Katika maisha, hakuna aliyeanza na mafanikio makubwa  moja kwa moja, bali mafanikio hujengwa taratibu siku hadi na kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kwa juhudi za kila siku mwisho huzaa mafanikio makubwa.
Kuna wakati unaweza ukajiona huna kitu, na ukawa unapata tabu sana kujiuliza nawezaje kufanikiwa hadi kufikia mafanikio makubwa? Kama hayo ndiyo mawazo uliyonayo, tulia, uwezo wa kufanikiwa unao, hata kama huna mtaji mkubwa au ulichonacho ni kidogo.
Ni rahisi tu unaweza usianze na kikubwa sana ulichonacho  lakini ukafikia mafanikio makubwa. Kitu cha kujiuliza zipo siri gani au hatua gani ambazo unatakiwa uzifuate kama kiwango cha mtaji ulichonacho ni kidogo au umeanza na kidogo?
Fuatana nasi katika makala haya kujua hatua za kupitia ili kuanza na kidogo ulichonacho hadi kufanikiwa.
1. Chukua hatua.
Amua kitu gani unataka kukifanya, kisha anza kukifanya kitu hicho  mara moja. Kama kuna biashara unataka kuifanya na una mtaji mdogo anza na mtaji huo, naamini utakusogeza kwenye lengo lako hata kama ni kidogo.
Katika hatua hii, acha kusubiri sana kwamba hadi kila kitu kiwe kamili. Siri kubwa ya kupata mafanikio kama ulichonacho ni kidogo, anzia hapo hapo, usisubiri kesho au wakati mwingine, maana huo wakati haupo.
2. Fanya kila siku.
Kwa chochote kile ulichokichagua hapa unatakiwa kukifanya kila siku. Hapa ndipo ‘muujiza’ wa kuweza kufanikiwa kwa kidogo ulichonacho unapoanzia. Hutaweza kufanikiwa kama hutafanya kila siku.
Kile kidgo ambacho kinaokena kwa macho ya kawaida hakiwezi kukuletea mafanikio ukikifanya kila siku kinauwezo wa kukupa mafanikio. Haijalishi ni kitu gani, lakini jambo la msingi kifanye kila siku, utapata matokeo makubwa.
3. Jenga matazamo sahihi.
Kuchuku hatua na kufanya kila siku hiyo peke yake haitishi kwa wewe kuanza kidogo ulichacho hadi uweze kufikia mafanikio. Unatakiwa kuongeza kitu kingine cha ziaida ambacho ni mtazamo sahihi.
Unatakiwa kukiona kitu hicho unachokwenda kukifanya katika jicho la mafanikio. Hutakiwi kuona kama vile kitashindwa, ni muhimu sana kukiona kitu hicho kwamba lazima kitoe matokeo sahihi. Kwa mtazamo huo utakufanikisha.
4. Jitoe kwa muda mrefu.
Ili uweze kupata matokeo ya kile unachokihitaji unatakiwa kujitoa kwa muda mrefu. Si suala la kusema unabadili kitu halafu unataka kutumia muda mfupi. Hakuna mkato katika mafanikio. Unatakiwa kujitoa haswaa.
Unatakiwa kuweka nguvu na akili nyingi katika eneo moja na kwa muda mrefu, mpaka likuletee matokeo unayoyataka. Kitaalamu inachukua masaa 10,000 ili kuweza kupata kile unachokitaka. Je, upo tayari kuwekeza katika masaa hayo?
5. Kila wakati kuwa na imani na hamasa ya kutosha.
Hata kama unachokifanya unakiona ni kidogo na hakikupi yale matokeo ya haraka kama unayoyataka, lakini kwako ni muhimu na lazima sana kuweza kujenga imani na hamasa ya kile unachokifanya.
Amini kile unachokifanya, kitakusadia na kitakufikisha kwenye malengo yako. Kwa imani hiyo utajikuta unaanza kujenga taratibu hamasa ambayo itakusukuma zaidi kuweza kufanikiwa.
6. Kuwa tayari kulipa gharama.
Angalia ni gharama gani ambazo unatakiwa uzilipe ili kupata hicho unachokihitaji. Inawezekana gharama ikawa ni kujitoa kwa muda wako au hata pesa lakini muhimu kwako gharama ni lazima zilipwe.
Hakuna mafanikio ambayo unaweza ukayapata pasipo kuhusisha gharama. Unapokuwa unatoa gharama hiyo ni njia mojawapo ya kukuhakikishia unafikia mafanikio yako bila shida yoyote.
7. Tengeneza nidhamu binafsi.
Mafanikio hayaji kwako, mpaka uwe umetengeneza nidhamu binafsi. Unapokuwa nidhamu binafsi katika eneo la kazi yako, kifedha au muda, itakufanya na kukusaidia kuweza kufikia mafanikio yoyote yale unayoyahitaji.
Tunakutakia siku njema na kila la kheri, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,