Ni furaha tena, huenda umeshachoka kusikia kuhusu furaha, lakini nikuambie kitu kimoja, maisha yenye maana ni yale maisha yenye furaha. Maisha bora na yenye mafanikio ni maisha yenye furaha. Na kwa kumaliza kabisa nikuambie kwamba dunia imeendelea kiteknolojia kiasi kwamba sasa wanadamu tunajua jinsi tunavyoweza kupeleka vyombo kwenye sayari za mbali, lakini hatujui jinsi ya kuwa na furaha kwenye maisha yetu. Hivyo tutaendelea kusikia hili la furaha na kujifunza mara kwa mara.
Furaha, kama ambavyo tumekuwa tunasema inaanzia ndani ya mtu mwenyewe. Kitu chochote ambacho hakianzii ndani yako hakiwezi kukupa furaha, na hata kama kitakupa, basi haitadumu. Furaha ya kweli na ya kudumu inaanzia ndani yako mwenyewe. Hii ina maana kwamba kama tunataka kuwa na furaha, basi tukazane na vile vitu ambavyo vinaanzia ndani yetu wenyewe. Lakini je ni vitu gani vinaanzia ndani yetu wenyewe?
Kutoa kwa wengine kunatuletea furaha, lakini huwezi kutoa kama hakuna wengine, hivyo furaha hii inategemea uwepo wa wengine, haiwezi kutoka kwako moja kwa moja.
Kuwa katikati ya marafiki huku mkipiga hadithi na kukumbushana mlipotoka kunakuletea furaha, lakini hili linategemea uwepo wa wengine. Wasipokuwepo, kama hukuwa na furaha hutakuwa na furaha.
Vitu vingi tunavyofanya kwenye maisha vinategemea wengine ndiyo furaha yetu ikamilike, hata tunapovaa ili tupendeze, lengo ni wengine watuone, au tunaponunua vitu vya kifahari, lengo hasa ni wengine watuone.
Sasa kuna kitu kimoja ambacho kinatoka ndani yako mwenyewe na hakitegemei sana uwepo wa wengine. Kitu hicho ni HEKIMA. Hekima inaanza na wewe mwenyewe, na siyo lazima kuwepo na wengine ndiyo uweze kuwa na hekima. Unachagua kuwa na hekima ambayo itakuwezesha kufanya maamuzi bora ya maisha yako, kufanya kile ambacho umechagua kukifanya kwa ufanisi mkubwa na kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Misingi Minne (4) Ya Maisha Ya Wema.
Unachagua kuwa na hekima kwa kujifunza kila siku kwenye kila unachopitia, kisha kufanyia kazi yale ambayo umejifunza.
Kama unataka kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha, kuwa na HEKIMA, haijalishi upo kwenye hatua ipi kwenye maisha, haijalishi unafanya shughuli gani kwenye maisha yako, HEKIMA itakufungulia milango mingi kwenye maisha yako na itakuletea kuridhika na maisha yako.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)