Kila mtu anayeomba ushauri huwa anaomba kushauriwa ni kitu gani rahisi anachoweza kufanya ili kufanikiwa.
Mtu atakuambia hebu nishauri ni biashara gani ninayoweza kufanya na isinisumbue ili niweze kufanikiwa?

Au mwingine atakuuliza ni kazi gani nifanye sasa ambayo haitakuwa na usumbufu kwangu na itaniletea mafanikio?
Unajua jibu ni nini? Jibu ni hakuna. Hakuna kazi yoyote ambayo unaweza kufanya isiwe na changamoto na matatizo yake. Hakuna biashara yoyote unayoweza kufanya ikawa mteremko tu, kila kitu kinaenda kama unavyotaka.
Na muhimu zaidi, hakuna maisha ambayo ni rahisi na yanakwenda kama unavyotaka, iwe ni maisha yako binafsi au maisha ya familia.
Changamoto na vikwazo vipo kwenye kila kitu unachojaribu kufanya kwenye maisha yako.
Swali jingine muhimu ni je uache kufanya chochote kwenye maisha kwa sababu kina vikwazo? Je mafanikio hayawezekani tena kwa sababu kile tunachotaka kina vikwazo?
Majibu ni hapana, usiache kufanya kwa sababu kuna vikwazo. Na hapana, siyo kwamba mafanikio hayawezekani kutokana na vikwazo.
Ukweli ni kwamba, mafanikio ni kutafuta vikwazo ambavyo unaweza kuvivuka, ni kutafuta changamoto ambazo unaweza kuzitatua na ukatatua changamoto hizi vizuri.
Mafanikio kwenye biashara ni kufanya biashara ambayo unaweza kukabiliana na vikwazo na changamoto zake. Iwe ni kwenye ufanyaji wa kazi, muda, ushirikiano na wengine na mengine mengi.
Mafanikio kwenye kazi ni kufanya kazi ambayo upo tayari kukabiliana na changamoto za kazi hiyo. Iwe ni uchovu, kukosa muda, kipato kidogo na mengine.
Na hata mafanikio kwenye ndoa ni kuishi na mtu ambaye upo tayari kukubaliana na changamoto zake. Kwa sababu kila mtu ana changamoto zake.
Hayo ndiyo mafanikio rafiki yangu, siyo lele mama, siyo mteremko. Chagua mwenyewe kipi upo tayari kuteseka nacho, kipi upo tayari kupambana nacho, na hakuna yeyote atakayeweza kukuzuia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK