKA KULETA MABADILIKO? ANZA HIVI
12. Kutengeneza masoko mapya kuna vihatarishi kidogo (less risky) na kunalipa zaidi kuliko kuingia kwenye masoko ambayo tayari yapo, ambapo utakutana na ushindani mkubwa. Hii inafaa sana kwa kampuni ambayo ndio inakua, ila kampuni ikishakua kubwa ni vigumu kuwekeza kwenye masoko mapya maana, kampuni kubwa inahitaji soko lenye kuleta mapato makubwa ili liweze kukidhi gharama za uendeshaji ambazo ni kubwa na pia liweze kupata faida. Hii ndiyo sababu kubwa kwa nini kampuni kubwa haziwekezi kwenye masoko madogo yanayoibukia
13. Meneja ambao wanakabiliana mabadiliko ya technolojia wanapaswa kua viongozi na si wafuasi (must be leaders, not followers) hasa wakati wa kutengeneza biashara ya hizi teknolojia mpya. Hii ina maana watu hao wanapaswa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi katika kuanzisha miradi ya kutengeneza teknolojia hizo kulingana na saizi ya soko wanalolilenga. Hii ina maana ukizalisha kwa ukubwa ukazidi uhitaji wa soko, haitakua jambo sahihi hasa kiuchumi, maana gharama za uzalishaji zitakua zimetumika kubwa lakini huduma, au bidhaa zinazonunulika ni kidogo. Leadership is more crucial in coping with disruptive technologies than with sustaining ones.
14. Ubunifu (Innovation) sio kitu rahisi, ila ni kitu cha muhimu sana ili kampuni iweze kua hai. La sivyo haitafika mbali, maana wengine wakibuni, wewe ukawa unang’ang’ana na vya zamani utaachwa hapo, na anguko la kampuni haliepukiki. Mfano kampuni ya Vodacom imebuni utumaji fedha wa simu maarufu kama M-PESA, halafu Tigo na Airtel wakakosa hiyo huduma, unadhani wangeelea kupata wateja? Hata wale waliokua nao wangeenda kule kwenye ubunifu.
15. Utafiti unaonyesha makampuni mengi yaliyofanikiwa, yalitupilia mbali ile mikakati ya kibiashara ya awali (they abandoned their original business strategies) pindi walipoanza utekelezaji wa mipango yao na kujifunza kipi kinaweza kufanya kazi na kipi hakitaweza kufanya kazi kwenye soko. Tofauti kubwa kati ya kampuni zinazofeli na zinazofanikiwa haipo katika ubora wa mikakati yao ya awali. Kutengeneza mikakati mizuri mwanzoni sio muhimu katika kufikia mafanikio kama kuweza kuhifadhi rasilimali za kutosha, ili wakati biashara inapopata mpenyo sahihi uwe na rasilimali za kutosha kuzalisha hizo bidhaa au huduma. Katika kujaribu biashara, unaweza kukuta mipango ya awali iliyopangwa haifanyi kazi katika uhalisia wa utekelezaji, hivyo kubidi kubadilisha mikakati na mipango hata zaidi ya mara mbili au tatu. Sasa kikubwa katika pointi hii ni kwamba, pindi utakapogundua mkakati sahihi, je utakua umebakiwa na rasilimali za kutekeleza mipango? Kitakachoikoa kampuni hapa, ni ule uwezo wake wa kuhifadhi (conserve) rasilimali zake, au kua na mahusiano mazuri na wawekezaji wake (investors), ili kama kampuni imeishiwa na rasilimali, waweze kutoa fedha nyingine kwa ajili ya kuwekeza. Those that run out of resources or credibility before they can iterate toward a viable strategy are the ones that fail.
16. Kufeli kwa kampuni kunatokana pia na woga wa mameneja. Meneja wanaogopa kuhamasisha uzalishaji wa teknolojia mpya, maana wanaohofia pindi teknolojia hizo zitakaposhindwa kufanya vizuri sokoni, basi wataonekana wameshindwa. Hivyo kutotaka kuchafua sifa zao wao wanakomaa na teknolojia zilizopo sokoni tu maana kwa wakati huo ndio zinaingiza kipato kwa kampuni
17. Mipango katika teknolojia iliyopo na Teknolojia mpya. Katika teknolojia iliyopo mipango inafaa kuwekwa kabla ya utekelezaji maana hata utabiri (forecasts) unaweza kua sahihi. Tofauti na kwa teknolojia mpya ni kwamba utekelezaji unatangulia kabla ya kuweka mipango. Maana utabiri wa teknolojia mpya ni mgumu, na mengi hua tofauti sana na utabiri na mipango ya awali. Hivyo basi mipango kwa ajili ya kukabiliana na teknolojia mpya inapaswa kua kwa ajili ya kujifunza na si kwa utekelezaji. They must be plans for learning rather than plans for implementation. Hii itasaidia kupata taarifa sahihi za soko jipya linaloibukia.
SOMA; Hakuna Nguvu Inayopotea, Endelea Kuweka Juhudi.
18. Kukabiliana na teknolojia mpya kwa kampuni kubwa yapo mambo yakuzingatia: Kwanza jukumu la teknolojia hizo mpya linapaswa kupewa kampuni ndogo, ambazo wateja wake wanazihitaji. Mnaingia nao ubia, maana gharama za uzalishaji za kampuni ndogo ni ndogo pia kulinganisha na za kampuni kubwa. Hivyo kampuni kubwa inaweza kuingia ubia na kampuni ndogo, na kuwapatia rasilimali za awali.
19. Kampuni kubwa pia inaweza kuchagua mbinu nyingine ya kuanzisha kampuni nyingine ndogo au unaweza kuiita kampuni dada ambayo ni ndogo na inaweza kujiendesha kutokana na mapato kidogo yapatikanayo kutoka kwenye uanzishwaji wa teknolojia mpya. Hii ni kwa sababu masoko mapya ya teknolojia mpya hayana mapato makubwa, hivyo kwa kampuni ndogo itakua rahisi maana hata gharama zake za uendeshaji ni ndogo pia.
20. Usitumie rasilimali nyingi sana mwanzoni wakati unakabiliana na teknolojia mpya, maana mafanikio yake hayatabiriki. Unaweza kutumia fedha nyingi kwenye mpango ambao sio sahihi, ikifika wakati umefanikiwa kupata mkakati sahihi, unakuta umeishiwa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji.
Asanteni sana. Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com