Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, hatutauacha msingi huu kamwe kwenye maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kubusu APPS NA NIDHAMU BINAFSI…
Kadiri maendeleo yanavyokua, ndiyo maisha yetu yanazidi kuwa bora, lakini siyo rahisi.
Maana watu wengi wamekuwa wakifikiri ujio wa teknolojia mpya unarahisisha maisha, hapana, bali unaboresha maisha.
Hizi simu janja ambazo ndiyo zimeleta mabadiliko maku wa kwenye mawasiliano, zina uwezo wa kuwa na programu(APPS) mbalimbali tunazoweza kutumia kwenye maisha yetu.
Sasa hivi kuna program karibu ya kila aina, chochote unachotaka, ukiingia playstore au app store hukosi.
Kuanzia kwenye afya, ufanisi, kazi, biashara, burudani na kadhalika.
Sasa uwepo wa programu hizi, umewafanya wengi kuamini maisha yanakuwa rahisi, na hivyo kuzitegemea sana.
Kwa mfano, mtu anayetaka kufanya mazoezi, atatafuta ni app gani nzuri ya mazoezi.
Anayetaka kuandika atatafuta ni app gani nzuri ya kuandika.
Lakini pamoja na uwepo wa app zote hizo, bado kufanya mazoezi, kuandika, na mengine, yanahitaji uache kile unafanya na ufanye hicho unataka kufanya.
Hata ungekuwa na app bora kiasi gani, lazima utoke hapo ulipo na uende kufanya mazoezi hasa.
Hata ungepata app nzuri kiasi gani, lazima uache vingine unafanya, ukae chini na kuandika.
Iwe ni kupunguza uzito, kusimamia muda wako vizuri, kuongeza ufanisi wako, cha kwanza unachohitaji ni NIDHAMU BINAFSI kwanza, ya kuweza kuacha mengine, na kufanya kile umepanga.
Hakuna app inayoweza kukuletea nidhamu binafsi. App itakusaidia kama tayari una nidhamu binafsi.
Hivyo rafiki, kabla hujakazana kutafuta kila aina ya app, jiulize kwanza una nidhamu binafsi? Upo tayari kuacha kila kitu na kufanya kile ulichopanga kufanya?
Hapo ndiyo pazuri kuanzia, na anzia hapo.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info