Habari za leo rafiki?

Karibu kwenye kipengele chetu cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia sisi kufikia mafanikio makubwa. Kupitia kipengele hiki unaniandikia changamoto inayokusumbua na mimi nakushauri hatua sahihi unazoweza kuchukua ili kuondokana na changamoto hizo.

 

Changamoto ni sehemu ya maisha yetu, hivyo hatupaswi kuzikimbia u kuziogopa, bali kujifunza kupitia changamoto hizo ili kuwa bora zaidi.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kuwakopesha watu fedha halafu wanashindwa kukulipa. Je unawezaje kuondokana na hali hii? Tutajifunza kupitia changamoto ya msomaji na rafiki yetu, kama alivyotuandikia.

SOMA;  USHAURI; Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Madeni Mabaya.

Habari coach.
Changamoto yangu kubwa ni kuwa na huruma sana iliyopitiliza ambapo mtu akiwa na shida na kuja kwangu na kukopa pesa basi ni lazima nitampa hata kama nina hela ya mtu ili mradi tu ananiahidi kuwa atalipa. Hii imenipelekea kuwakopesha watu wengi zaidi ya milioni 10 kwa kiasi tofauti kwa kila anayekuja. Matokeo huu ni mwaka wa 3 sasa hizo pesa sijalipwa naishia kugombana na watu tu. Nisaidie kuondokana na tatizo hili. Kwani imefika mahali sasa mambo yangu yote hayaendi tena wengine wananiendea kwenye imani za kishirikina ili nisahau kuwadai. Pia ninapowadai napata sana taabu ya kuishia kwenye beef na mtu pamoja na familia zao. Clara F. N

Clara kwanza kabisa nikupe pole kwa changamoto hiyo unayopitia, ni hali ya kuumiza sana pale unapomwamini mtu na kutoa msaada halafu msaada wako unaishia kukuumiza wewe mwenyewe. 

Ni haki yako kabisa kupata fedha zako ambazo umewapa watu hao na inaumiza pale unaposhindwa kutimiza mipango yako mingine kutokana na watu kushindwa kutimiza walichoahidi.

Lakini pamoja na matatizo hayo ya watu, wewe mwenyewe umechangia kuingia kwenye matatizo hayo, na hivyo napenda tuanzie hapo, tuanze na wewe kwanza. Ili ujifunze na hili lisirudie tena kwako.

Kuhusu tabia yako ya kukopesha kwa urahisi.

Iko hivi, binadamu wanapenda kupata kitu kwa urahisi, hivyo kwa namna yoyote ile wamekuwa wakitafuta njia rahisi ya kutimiza mahitaji yao. Na wanapoipata njia hiyo wanawaambia na wengine pia, kama ulivyo msemo kizuri kula na wenzio.

SOMA; Njia Ya Uhakika Ya Kuondokana Na Madeni Sugu Na Kufikia Uhuru Wa Kifedha Kwenye Maisha Yako.

Sasa hiki ndiyo watu wamekuwa wakifanya kwako, wanajua una udhaifu wa huruma, unaweza kumsikiliza mtu na ukamhurumia bila hata ya kuhoji wewe ukachukua hatua ya kumsaidia. Hivyo kesho atakuja tena na hadithi yenye huruma zaidi na wewe utasaidia. Na kibaya zaidi watawaambia wenzao pia na wao watakuja na hadithi zenye huruma na wewe utaishia kukubaliana nao na kuwakopesha.

Hivi ndivyo umetengeneza matatizo hayo ya kifedha mpaka kufikia kiwango hicho cha milioni 10.

Ukweli ni kwamba uliwakopesha watu fedha bila ya kujiridhisha iwapo wanazihitaji kweli, na kama wanazihitaji kweli basi hukujiridhisha kama wanaweza kuzilipa. Na hivyo kufanya kosa kwako na kwa wao pia. Kwa kifupi iko hivi, watu wanapenda fedha za kupata kiurahisi, hivyo wakiona mwanya huo wanautumia, hawataki kujali watakuja kuzilipaje. Hivyo kwa kuwa wewe ulikuwa unatoa kiurahisi, hata wale ambao walikuwa hawana uhitaji mkubwa sana na wao walishawishika kukukopa, na kama ni ndugu basi ulichochea zaidi.

Unafikiri kwa nini benki huwa haziwakopeshi watu kirahisi? Kwa sababu wanajua kusingekuwa na masharti kila mtu angekimbilia kuchukua mkopo, na wengi wa hao hawawezi kulipa mikopo hiyo kabisa.

