Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa haujambo na unaendelea vizuri kupambana na majukumu ya kila siku. Maisha ni kupambana kila siku rafiki kuhakikisha unakipata kile unachokitafuta, ubaya ni kukata tamaa tu.

 

Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani leo ni siku bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kufanya makubwa na kutegemea kupata kilicho bora. Rafiki, tunaalikwa kutumia vema muda wetu huu tuliopewa bure kwani kumbuka muda ukienda haurudi.

Mpendwa msomaji, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa hiyo, nakusihi sana tuweze kusafiri pamoja hadi pale tamati ya somo letu la leo.

Maisha yanakuwa magumu pale unapoanza kujifananisha na watu wengine, hatimaye unaweza ukajiona wenzako ndiyo wanaishi na wewe unachekesha. Lakini kwa mwana mafanikio yeyote anaamini kuishi katika maisha yake halisi bila kujifananisha na watu wengine. Maisha ambayo ni mazuri kuishi hapa duniani ni yale maisha ya kuishi maisha yako bila kujilinganisha na watu wengine.

SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuendelea Kuwa Na Hamasa Kubwa Kila Siku.

Rafiki, maisha ya kuhesabu vitu ambavyo hauna ni maisha ambayo yatakufanya uishi katika hali ya kutokua na furaha lakini ukiishi maisha ya kuwa na shukrani na vile ambavyo unavyo ni maisha yanayokupa hamasa ya kuzidi kufanikiwa na kuziona fursa. Usijidharau na kuidharau hali uliyokuwa nayo katika maisha yako bali itumie hali hiyo kama daraja kukuwezesha kwenda mbele zaidi ya hapo ulipo sasa.

Ndugu msomaji, natumaini ulishawahi kusikia msemo mmoja wa lugha ya kingereza unaosema it is too late maana yake umechelewa sana, lakini rafiki katika maisha jambo muhimu ambalo bado hujachelewa kulifanya katika maisha yako ni kuanza kufanya kile unachopenda kufanya. 

Hujachelewa bado kufanya kile unachokipenda, hujachelewa bado kutimiza ndoto yako hapa duniani, hujachelewa bado kutoa wimbo unaopenda kuutoa, hujachelewa bado kuchora picha unayopenda kuichora, hujachelewa bado kuandika kitabu kizuri kilicho ndani ya maisha yako.

Wengi unakuta wanakata tamaa mapema na kujiambia wimbo wa nimeshachelewa yaani it’s is too late hakuna kuchelewa hapa duniani, kama bado uko hai basi unaweza kufanya chochote ili kutimiza ndoto yako. Huenda kile unachofanya bado hakijaanza kukupa matokeo unayoyataka ila amini kuwa mambo yatakwenda vema ni swala la kujipa muda tu. Ukishaanza kujiambia katika akili yako umechelewa basi utashindwa kufanya vitu vingi sana, wapo ambao wanaahirisha kuoa au kuolewa kwa kusema wameshachelewa, wapo wanaotaka kusoma na kujiendeleza zaidi lakini wanajiimbia wimbo wa nimeshachelewa tayari.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Jasiri Na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Ya Unavyofikiria. ( 2)

Wewe kama mwana mafanikio hutakiwi kujiambia umechelewa katika eneo lolote lile bali wewe endeleza mapambano mpaka pale siku yako ya mwisho kuvuta pumzi duniani. Wengine wanajidharau na umri waliokuwa nao na kusema kwa sasa wameshachelewa hivyo hawawezi kufanya kitu chochote, mimi napenda kuamini katika uwezekano wa mambo ndiyo dalili ya mtu chanya katika safari ya mafanikio. Kigezo cha umri kwenda siyo sababu ya wewe kushindwa kufanya kile unachokipenda bado una nafasi ya kubadilisha maisha yako vile unavyotaka kuwa.

Ndugu msomaji, tuna mifano ya watu kama Nelson Mandela ambao walikuwa wamekaa gerezani kwa muda wa miaka ishirini na saba (27) lakini hakusema ameshachelewa kutimiza ndoto yake lakini alipambana aliamua kuanza na muda huo huo aliokuwa nao kutimiza ndoto yake ya kuwa raisi na hatimaye alifanikiwa. Kwa hiyo, kama Nelson Mandela angeamua kujiimbia wimbo wa ameshachelewa sana leo hii asingejulikana kama rais na kuacha alama kubwa hapa duniani.

Kwa hiyo, rafiki hata wewe kama una ndoto yako usijiimbie wimbo wa umeshachelewa sana bado muda unao na muda bora kwako wa kuanza kutimiza ndoto yako ni sasa na wala siyo baadaye wala kesho. Kuwa na ndoto kubwa, anza kidogo na anza sasa yaani dream big, start small and begin now. Usikubali kufa na ndoto yako kwa kujiimbia wimbo wa umeshachelewa kuanza hapana bado hujachelewa kuanza una nafasi ya kushinda kama bado uko hai.

Hatua ya kuchukua leo, kuanzia leo kataa kabisa kujiimbia wimbo wa umeshachelewa na badala yake anza kuchukua hatua hapo hapo ulipo bila kujali kile ulichokuwa nacho. Hujachelewa kufanya kama bado uko hai na una nafasi ya kushinda kama bado unaendelea kuvuta pumzi.

Kwa hiyo, maisha ni mapambano mpaka siku yako ya mwisho hapa duniani, kama uko duniani bado hujachelewa kutimiza ndoto yako. Watu ambao hawawezi kutimiza ndoto zao ni wale waliolala makaburini lakini wewe ambao uko hai na unaendelea kuvuta pumzi ya Mungu bure bado una nafasi. Usikubali kukata tamaa hata siku moja, endelea kupambana mpaka upate ushindi unaotaka.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com