Moja ya vikwazo vikubwa sana kwenye mafanikio yetu, ni sisi wenyewe. Mawazo ambayo tunakuwa nayo juu ya vitu au watu fulani, hutuzuia kabisa kuchukua hatua, hutufanya tushindwe kabla hata hatujaanza.

Upo mfano mmoja wa kijana aliyeajiriwa kwenye duka kwa ajili ya kutafuta wateja. Kazi yake ilikuwa kuwatembelea watu na kuwashawishi kununua. Siku moja alielekezwa aende kwenye duka jingine akawauzie kitu, aliambiwa kwenye duka lile huwa wananunua, hivyo hatakuwa na kazi ngumu kuwashawishi. Kijana akaenda na baada ya muda akarudi akiwa ameshauza. Walipoangalia kamuuzia nani, walishangaa, alipoenda siyo alipoelekezwa, alikuwa amekosea. Lakini cha kushangaza zaidi, aliyemuuzia huwa hanunui kwao kabisa, hivyo wanamjua siyo mnunuaji.

gold coins

Kwa kuwa walishajifunza kuwa siyo mnunuaji, basi wanakuwa hawajisumbui hata kumshawishi. Lakini kwa kuwa kijana mgeni alipewa uhakika kwamba ni mnunuaji, alikazana mpaka akaweza kumuuzia.

Yapo mambo mengi kwenye maisha yetu ambayo tumeshajipa mawazo ya aina fulani, ambayo yanatufanya tusijisumbue kuchukua hatua ambazo tunapaswa kuchukua.

Rai yangu kwako leo rafiki yangu, ni ufanye kama ndiyo unaanza upya. Kwenye chochote unachofanya, futa kabisa yale mawazo ambayo ulishajipandikizia kuhusiana na kitu hicho. Fanya kama ndiyo unaanza, kama hujui chochote, halafu weka juhudi kuhakikisha unapata matokeo bora.

SOMA; UKURASA WA 253; Hakuna Aliye Bora Au Hovyo Zaidi Yako.

Jaribu leo kwa hatua ambazo ni ndogo, kwenye vitu ambavyo ulishavikatia tamaa kabisa. Labda ni mteja ambaye umeshakata tamaa kwamba hatanunua tena kwako. Fikiria kama ndiyo unamjua kwa mara ya kwanza na mshawishi anunue. Labda ni mtu ambaye umeshamweka kwenye kundi la watu ambao hawakulipi madeni yako, anza leo ukitaka akulipe deni lako, bila ya kuwa na mawazo kwamba hakulipi.

Chochote unachofanya, ambacho unakijali kweli, futa kabisa mawazo yote hasi uliyonayo juu ya kile unachofanya na anza upya. Anza ukiwa na hamasa ya kufanya makubwa, na kwa sehemu kubwa utaweza kufanya makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog