Watu wengi wamekuwa na mazoea ya kufanya biashara siku hadi siku kwa ajili ya kuingiza kipato kupitia biashara zao, lakini si kwa ajili ya kukuza biashara hizo kwa kiwango kikubwa hadi kufikia hatua ya kupata utajiri na kujitegemea kifedha. Wapo wengine ambao wamekuwa wakijaribu kujitumbukiza katika kusaka utajiri huo bila kujua chochote ni namna gani huo utajiri unatafutwa .
Watu hawa hawana kosa, hawakupewa siri ya kutengeneza pesa kupitia biashara zao na kujenga utajiri zaidi ya kukaa tu na kusubiri pengine faida kidogo wanayoipata. Ili kuwa tajiri huna budi kuwa na zana zinazotakiwa katika kuusaka huo utajiri.
Katika makala haya utajifunza kanuni za msingi ambazo unaweza kuzitumia katika kukuza biashara yako na kujijengea uwezo binafsi wa kutengeneza pesa na hatimaye kuwa tajiri. Kanuni hizo ni zipi?
Zifuatazo ni kanuni za msingi zitakazo kuongoza katika kukuza biashara yako na hadi kuufikia utajiri:-
1. Unapopata kiasi chochote cha pesa weka kidogo kama akiba.
Huna budi kutunza asilimia kumi ya kile unachochuma. Jilipe wewe kwanza, kwa faida ndogo unayoipata kupitia biashara zako. Weka kwenye kisanduku hela hiyo hata kama ni kidogo kwani ndiyo malipo yako wewe mtafutaji. Hiyo itakuwa akiba yako ya baadae. Utajikuta hela hiyo baada ya miaka mitatu au mitano itakuwa nyingi kiasi cha kwamba itakusaidia kuweza kufungua miradi mingine unayotaka kuanzisha.

 2. Dhibiti matumizi yako.
Hata uwe unaingiza faida nyingi vipi kama unashindwa kudhibiti matumizi yako biashara hiyo haitaweza kukua zaidi ya kiwango cha sasa. Maana ukiwa na matumizi ya ovyo itapelelekea wewe kupoteza pesa nyingi ambazo zilikuwa hazina sababu ya kupotea na pengine zingekusaidia kuwekeza katika eneo lingine.
Kitu cha kufanya ili uweze kudhibiti matumizi yako ni lazima kuwa na vitabu muhimu ambavyo vitakusaidia kuweka rekodi na hasa bajeti katika biashara yako kama Kitabu cha mapato na matumizi, Kitabu cha kuonesha ukwasi, na Kitabu cha bajeti. Kudhibiti matumizi ni njia mojawapo bora ya kukusaidia kukuza biashara yako ikiwa utaizingatia vizuri.
3. Jiwekee vyanzo vingine vya fedha.
Kama biashara yako imekuwa kubwa kabisa, huna haja ya kuendelea kufanya biashara hiyo peke yake. Tengeneza vyanzo vingine vya fedha, yaani kuwa na miradi mingi ambayo haikutegemei mpaka uwepo katika utendaji itakusaidia wewe kukupa muda wa kutosha kwa ajili ya kufikiri mipango mipya na udhibiti. Hata pale miradi yako inapokuwa inaenda kombo au vibaya inakuwa ni rahisi sana kutambua.
Vitega uchumi ambavyo utakuwa navyo vitakusaidia sana kukuza biashara zako mara dufu na zaidi kuongeza pato lako. Hii itakusaidia sana kuufikia utajiri unaoutafuta labda pengine nia hiyo uwe huna. Kwa hiyo, kukuza biashara na kuzitengenezea matawi ni suala la muhimu sana ambalo unatakiwa kulitambua kwamba linasaidia kukuza biashara zako kwa kasi kubwa.
4. Tunza mtaji wako.
Utakuwa hufanyi chochote cha maana kama utakuwa unapunguza mtaji wako. Kama umepata hasara katika biashara zako na unaona hasara hiyo inaweza kukata mtaji wako, basi hakikisha unakata gharama zisizo za lazima ili faida ndogo inayopatikana iweze kufidia hasara inayotaka kukata mtaji wako.
Usiwekeze kwa pupa fanya kwanza uchunguzi ukishaona biashara inalipa ndo ufanye au nenda kawaulize wataalamu wanaoijua hiyo biashara, vinginevyo bila kuwa makini katika hili utajikuta badala ya kukuza biashara yako ili ikuletee faida unaiua.
5. Uwe makini unapokopesha.
Katika bishara yako ili iweze kukua na kukutengenezea pesa ya kutosha huwa yapo mambo mengi sana unayotakiwa kuwa nayo makini. Mojawapo ni namna unavyokopesha Angalia unapokopesha usikopeshe wasiokopesheka. Kukopesha isiwe fimbo ya kujipigia mwenyewe kwenye biashara yako. Siyo lazima ukopeshe hata kama kuna ahadi na dalili nzuri za kulipwa kwa riba kubwa. Ukiwa makini katika hili pia utamudu kukuza biashara yako.
6. Ongeza uwezo wa kuendelea kupata pesa kupitia biashara yako.
Ni watu wachache wanaosoma baada ya kumaliza shule. Kama utaacha kuunoa ubongo wako kabisa lazima ujue utakwama. Lazima kuunoa ubongo wako kila wakati kwa kujisomea,kushiriki kwenye semina za biashara, na mambo kama hayo. Usiposoma ubongo wako utaota kutu na kamwe hutasonga mbele kwani itafika wakati utashindwa kukabiliana na changamoto hata ndogo tu zinazojitokeza kwenye biashara yako.
Uwezo wa kufanikiwa na kufika pale zaidi ya ulipo unao, unaweza ukatumia kanuni hizo kama msingi wa kujijengea namna unavyoweza kukuza biashara yako hadi kufikia utajiri.   
Kwa mbinu au kanuni zingine za biashara na mafanikio utaendelea kujifunza hapa hapa kwenye gazeti mtandao huu wa AMKA MTANZANIA, kwani kumbuka elimu haina mwisho, nakutakia mafanikio mema na tukutane wiki ijayo kwa makala nyingine nzuri.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,