Tarehe moja ya mwezi wa tano kila mwaka, ni siku ya kimataifa ya wafanyakazi. Siku hii ina historia kubwa sana kwa wafanyakazi wote, kwa sababu imekuwa ni siku ya kuazimisha harakati mbalimbali zinazofanywa na wafanyakazi ili kuhakikisha mazingira yao ya kazi na maslahi yao yanakuwa mazuri zaidi.

 

Kazi, kwa mfumo wa kuajiriwa hakikuwa kitu cha asili kwetu binadamu, kwani kwa miaka mingi sana iliyopita, hakukuwa na kazi rasmi za ajira. Bali kila mtu alijituma kwa namna yake, mkulima akalima, mfugaji akafuga, na mchongaji akachonga. Baada ya kila mtu kuzalisha chake, basi kulikuwa na njia mbalimbali za kubadilishana thamani, mwenye mazao akabadilishana na wanyama na kadhalika. Baadaye ikaja fedha na kubadilishana thamani kukawa bora zaidi.

Mabadiliko makubwa sana yalikuja baada ya mapinduzi ya viwanda, yaliyotokea kati ya karne ya 18 na karne ya 19. Hapa ndipo uzalishaji uliongezeka zaidi na hivyo kuhitaji watu wa kufanya kazi zaidi, na kwa muda mrefu. Na katika hili ndipo zilipozaliwa ajira rasmi, ambapo mtu aliajiriwa kwa ajili ya kufanya shughuli fulani, na baadaye kulipwa mshahara.

SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.

Mazingira ya zamani ya kazi yalikuwa magumu sana, muda wa kufanya kazi ulikuwa hauna kiwango, ni kadiri mwajiri anavyoamua. Watu walikuwa wakifanyishwa kazi mpaka masaa 

16 kwa siku, malipo yalikuwa madogo na hata afya za wafanyakazi zilikuwa hatarini. Yaani mapinduzi ya viwanda na uhitaji mkubwa wa wafanyakazi, ulipelekea watu nao kuchukuliwa kama bidhaa tu au rasilimali ya uzalishaji.

Harakati mbalimbali za makundi ya wafanyakazi, zimeboresha sana mazingira ya kazi. Kwa mfano sheria ya kufanya kazi masaa nane kwa siku, siku tano kwa wiki, imetokana na harakati za makundi na vyama vya wafanyakazi. Hivyo unapokwenda kusherekea siku ya wafanyakazi leo, kumbuka kuna waliopitia magumu sana mpaka tunafika hapa tulipo sasa.

Leo katika barua yangu hii kwa marafiki zangu wote ambao ni wafanyakazi, nachukua nafasi ya kuwapongeza sana kwa kazi wanazofanya. Wafanyakazi ni watu muhimu kwenye taifa lolote, watu ambao wanatoa huduma za msingi sana, watu ambao wanazalisha bidhaa muhimu kwa maisha, ni watu muhimu. Lakini mara nyingi watu husahau umuhimu wao kutokana na mazingira yalivyo. Labda kwa waajiri kutojali, au kwa kipato kuwa kidogo na hivyo kuona kama hawana maana. Pia kuibuka kwa harakati za biashara na ujasiriamali, kunafanya baadhi ya watu kuona walioajiriwa kama hawajielewi hivi, hawajui wanachofanya kwenye maisha yao.

Leo katika barua hii, nataka nikukumbushe umuhimu wako kwako binafsi na taifa kwa ujumla, na baada ya hapo, nikupe njia mbadala ya kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi ukiwa kwenye ajira yako.

SOMA; Kama Unatafuta Kazi, Acha Kufanya Makosa Haya Ili Kuipata Kazi Hiyo.

Wewe kama mfanyakazi na mwajiriwa ni mtu muhimu sana.

Napenda nianze kwa kukukumbusha hilo, kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda, na maisha yanavyozidi kuwa magumu, watu wanasahau kabisa hilo. Zimekuwepo kauli na harakati za kuwafanya wale wote walioajiriwa kujiona kama ni kosa kubwa kwao kufanya hivyo. Na wapo ambao wamejaribu kuondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri, na huko maisha yao yakawa magumu kuliko hata walivyokuwa kwenye ajira.

Wewe mfanyakazi ni muhimu sana, kwa sababu hata kila mtu akijiajiri, au kufanya biashara, bado atahitaji mtu wa kumsaidia kazi zake, hataweza kufanya kila kitu. Hivyo bila ya watu wa kufanya kazi, ndoto za wengi haziwezi kufikiwa.

