Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo letu tutakwenda kujifunza makosa mawili makubwa yanayogharimu maisha ya watu wengi.

Katika maisha ya binadamu kuna mambo mawili wanayofanya watu na kuwagharimu sana katika maisha yao. Unaweza kuweka juhudi kubwa sana katika kile unachofanya lakini kama utakuwa umetawaliwa na mambo haya mawili unakuwa kama unahamisha maji baharini. Ni wazi kabisa kila mmoja wetu ameshawahi kufanya makosa katika maisha yake kwa sababu makosa ndiye mwalimu mkubwa katika maisha yetu. Huwa tunajaribu vitu mbalimbali katika maisha yetu muda mwingine tunaanguka badala ya kushinda lakini katika kujifunza hakuna kushindwa bali kushinda. Kila kosa unalofanya ni kama dhahabu kwako kufanya vizuri baadaye.

Mpendwa msomaji, tuna vitu viwili ambavyo huwa vinagharimu sana maisha ya watu. 

Vitu hivyo ni uzembe na ujinga. Ukijaribu kuangalia katika maisha ya kila mtu ambaye hayuko makini lazima atakuwa ameshaathiriwa na vitu hivi viwili. Matatizo mengi yanayotokea katika maisha yetu chanzo chake kikubwa ni uzembe na ujinga. Watu wametwaliwa na uzembe kuanzia maisha ya kimwili, kiroho na kiakili. Ujinga ndiyo ugonjwa uliotapakaa miongoni mwa watu wengi.

Watu wanaendesha maisha yao kwa mazoea uzembe na ujinga unakua umetamalaki. Na tunapaswa kujua kuwa kuna tofauti kati ya makosa na uzembe. Uzembe ni kukosa umakini juu ya jambo au mambo fulani. Inawezekana mtu anapika jikoni huku anafua nguo nje anawasha jiko na kubandika chakula jikoni anatoka nje na kusahau kuwa alibandika chakula jikoni hivyo matokeo yake chakula kinaungua. Kwa hiyo uzembe una wagharimu kiasi kikubwa watu wengi.

Ukiwa unaweka uzembe katika jambo lolote lazima utapata hasara tu, uzembe hautakiwi kila eneo la maisha yetu iwe ni kazini, kwenye biashara, mahusiano, shule na kila kitu uzembe hauitajiki hata kidogo katika maisha yetu. Mzazi akileta uzembe katika malezi ya mtoto hawezi kuja kukwepa hasara yake hapo baadaye. Ukileta uzembe katika afya yako lazima utapata adhabu ya magonjwa hivyo utashindwa kufurahia maisha yako.

Ujinga ndiyo kabisa, watu hawapendi kujifunza vitu mbalimbali wamezoea kuishi kimazoea tu. Watu wanatapeliwa kwa sababu ya ujinga. Elimu bado inahitajika sana katika maisha ya kila binadamu. Kuna kazi kubwa sana ya kuondoa ujinga katika jamii yetu ndiyo maana tunaalikwa watu waweze kujifunza kwa kusoma makala chanya, vitabu na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Rafiki, tunakosea sehemu nyingi katika maisha yetu kwa sababu ya ujinga. Laiti kama kila mtu angekuwa ana elimu ya mambo mbalimbali ingekuwa ngumu kuanguka. Ujinga ni kama ukungu ambao unatuzuia tusione mbele kuna nini hivyo kama unataka kufanya kitu ni vizuri ukajifunza kwa watu ambao tayari wana mwanga juu ya vitu hivyo.

Tunaalikwa kuwa makini katika maisha yetu juu ya kitu chochote kile ili kuepuka adhabu za ujinga na uzembe kwa sababu ukifanya uzembe lazima uwe tayari kupokea adhabu. 

Uzembe ni kama tundu dogo katika meli ambalo linaweza kusababisha maji kuingia ndani ya meli kidogo kidogo na hatimaye meli kuzama. Vivyo hivyo katika ndoo, mtu anayechota maji na ndoo iliyotoboka kwa chini ataweza kusubiria ndoo ijae lakini haiwezi kujaa kwa sababu ya lile tobo katika ndoo.

Hatua ya kuchukua leo, dawa ya uzembe ni kuwa makini na dawa ya ujinga ni maarifa. 

Hivyo zingatia hayo ili kuepuka madhara ya vitu hivi katika maisha yako.

Kwa kuhitimisha, tunapaswa kuwa makini sana katika maisha yetu kwani uzembe unagharimu maisha ya watu wengi sana lakini pia ujinga ni changamoto kubwa sana katika jamii yetu. Hivyo popote pale ulipo jitahidi kujifunza na kuwa balozi mzuri wa mabadiliko katika jamii yako.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com