Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri katika kutimiza majukumu yako ya kila siku. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo katika maisha yako kwani ni zawadi ya kipekee ambayo huwa haipatikani mara mbili na wala huwezi kwenda kununua dukani.

 

Mpendwa msomaji, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kushirikishana yale niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa hiyo, nakusihi karibu tuweze kusafiri pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo. Katika makala yetu ya leo nitakwenda kukushirikisha mshauri wa kwanza katika maisha ya ndoa, mshauri wa kwanza katika maisha ya ndoa ni nani? Karibu tuweze kujifunza.

SOMA; Hizi Ndizo Hazina Saba (07) Muhimu Katika Maisha Ya Ndoa.

Rafiki, kama kuna vitu ambavyo utaondoka hapa duniani na bado hujavimaliza basi ni kujifunza, kadiri unavyozidi kujifunza kila siku ndipo unapogundua kuwa hujui kitu. Ndiyo maana tunaalikwa kujifunza kila siku kama vile tunavyokula kila siku, watu wanaoishi maisha ya ndoa huwa wanajisahau sana na kujiamini kuwa wakishafunga ndoa basi biashara imekwisha anaendelea kuishi maisha yake yale yale ya mazoea. Watu walioko katika maisha ya ndoa ni wachache sana wanaojitambua na kupenda kujifunza kuhusiana na maisha yao ya ndoa kwani unapofunga ndoa hakuna mtu anayepewa kitabu cha mwongozo wa kuishi maisha ya ndoa .

Siku zote adui mkubwa katika maisha ya ndoa ni wanandoa wenyewe, wengi wanapenda sana kumsingizia shetani kabla ya kujichunguza wao wenyewe. Kabla ya kumtafuta mchawi ni nani ni vema mkaa chini nyie wenyewe yaani wanandoa kuchunguza kiini cha matatizo na kuhojiana nyie wawili kwanza kabla ya kutafuta mshauri kutoka nje. Kwa hiyo, mshauri wa kwanza katika mahusiano ya ndoa ni wanandoa wenyewe na siyo mtu mwingine. Inawezekana wanandoa wanafanya maamuzi mengi kwa kuongozwa na hisia na siyo akili na ukishafanya maamuzi kwa kuongozwa na hisia lazima itakugharimu tu na utakuwa tayari kulipa gharama.

SOMA; Hizi Ndiyo Njaa Mbili Zinazowasumbua Wanandoa Katika Maisha Yao Ya Ndoa.

Huwa na shangazwa na wanandoa wanaokwenda kuanika matatizo yao nje kwa mfano, wanawake wengine wakienda saluni ni kama vile wamepewa tiketi ya kwenda kusimulia tamthilia au hadithi ya maisha yake ya ndoa na mwenza wake. Mwanamke makini anayeongozwa na akili hawezi kwenda saluni na kuwasimulia wenzake mambo yake ya ndani ya ndoa kwa marafiki zake tena saluni, unakuta hata mtu hajaulizwa ila kulingana na mifumo ya saluni mwingine akiona mwenzake mbona anafunguka mambo yake ya ndani na yeye anashawishika kusimulia yake.

Ndugu msomaji, pale wenza wanapokuwa wana changamoto, kitu cha kwanza mnachotakiwa kufanya ni kukaa chini na kutatua tatizo bila kulalamika na usikimbilie kuomba ushauri nje kwanza bila kumshirikisha mwenzako na mkayamaliza. Unakuta mwingine anakwenda kuomba ushauri juu ya mwenza wake ana tabia hizi na hizi na ukimuuliza je mlishawahi kukaa chini na mwenza wako kujadili juu ya hilo jambo? Anajibu hapana na wala sijamwambia, sasa kama hujamwambia unafikiri utapata suluhisho nje kama hamjakaa chini nyie wenyewe kwanza kwa sababu kiini cha tatizo kipo ndani mwenu na siyo nje.

Na kuna baadhi ya wanandoa midomo yao iko kama bata, wanashindwa kukaa na kitu kama vile bata anavyoachia tu haja zake popote pale bila hata kujizuia. Mambo yenu ya ndoa yanatakiwa kubaki katika kuta nne za chumba chenu na wala siyo nje. Ni fedheha kubwa pale unapokuwa unamwambia kila mtu mambo yako ya ndani, siyo kila mtu wa kumwambia na kumuomba ushauri. Hutakiwi kumwamini kila mtu katika maisha yako unatakiwa kujifunza kusema hapana kwa kila mtu.

SOMA; Hawa Ndio Maadui Wakubwa Wawili Wa Uchumba Au Ndoa Yako.

Hatua ya kuchukua leo, mwenza wako ndiye mshauri wako wa kwanza kaa naye na mweleze matatizo yenu na myatatue nyie wawili kwanza kabla ya kukimbilia nje. Usiwe kinara wa kusambaza umbea wa maneno nje kwani kuanika mambo ya ndoa nje ni kujimaliza nyie wenyewe.

Mpendwa msomaji, kama wanandoa mnatakiwa kuheshimiana nyie kwa nyie, mnatakiwa kupendana kwa upendo wa kutoka moyoni na siyo wa machoni, tunza siri za mwenza wako na msipeleke maneno nje kwa watu. Waswahili wanasema kikulacho kinguoni mwako, yule unayemwona mzuri wa kumwambia mambo yako ndiyo huyo huyo anatumia udhaifu wenu kuwaharibu. Kwani kuna watu wengine hawapendi kuona kabisa watu wakiishi kwa amani na furaha, akiona mambo yanaenda vibaya yeye ndiye furaha yake hivyo msiwape watu wa nje nafasi katika maisha yenu ya ndoa.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com