Zipo huduma nyingi tunazopata ambazo zinaboresha maisha yetu, huduma kama afya na elimu, wapo watu ambao wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha unakuwa na afya bora. Kwamba ukipata ajali hata kama ni saa sita usiku, unaweza kuwahishwa hospitali na maisha yako yakaokolewa. Yupo mtu ambaye saa sita hiyo usiku amechagua kuwa kazini na siyo nyumbani na familia yake, ni mtu muhimu sana.

Tunapeleka watoto wetu mashuleni wakasome, iwe ni shule ya umma au ya binafsi, wale wanaofundisha watoto wetu siyo wanaomiliki shule, bali walimu ambao wameajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Kila tunachotumia kwenye maisha yetu, kuanzia vyakula, mavazi na hata vingine vya matumizi ya kila siku, kuna watu ambao wameajiriwa kuzalisha vitu hivi. Hivyo wafanyakazi ni muhimu na wataendelea kuwa muhimu kwenye maisha ya kila mmoja wetu.

Unawezaje kuyafanya maisha yako kuwa bora ukiwa mwajiriwa?

Pamoja na umuhimu mkubwa wa wafanyakazi kwenye maisha yetu ya kila siku, lazima tukubaliane na ukweli kwamba, maisha ya waajiriwa wengi siyo bora kwa viwango walivyokuwa wamejiwekea wao wenyewe. Wengi wapo kwenye madeni na vipato vyao havitoshelezi kulingana na mahitaji yao. Na kwa kuwa wao siyo waamuzi wa mwishi wa kipato gani wapate, hawawezi kuongeza kipato kadiri wanavyotaka wao wenyewe.

Pamoja na hayo, bado siyo sababu ya wewe mfanyakazi kukosa maisha bora, kuwa na maisha ya chini wakati kila anayekuzunguka anapiga hatua. Hivyo mimi rafiki yako, nakwenda kukushirikisha hatua tatu muhimu za kuchukua ili kuboresha zaidi kazi unayofanya, kuongeza kipato kwenye kazi yako na nje ya kazi yako, na hata kuweza kufikia utajiri ukiwa kwenye ajira.

1. Kuboresha zaidi kazi yako.

Moja ya sababu zinazofanya waajiriwa wengi kukwama, yaani kuwa pale pale miaka nenda rudi, ni kufanya kazi kwa mazoea, wengi wamekuwa wanafanya kazi vile vile, hawaweki juhudi yoyote kubwa kuboresha zaidi kazi zao, na kisingizio kimekuwa kwamba hata hivyo hawanilipi vizuri.

Sikia rafiki yangu, watu hawaanzi kukulipa vizuri ndiyo wewe ufanye kazi, bali wewe unapaswa kuanza kufanya kazi bora ili kuwashawishi watu wakulipe vizuri zaidi. Ninachojua mimi ni kwamba watu wana changamoto, hiyo inaanza na mwajiri wako, hivyo wewe kama mwajiriwa, unapojua changamoto za mwajiri wako, na kumsaidia kuzipunguza, ataona umuhimu wako na hatokubali kukupoteza, hivyo atakulipa vizuri zaidi.

Lakini kama wewe unafanya kazi ya kawaida tu, ila unachoweza ni kuongea na kulalamika sana, utaendelea kulipwa kidogo unacholipwa na ikitokea nafasi ya watu kupunguzwa, utakuwa wa kwanza kutumia nafasi hiyo.

Weka juhudi sana kwenye kazi yako, nenda hatua ya ziada na jifunze zaidi ili kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya. Japokuwa umeajiriwa, fanya ile kazi kama yako, chukulia ni kazi yako binafsi unaifanya, kazi ambayo inabeba jina lako na dunia nzima inakuona unavyofanya, na hivyo utaifanya kwa ubora sana.

SOMA; Hii Ndio Kazi Inayolipa Sana Ambayo Hata Wewe Unaweza Kuifanya.

2. Kuongeza kipato kwenye ajira na nje ya ajira.
Kwa kuwa moja ya changamoto za kuwa kwenye ajira ni kutokuweza kudhibiti ongezeko lako la kipato, basi unahitaji kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha hilo linatokea, ukiwa ndani ya ajira yako.

