Zipo tamaduni nyingi ambazo watu wengi wanazo kulingana na kabila au taifa wanalotoka. Hata hivyo tamaduni hizo zinaweza zikawa za msaada au zisiwe na msaada hiyo tu inategemea na utamaduni wenyewe jinsi ulivyo.
Lakini katika makala haya sitazungumzia tamaduni hizi za kabila na kabila au utamaduni wa taifa na taifa, hapa leo nitazungumzia utamaduni wako wewe binafsi ambao unaweza ukaujenga na kukuwezesha kufanikiwa.
Si unajua tena unaweza ukajenga utamaduni wako mwenyewe yaani utamaduni wa jinsi unavyotaka kuendesha maisha yako na usiingiliane na kitu chochote na ukakukupa mafanikio? Naona unanishangaa, naamimi muda utafika utanielewa.
Utamaduni ambao nataka kuongelea hapa kwako leo, ni utamaduni wa kufikiri mambo ambayo yanaweza kukusaidia kwenye maisha na si kukuangusha. Unajua kila mtu anafikiri, ila kwa bahati mbaya wengi wanafikiri mambo yakuyaharibu sana.
Anza kuchukua muda wako kutafakari kile ambacho unaona kinaweza kubadili maisha yako, badala ya kukaa na kulalamika pasipo kuchukua hatua zozote. Malalamiko peke yake hayawezi kukusaidia, kitakachokusaidia ni wewe kuchukua hatua.
Chochote unachokizingatia kwenye maisha yako, zingatia kile ambacho unaona kina mchango wa kubadli maisha yako. Usizingatie kile ambacho unaona kinaweza kukuangusha kama malalamiko.
Wanaolalamika ni watu ambao hawapigi hatua kwenye maisha yao. Hiyo inakuja kwa sababu wanakuwa ni watu ambao badala ya kuweza kuchukua hatua, wanajikuta hatua zao wanazichukua kwenye midomo yao.
Unatakiwa kujiuliza kama unalalamika au unalaumu sana, basi ujue kabisa upo nje ya mafanikio yako na unajenga utamaduni mbovu kabisa. Haitawezekana wewe ufanikiwe kama upo kwenye hali hiyo ya kulalamika, unatakiwa ufikiri kile ambacho unaona kitaweza kukusaidia kufanikiwa.
Unatakiwa kuwa na utamaduni wa kufikiri yale yanayokusaidia tu na si kufikiri yale yanayoweza kukuzuia wewe kupiga hatua. Angalia una uwezo wa kufanya kitu kipi ambacho kitu hicho kwa kukifanya kwako kitakufanya uweze kusonga mbele.
Kama nilivyosema huna haja ya kuendelea kulalamika bila kuchukua hatua. Kuchukua hatua ni muhimu sana katika kuweza kukufikisha kwenye safari yako ya mafanikio uyatakayo. Pasipo kuchukua hatua na ukawa ni wa kulalamika utakwama tu.
Badala ya kuhofia kwa yale ambayo yameshatokea kwenye maisha yako na kujawa na wasiwasi mwingi, badilisha mwelekeo mara moja na kuanza kuangalia ni wapi ambapo unaweza ukaweka juhudi za kuweza na kufanya kitu cha kukusaidia kufanikiwa.
Sehemu ambayo utaweka mazingatio yako, sehemu ambayo utaweka akili yako yote hapo na kufanyia kazi, hiyo ndiyo sehemu ambayo itaanza kukupa mafaniko yako na sio kinyume cha hapo kama unafikiri hivyo.
Hakuna uchawi au muujiza ambao unaweza ukatokea kwa wewe kama utakuwa huna utamaduni wa kuzingatia yale mambo yanayokusaidia na badala yake unazingatia mambo yanayokuangusha kama vile hofu na kulalamika kwingi ambako hakuna msingi wowote kwako.
Kwa uhakika unapaswa kujua mambo hayo hayawezi kukusaidia sana kufikia mafanikio yako. Utake usitake utakwama tu kama mazingatio yako yanazingatia sana mambo duni ya kuweza kukuangusha badala ya kukufanikisha.
Kwa hiyo cha kufanya leo wewe, ni kuchukua muda wako kujenga utamaduni wa kufanya mambo ambayo unaona moja kwa moja yataweza kubadili maisha na si kufanya mambo ambayo hayawezi kubadili maisha yako.
Mafanikio katika maisha yanajengwa kwa kuchukua hatua ya mambo ambayo yanabadili maisha yako na kuyafikiri mara kwa mara kwa kuangalia ni njia ipi ambayo unaweza kuyatenda tena kwa namna ya kimafanikio.
Utakuwa unajidangana sana na unajiangusha ikiwa kila wakati unatafakari yale yanayobomoa maisha yako. Usijaribu hata mara moja kutafakari mambo haya, kwani mambo haya yanaharibu maisha yako na yatakufanya ushindwe.
Kama nilivyosema, jenga utamaduni sahihi wa kufakari mambo haya yanayojenga maisha yako ili uweze kufanikiwa katika maisha yako kwa kishindo kikubwa. Sina shaka hilo linawezekana kwako na kikubwa chukua hatua za kufanyia kazi hilo.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatumia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Tovuti; http//www.amkamtanzania.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com