Hivyo basi, hatua ya wewe kuchukua kwa sasa, ili kuepuka matatizo zaidi kwako, usikopeshe mtu kabisa. kwa vyovyote vile usikopeshe mtu, kama kuna mtu ana shida kweli na wewe unaona ana shida ya uhakika, ya kufa na kupona, basi msaidie. Hata kama yeye anataka kama mkopo, mpe kile kiasi ambacho hata kama hatakurudishia utakuwa umempa kama sehemu ya msaada wako kwake. Lakini kukopesha kwa ahadi ya kurejeshewa baadaye usifanye hivyo.

Yaani kataa kabisa na kama ni ndugu yako ndiyo unahitaji kuwa makini zaidi. Kama nilivyosema hapo juu, saidia pale unapoweza lakini usikopeshe. Utajikuta unazidi kutengeneza matatizo makubwa kwako na kuharibu mahusiano yako na wengine.

SOMA; Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Madeni Mabaya.

Najua hili linaweza kuwa gumu kwako, kwa kuwa utahofia watu watakuona una roho mbaya, lakini fanya hivyo. Mtu anapokuja kutaka mkopo mweleze hata wewe una changamoto za kifedha. Hii itakupa wewe uhuru wa kuweza kutekeleza mipango yako ya kifedha. Kama ipo shida kubwa saidia kadiri ya uwezo wako.

Kuhusu fedha unazodai sasa.

Kwa wale ambao unawadai sasa, mtafute kila mmoja na kaa naye chini. Mwulize kuhusu deni lake kwako na mwulize ana mpango gani wa kukulipa. Msikilize kwa makini amepanga kukulipaje, kiasi gani na kwa muda gani. Na kama hana mpango kabisa wa kukulipa mwambie akuambie hivyo. Sasa mtu akishakupa huo mpango wake wa kukulipa, mwambie muandikishiane na mtafute shahidi wa kusimamia hilo. Na kama atashindwa kutimiza kile alichoahidi basi uwe na nafasi ya kuchukua hatua zaidi. Fanya hili kwa utulivu wa hali ya juu, usiwe na jazba au kuonesha kama unataka kumkomoa, bali ongea na kila unayemdai vizuri kutaka kupata mpango wake wa kukulipa.

Iwapo mtu ameonesha hana nia ya kukulipa tena basi wewe angalia mwenyewe hatua zipi unachukua. Kama ni mimi ningeachana naye, na kuendelea na maisha yangu. Najua kuachana naye inanipa mimi uhuru wa kufanya mambo yangu na siyo kusumbuana na mtu ambaye hana mpango wowote wa kulipa. Lakini pia atakuwa ameamua kuharibu kabisa mahusiano baina yetu. 

Hivyo chagua kama utaamua kuchukua hatua au kuachana na wale ambao hawana mpango wa kukulipa.

Kuhusu kufanyiwa ushirikina ili usahau kudai.

Hii siyo kweli rafiki, hakuna anayeweza kukufanyia wewe ushirikina ili usahau kumdai. Bali wanachokifanya watu ni kucheza na hisia zako ili uone aibu kuwadai au uwaonee huruma kuwadai. Hivyo kuwa makini, fanya kama nilivyokushauri hapo juu na fuatilia kadiri mtakavyokubaliana. Kama utasahau hapo ni wewe mwenyewe na siyo ushirikina wa mtu. 

Ingekuwa watu wana uwezo wa kutumia ushirikina kwa aina hiyo, wangeutumia kukopa kirahisi benki na kusahaulisha benki isiwadai. Lakini hilo halitokei kwenye benki kwa sababu benki zinaendeshwa na taratibu na siyo hisia.

Mwisho kabisa nikutake utue mzigo huo na kuweza kupiga hatua. Hata kama watu watakubaliana na wewe kukulipa, usiweke fedha hiyo ya deni kwenye mipango yako mingine. 

Unaweza kuamua kuchukulia kama umefanya biashara ukapata hasara. Hii itakupa wewe nafasi ya kuchukua hatua mpya kwenye maisha yako, ambapo utajua kipi sahihi kufanya. Na kumbuka, usikopeshe tena, saidia pale unapoweza, lakini usikopeshe. Na kwa upande wa ndugu kuwa makini zaidi, maana hawa wanajua udhaifu wako na kuweza kuutumia kwa manufaa yao.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.