Njia ya kwanza ni kuongeza kipato ndani ya ajira uliyopo, na hapa unafanya kama nilivyokushirikisha hapo juu. Ongeza juhudi zaidi, nenda hatua ya ziada na tatua changamoto zaidi. Hii itamfanya mwajiri aone thamani yako zaidi na kuwa tayari kukuongezea kipato ili uendelee kuwa naye zaidi. Pia unaweza kuangalia ni kipi ambacho mwajiri wako anakosa, ukaona unawezaje kumpatia, ukaongea naye na ukampa kile anachokosa kwa makubaliano ya kuongeza kipato. Wewe unaijua kazi yako vizuri, angalia kila namna ambayo unaweza kuweka juhudi zaidi na kipato chako kikaongezeka zaidi.

Njia ya pili ni kuongeza kipato nje ya ajira yako. Na hapa unaweza kutafuta ajira ambayo unaweza kuifanya kwa muda wako wa ziada, wengi wanapenda kuita part time job, au kuanza biashara ukiwa bado upo kwenye ajira. Katika njia hizo mbili, nakushauri sana uchukue njia ya kuanza biashara ukiwa bado upo kwenye ajira, hii itakufungulia uhuru zaidi wa baadaye, hasa kwenye kipato, ukilinganisha na kazi ya ziada.

Nimeandika na kueleza vizuri sana unavyoweza KUANZA NA KUKUZA BIASHARA YAKO ukiwa bado umeajiriwa kwenye kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA. Nimeeleza kuanzia wazo la biashara, mtaji, muda, usimamizi, ushirika na hata uwekezaji kwenye kitabu hichi. Ninachokushauri ni upate na kusoma kitabu hichi cha BIASHARA NDANI YA AJIRA. 

Kitabu kinauzwa tsh elfu 10, na unaweza kutumiwa popote pale ulipo Tanzania. Kukipata, tuwasiliane kwa simu 0717396253.

3. Kuwa tajiri.

Moja ya vitu vigumu sana kutokea kwenye ajira, ni kuwa tajiri. Najua neno utajiri lina ukakasi mwingi, kuna ambao wanajifanya hawataki utajiri lakini usiku hawalali wakifikiria watawezaje kuendesha maisha yao, ikiwa ni tarehe 15, mshahara umeisha na kuna zaidi ya siku kumi mbele kufikia mshahara unaofuata. Hivyo tuweke unafiki pembeni na tuseme kwamba unautaka utajiri. na tukubaliane kwamba hutaweza kuupata utajiri kwa kutegemea kipato kimoja pekee, ambacho ni mshahara.

Hivyo basi, ili kufikia utajiri, zipo njia kuu mbili za kupita, na unaweza kuzipita hata ukiwa bado upo kwenye ajira yao.

Njia ya kwanza ni hiyo ya kuanza biashara ukiwa kwenye ajira yako. Kama nilivyoeleza hapo juu, pata kitabu pia kitakusaidia sana.

Njia ya pili ni kuwekeza. Unahitaji kuwa na uwekezaji ambao baadaye utakuzalishia wewe faida, hata kama hufanyi kazi moja kwa moja. Mimi nimekuwa nasema hivi, UTAJIRI NI PALE FEDHA INAPOKUFANYIA WEWE KAZI, NA UMASIKINI NI PALE 

UNAPOIFANYIA KAZI FEDHA. Hivyo, hata kama mshahara wako ni milioni 10 kwa mwezi, kama ndiyo chanzo chako pekee cha kipato, wewe bado ni masikini, kwa sababu ukiacha kufanya kazi sasa, huna kipato cha uhakika. Unahitaji kuwekeza ili uweze kujijengea kipato cha uhakika hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.

Yapo maeneo mengi ya kuwekeza, kuanzia kwenye hisa, vipande, hatifungani, kilimo, mashamba, majengo na hata kwenye biashara mbalimbali. Anza sasa kuwekeza hata kwa hatua ndogo ili uweze kuondoka kwenye utegemezi wa mshahara pekee.

Ninaamini kuna kitu ambacho wewe rafiki yangu umeondoka nacho kwenye barua hii ya wazi kwako, ninachokuomba usifurahie tu kusoma na kuendelea na BUSINESS AS USUAL, badala yake anza kuchukua hatua sasa. Kila inapofika tarehe moja ambayo ni maadhimisho ya siku ya wafanyakazi, na wewe fanya tathmini zako kujua upo wapi na unaelekea wapi kwenye ulimwengu wa kazi na hata ubora wa maisha yako kwa ujumla.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.