Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza sababu kuu moja kwanini watu wanaajiriwa au wanajiajiri katika maisha yao hivyo basi,  karibu tujifunze.

Rafiki, kama ni kitu muhimu ambacho tunapaswa kujenga katika maisha yetu hapa duniani basi ni jina. Jina ndiyo utambulisho wetu, majina yetu ndiyo yanaongea hata kama sisi hatupo mahali fulani. Leo hii watu wakitaja jina lako mahali wanapata taswira gani katika akili zao? Wale watu ambao wamejingea majina ndiyo wana nafasi kubwa sana duniani.

Kama kuna kazi nguvu duniani basi moja wapo ni kazi ya kujenga jina. Kujenga jina ni mchakato mrefu unaohitaji mtu kudumu katika maono yake kwa muda mrefu. Na majina yetu hayawezi kujengwa kwa siku moja. Kumbe tunapokuwa tunafanya chochote kile katika hii dunia ni tunajenga jina. Kazi yoyote inayopita katika mikono yako ujue ndiyo unaacha alama yako duniani. Na tunajenga majina yetu kwa kazi tunazofanya kila siku katika maisha yetu.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE SCHOOL OF GREATNESS (Mwongozo Wa Kuwa Na Maisha Makubwa, Mapezi Ya Dhati Na Kuacha Jina.)

Ndugu msomaji, kama unasoma hapa natumaini utakuwa umejiajiri au umeajiriwa je na huenda uko moja ya sehemu hizo nilizotaja na hujui kwanini umejiajri au umeajiriwa. Watu wanaajiriwa au wanajiajiri hawajui lengo lao kuu ni nini, watu wengi wanapojiajiri au kuajiriwa basi kipaumbele chao cha kwanza ni kuangalia anapata nini yaani anaangalia anapata malipo kiasi gani. Hata mtu akiambiwa kuna kazi sehemu kitu cha kwanza atakacho kuuliza siyo kingine bali ni malipo.

Kwahiyo, watu wamejiandaa kupata malipo na siyo kutoa thamani pale wanapoitwa kufanya kazi. Sasa sababu kuu moja inayosababisha watu wengi kuajiriwa au kujiajiri ni moja tu ambayo ni kupunguza matatizo. Unaajiriwa sehemu ili uende ukapunguze matatizo ya sehemu husika na unajiajiri ili uende ukapunguze matatizo sehemu husika na siyo vinginevyo.

Rafiki, hakuna mtu ambaye anakuajiri kwa lengo la kwenda kuongeza matatizo bali kupunguza matatizo ya sehemu husika. Watu wanashida hivyo wanahitaji kutatuliwa matatizo yao, unajiajiri kwa lengo la kwenda kutatua matatizo ya watu na matatizo ndiyo yanazaa fursa nyingi katika jamii yetu. Mwanzoni huduma za kibenki zilikuwa ni shida lakini sasa hivi watu wengi wameamua kutatua tatizo hilo na kusogeza huduma hizo karibu kabisa na maeneo tunayoishi kupitia mitandao ya simu zetu za mikononi.

Tunapaswa kuelewa kuwa mtu anakuhitaji umfanyie kazi anahitaji umsaidie kupunguza matatizo na siyo kumuongezea matatizo. Hakuna mtu anayeajiri au kuajiriwa kwa lengo la kuongeza matatizo, unaajiriwa ili ukapunguze matatizo sehemu husika. Wengi hawalijui hilo wanajua wanapoajiriwa au kujiajiri lengo ni kutafuta tu pesa hapana, uko hapo ulipo kwa ajili ya kutatua matatizo ya watu. Leo hii unanisoma hapa kwa sababu nimechagua kutatua matatizo ya ujinga. Ujinga ni ugonjwa mkubwa katika jamii yetu na watu wanakosa mambo mazuri katika maisha yao kwa sababu ya kukosa maarifa.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Waalimu Wa Sanaa Na Kada Nyingine Zilizokosa Kipaumbele Kwenye Ajira Za Serikali. ( Kama Umesoma Na Huna Ajira, Pia Soma Hapa.)

Hatua ya kuchukua leo, hakuna mtu anayeajiriwa kwa lengo la kuongeza matatizo bali unaajiriwa au kujiajiri kwa lengo la kupunguza matatizo. Kama umeajiriwa au umejiajiri jua kabisa uko hapo kwa lengo la kutatua matatizo na kupunguza matatizo na siyo kupata hela tu. Kama unapunguza matatizo una stahili kupata malipo lakini kama unaongeza matatizo hustahili malipo.

Unapokuwa unatatua matatizo ya watu na kufanya kazi bora ndiyo chanzo cha wewe kujenga jina lako. Kazi yako ndiyo itakutangaza na jina lako litakuwa bora kulingana na kazi unafanya katika kutatua matatizo ya watu. Unapofanya kitu hovyo hovyo ujue unaharibu jina lako na unapozalisha kazi bora ujue unajenga jina lako. Hatima ya kujenga jina lako liko katika kutatua matatizo ya watu hivyo ukipewa kazi ya mtu ifanye kazi kwa ubora kwanza ndiyo uangalie malipo.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.