Uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo ni aina ya uwekezaji ambao umebadili maisha ya watu wengi zaidi duniani tofauti na uwekezaji mwingine. Ni uwekezaji ambao unaweza kufanyika mahali popote na wakati wowote kutegemea na aina ya huduma unayoitoa, mafanikio ya watu mbalimbali waliowekeza kwenye rasilimali ardhi na majengo umetoa hamasa na kufungua milango kwa watu wengi zaidi kutumia fursa hii katika kuboresha maisha yao binafsi na jamii inayowazunguka. Nafurahi sana pale ninapowapokea marafiki wapya wakiwa na shauku kubwa ya kufanya uwekezaji kwenye rasilimali ardhi na majengo katika kutimiza malengo ambayo siku za nyuma waliamini kwamba hawawezi na ni jukumu la watu wa tabaka fulani. Kila siku zinavyozidi kusonga mbele idadi ya watu wapya inazidi kuongezeka wakiwa na dhamira ya dhati ya kuwa miongoni mwa watu wanaohitaji kuwa huru kifedha.

Tunapoelekea kwenye uchumi wa kati ni muhimu sana kwa sasa ukaanza kujipanga katika kufanya mabadiliko ya kifikra na kiutendaji katika kufikia malengo yako kwa ubora na ufanisi mkubwa. Mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kutokea yanatulazimisha kutumia mbinu mbadala tofauti na tulizozizoea ili kuendana na hali ya ushindani ambayo inaongezeka kila siku.

majengo 37

Hizi ni salamu kwa wale waliokwisha wekeza na kuamini kuwa wameshafika na hakuna hatua zozote zinazofanyika katika kujifunza, kuboresha na kuimarisha uwekezaji wao. Ukweli ni kwamba mnapaswa kushituka na kuendelea kujifunza na kuboresha huduma na uwekezaji wenu ili kuendana na hali ya mazingira ya sasa. Ni muhimu sana ukajiwekea dhamira ya kufanya zaidi ya ulivyofanya jana kuendana na mazingira na hali ya uhitaji kwa kutoa huduma bora na kufanya uwekezaji kwa kutumia mbinu za kisasa.

Hali ya sasa kila mtu anajitahidi kufanya mambo katika hali ya weledi, ubora na ufanisi mkubwa tofauti na walivyofanya wengine, hivyo ni muhimu sana kuchukua hatua ambazo wengine hawakuchukua, weka dhamira ya kufanya kitu ambacho wengine  hawajawahi kufanya. Pamoja na hayo, leo napenda kukukumbusha tena kuhusu umuhimu wa kuulinda uwekezaji wako kwenye ushindani wa soko na kuepuka baadhi ya changamoto ambazo zinazoweza kutokea wakati usioutarajia au kujiandaa.

Kodi Ya Ardhi Na Majengo

Moja ya jambo muhimu na la kukumbuka ni kuhakikisha unalipa kodi kwa wakati kuendana na sera na sheria zinazoratibu aina ya uwekezaji ambao umeufanya. Vipo viwango tofauti vya kodi vinavyobainishwa na utofauti wa sehemu na aina au kiwango cha uwekezaji ambao umeufanya. Si jambo jema kufanya malimbikizo ya kodi bila sababu ya maana kwa kuwa itakuweka katika hali ya hatari ambayo inatokana na uratibu wa sheria kali zilizopo. Changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni baadhi ya watu ambao wamefanya uwekezaji kwenye maeneo hatarishi, maeneo yenye migogoro, maeneo ya hifadhi, na maeneo yasiyo rasimishwa au kupimwa. Malalamiko yamekuwa ni mengi sana ambayo yanahitaji elimu na ufafanuzi kwa jamii, moja ya jambo linalowasumbua baadhi ya watu ni kwamba wanalipa kodi lakini kwa upande mwingine wameamuliwa kubomolewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujenga kwenye maeneo hatarishi. Hivyo ni muhimu sana kwa mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza baadhi ya changamoto ambazo zinaweza kuepukika.

SOMA; Haya Ndiyo Mambo Matano (05) Yanayoathiri Uwekezaji Wa Ardhi Na Majengo.

