Karibu kwenye kipengele hiki ambapo tunakumbushana mambo muhimu kuhusu maendeleo na mafanikio ya biashara zetu.

Leo tutagusia na kukumbushana eneo hili muhimu sana la biashara yako ambalo ni wateja.

Na kuna kitu kimoja muhimu sana unatakiwa kukumbuka mara zote, ya kwamba mteja yupo sahihi mara zote.

Inapotokea hali yoyote ya kutokuelewana kati yako wewe na mteja wako, basi jua ya kwamba mteja yupo sahihi. Hata kama una uhakika kabisa ya kwamba makosa ya mteja ndiyo yamepelekea hali hiyo, bado yeye anabaki kuwa sahihi.

Kwa nini mteja yupo sahihi mara zote?

Kwa sababu mteja ana nafasi kubwa ya kuchagua, na anaweza kuamua kununua kwako au kununua kwa mfanyabiashara mwingine kama wewe ambao wapo wengi sana.

Na kwa kuwa biashara za sasa karibu kila mtu anafanya, basi unahitaji kuwa makini sana na mahusiano yako na wateja wako.

Inapotokea hali yoyote ya kutokuelewana baina yako na mteja wako, badala ya kutaka kubishana, au kumwonesha amekosea, tafuta kujua ni kipi hasa kinaendelea kisha pendekeza suluhisho ambalo litakuwa bora kwenu wote, mteja apate kile anachotaka na wewe uuze kile unachouza.

Ukitaka kubishana na mteja, kumwonesha kwamba yeye ndiye mwenye makosa, mara zote yeye ndiye atakayeshinda. Kwa sababu hata kama utamshinda kwa kumwonesha amekosea, atakachofanya ni kutokuja tena kwenye biashara yako. na kwa dunia hii ya utandawazi, ana nafasi ya kuwaambia wengine pia nao wasije kwenye biashara yako.

Hivyo jua mteja mara zote yupo sahihi, na hujui hili ili kukubali akunyanyase, bali ujue ni jinsi gani ya kuboresha mahusiano yako na wateja wako na mwisho wa siku wote mfaidike.

Kila la kheri kwenye ukuaji wa biashara yako.

Kwa lolote ambalo ungependa tuliandikie hapa kwa ufupi weka kwenye maoni hapo chini.

TUPO PAMOJA.