Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza kanuni bora ya malezi ya watoto yenye mafanikio makubwa hivyo basi,  karibu tujifunze.

Malezi ya watoto ni kazi kama kazi nyingine tunazozijua na kuzifanya katika maisha yetu. muda mwingine kulingana majukumu huwa tunatafuta hata wasaidizi wetu ili waweze kutusaidia kulea watoto pale tunapokuwa tumebanwa na mambo mbalimbali.  Kumlea mtoto katika mazingira chanya kwenye dunia yenye mtazamo hasi inahitaji kazi kubwa.

malezi bora

Rafiki, kanuni bora ya malezi kwa watoto  yenye mafanikio makubwa ni matendo. Matendo katika malezi ya watoto ndiyo mwalimu mzuri atakayemwongoza mtoto wako katika mafanikio unayoyataka kuyaona katika maisha yake. Watoto wanapenda kujifunza kwa vitendo kutoka kwa wale wanaowalea aidha ni wazazi au walezi wao.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Raising Positive Kids In A Negative World (Jinsi Ya Kulea Watoto Wenye Mtazamo Chanya Kwenye Dunia Hasi).

Huwa tunajidanganya sisi wenyewe pale tunapowaambiwa watoto wafanye vitu ambavyo hata sisi wenyewe hatuvifanyi vitu hivyo. Tunapowaambiwa watoto wetu wawe wasafi basi mzazi ndiyo unapaswa kuonesha mfano wa kuwa msafi. Tunapowaambiwa watoto wetu wasali na waende nyumba za ibada basi mifano mzuri wanatakakuiona kutoka kwetu. Kama tunawaambia watoto kitu ambacho sisi wenyewe hatufanyi tunakuwa tunajidanganya na kamwe hatuwezi kupata malengo tuliyokusudia kuayapata juu ya watoto wetu.

Wazazi wanapokuwa wanafanya kwa vitendo yale wanayowaambiwa watoto wao basi hiyo ndiyo kanuni bora ya malezi. Unapowafundisha watoto wako utamaduni wa kujiwekea akiba wakati wewe mwenyewe unakushinda huo utamaduni hapo unakuwa unakosea. Kama unawahamasisha watoto wafanye mazoezi basi n a wewe inabidi uwe mstari wa mbele katika kufanya mazoezi kisiishie mdomoni tu.

Kama upendo uko kwa wazazi basi watoto nao watafurahia upendo na kuuishi upendo huo katika maisha yao. Huwezi kuwahubiria watoto juu ya falsafa ya upendo lakini maisha yenu nyie kama wazazi mnaishi katika magomvi, malumbano na mambo mengine yanayofanana na hayo. Kile tunachosema na kuwaambiwa watoto sharti la kwanza na sisi tuwe tunalifanya jambo hilo.

Mpendwa msomaji, mzazi ambaye hana falsafa katika maisha yake hana malezi mazuri kwa watoto. Binadamu ambaye hana falsafa hana maisha kabisa kwa sababu kama huna misingi au falsafa unayosimamia katika dunia hii ya leo basi utakuwa ni chambo kwa watu wengi kila mtu atakuwinda ili akuvune. Kumbuka kuwa watu wanaohangaika na kuyumbishwa ni wale ambao hawana falsafa au misingi wanayosimamia hivyo basi, tunaweza kusema kuwa watu ambao hawana misingi au mwelekeo basi, mwelekeo wowote utawachukua.

SOMA; Ifahamu Sehemu Iliyogeuka Kuwa Kimbilio La Wazazi Wengi Katika Malezi Ya Watoto.

Kama huna misingi au falsafa yoyote unayoitoa kwa watoto wako basi utakuwa umewaweka watoto wako rehani na dunia itawashambulia ili iwamalize. Kama mzazi hutakiwi kukosa kumjengea mtoto misingi bora katika maisha yake ambayo ataisimamia hata atakapokuwa mzee lakini akikosa misingi atakuwa ni chambo kwa dunia kila mtu atamwinda.

Hatua ya kuchukua leo, jifunze leo kumfundisha mtoto kitu chochote kwa vitendo na kile unachomhubiria hakikisha na wewe unakiishi kitu hicho. Kama huna uadilifu kwenye maisha yako utawezaje kumfundisha mtoto uadilifu? Mjengee mtoto misingi bora ya kifalsafa tokea akiwa mdogo ili iweze kumsaidia kwenye maisha yake.

Kwahiyo, kama mzazi amekosa kumjengea mtoto misingi ya kufanya vitu kwa matendo basi ni wazi kabisa mtoto atakuwa na hali mbaya katika dunia ya leo kwani dunia ya leo inatafuta watu ambao hawana misingi katika maisha yao ili iwatumie kwa manufaa yao na wala si kwa manufaa yako.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.