Ucheleweshaji Wa Malipo

Watu wengi wamewekeza kwenye kupangisha maeneo na majengo yao kwa matumizi mbalimbali yakiwemo makazi na biashara. Hivyo wengi wao wameweka utaratibu wa kufanyika malipo ya kabla au baada ya muda fulani kutegemea na aina ya makubaliano ambayo yamefanyika baina ya mmiliki na mpangishwaji. Changamoto kubwa inayowakabili wawekezaji wengi ni ucheleweshaji wa malipo kutoka kwa wapangaji ambao kwa namna tofauti huwa ni kikwazo kwa kuwa hawapati mapato ndani ya muda uliokubalika. Ni muhimu sana ukajiwekea utaratibu wa namna bora ya ulipaji ambayo itamuwezesha kulipa kwa wakati na bila usumbufu wowote. Epuka misuguano isiyo na ulazima kwa kusimamia taratibu mlizokubaliana, utashi na utu wa kimazingira. Unapaswa kuwa tayari kwa kuwa hii ni changamoto ya kawaida katika kutafuta uhuru wa kifedha hasa kwa wale wenye marejesho ya mkopo kwenye taasisi za fedha.

Gharama Za Matengenezo

Moja ya jambo linalowasumbua watu wengi ni kuhusu uwajibikaji hafifu wa kufanya matengenezo katika kuboresha na kurudishia baadhi ya vitu ambavyo vimeharibika katika kukidhi matumizi husika kwenye majengo. Maeneo na majengo yaliyopangishwa yanapaswa kufanyiwa matengenezo kila baada ya muda fulani katika kuboresha mwonekano na kukidhi matumizi kutegemea na ubora wa malighafi zilizotumika. Kwa kiasi kikubwa ni muhimu sana kuweka akiba kwa matengenezo ya dharura na kuweka sehemu ya mapato yako kwa matengenezo makubwa na ya lazima pasipo kuathiri mipango na malengo yako. Matengenezo hugharimu zaidi tofauti na kufanyika kwa ujenzi mpya, hivyo ni muhimu ukajiwekea utaratibu wa kuweka akiba ili kumudu gharama za matengenezo ambazo huwa kubwa tofauti na matarajio uliyojiwekea. Pia ni muhimu kutumia malighafi bora ili kuepuka gharama za matengenezo ya mara kwa mara ambazo huathiri mapato kwenye uwekezaji ulioufanya.

Mabadiliko Ya Sera Na Sheria

Maendeleo hayana ukomo, hivyo hatua mbalimbali zinazofanyika kuelekea kwenye kilele cha mafanikio husababisha mabadiliko ya kifikra na utashi katika ubunifu wa mbinu ambazo hurahisisha mfumo wa maisha ya watu. Hivyo mara nyingi hufanyika mabadiliko ya sheria na sera ili kuendana na wakati na kuwa kichocheo kikubwa kwenye maendeleo ya watu binafsi na jamii kwa ujumla. Hivyo ni muhimu sana kuwa makini na kuweka utaratibu wa kujifunza na kufuatilia sera na sheria mbalimbali zinazohusu aina ya uwekezaji ambao umeufanya ili kuepuka misuguano isiyo na ulazima kutoka kwenye mamlaka husika. Sheria na sera mbalimbali zinazoratibu mambo mbalimbali zina athari kubwa sana kwenye maisha halisi ya jamii hiyo, hivyo kama umewekeza kwenye majengo ya ofisi za biashara, hospitali, hoteli, shule, taasisi za fedha, kumbi za starehe, migahawa na vituo vya afya ni muhimu ukafahamu vema taratibu rasmi zinazoratibu aina ya uwekezaji wako ili kuepuka usumbufu na hasara zinazoweza kujitokeza.

SOMA; Fahamu Hatua Tano (05) Muhimu Za Kuzingatia Kabla Hujaanza Kuwekeza Kwenye Ardhi Na Majengo.

Ulinzi Na Usalama

Leo hii kuna idadi kubwa ya watu ambao wapo kwenye hali kubwa ya mashaka baada ya kutambua kuwa wamefanya uwekezaji kwenye maeneo yasiyo sahihi kutokana na sababu mbalimbali. Epuka migogoro isiyo na ulazima kwa kuwekeza sehemu salama na yenye uhakika usio na shaka yoyote. Pia ni muhimu ukaweka utaratibu utakaowezesha watu wote watakaofika kwenye eneo lako wanakuwa salama kwa namna yoyote kwa kuwa huu ni wajibu wa mmiliki na utawajibika kwa lolote litakalo tokea. Na bila kusahau kuweka ulinzi dhidi ya hatari zinazoukabili uwekezaji wako kwa kuhakiksha unakuwa na hati halali ya umiliki, bima dhidi ya majanga asilia, mifumo ya zimamoto na kuweka mfumo rasmi utakao ratibu ulinzi na usalama.  Ni hatari sana kufanya uwekezaji kiholela hali ambayo itakufanya ujutie siku zijazo.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com