Kati ya kitu ambacho huwezi kucheza nacho na ikitokea umekipoteza ndio imetoka hiyo, ni muda ulionao. Unaweza ukacheza na vyote kwenye maisha yako na ukavipoteza na ukaanza upya hadi kufanikiwa, lakini si muda wako, ukipoteza muda haurudi tena.

Upo uwezekano pesa ukaiweka ya akiba kama umeipata pesa nyingi na ya ziada. Hata hivyo inapotokea pesa imepotea, upo uwezekano pia wa kuweza kutafuta pesa zingine kwa baadae na ukawa tena na pesa kama kawaida utafikiri hukupoteza kitu.

Lakini uwezekano huo ambao upo kwenye pesa hauwezi kutokea hata kidogo kwenye muda wako. Muda ulionao ni kitu kingine ambapo thamani yake haipimiki kwa chochote. Unapochagua kupoteza muda wako ndio unapoteza maisha yako kabisa.

mkutano wa maandalizi

Unayo nafasi moja tu ya kufanya maisha yako ya kesho yawe bora ikiwa utaitumia leo kwa uhakika. Unayo nafasi moja ya kutumia fursa uliyonayo kwa uhakika hadi kufanikiwa kwa muda ulinao. Ikiwa utajichanganya na kutumia fursa hovyo huwezi kufanikiwa.

Muda ulionao leo unaweza kufanya maisha yako ya kesho yakawa mazuri sana au yakawa hovyo kabisa, kikubwa tu inategemea muda wako unautumiaje? Kama unautumia muda wako hovyo andika maumivu.

SOMA;Kama Haupo Tayari Kuwekeza Kwenye Mambo Haya Matatu, Sahau Kuhusu Mafanikio.

Ndio maana unatakiwa utambue leo yako ikipita, hiyo ndio imepita haiwezi kurudi tena. Kwa hiyo kama kuna jambo umeliahirisha na kuamua kulifanya kesho, basi ujue kabisa umesogeza mafanikio yako kesho.

Unachotakiwa kujua kitu kingine kinachowaangusha watu wengi kwenye maisha si kwa sababu hawana uwezo huo, bali kinachowaangusha ni kwamba wamekuwa ni watu wa kutumia muda wao hovyo sana kila siku.

Kama unajiona huna cha kufanya kwenye maisha yako, hebu tumia muda wako kidogo ulionao kuweza hata kujifunza juu ya maisha kupitia vitabu au semina ili uweze kubadilisha maisha yako. Usikubali kupoteza muda wako hovyo hiyo ni hatari kubwa sana kwako.

Juhudi zako lazima ziendane na kutambua umuhimu wa kutunza muda wako ili kufikia mafanikio makubwa. Ikiwa utakuwa unaishi tu kiholela na kuona muda kwako ni kitu ambacho hakina thamani kabisa utapotea.

Kumbuka kila wakati muda unaotengeneza maisha yako ni muda huo huo mdogo  ambao unaouna hauna thamani huo ndio unaofana maisha yako yawe bora au hovyo kabisa. Unatakiwa kuwa makini na muda wako ili kujenga maisha uyatakayo.

Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kujifunza maisha na mafanikio.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; http://www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com