Watu wanasema kama kufanya kazi kwa nguvu na juhudi kungekuwa ni ufunguo wa mafanikio, basi punda wangekuwa na mafanikio makubwa sana.
Ni kweli kwa asili, punda anabeba mizigo mizito sana na anaweza kustahimili mazingira magumu sana kama ya ukame. Lakini siyo mnyama mwenye mafanikio makubwa.
Kwa upande wa pili, simba ni mnyama anayeonekana kuwa mvivu sana, analala kwa masaa 20 kwa siku na anawinda kwa masaa mawili mpaka matatu kwa siku. Pamoja na uvivu huu, bado simba ni mnyama mwenye mafanikio makubwa.

Nini kinatofautisha wanyama hawa?
Au tukirudi kwetu sisi binadamu, nini kinatofautisha mtu anayefanya kazi kila siku kwa masaa zaidi ya kumi, lakini hakuna hatua anayopiga. Wakati kuna mwingine anafanya kazi masaa machache, labda na kwa siku chache ila anafanikiwa kupiga hatua kubwa?
Jibu lipo hapa, kiwango cha hatua ambazo mtu anachukua.
Kuna hatua za kawaida ambazo wengi huwa wanachukua, na haziwaletei matokeo makubwa bali yale ya kawaida.
Na kuna hatua kubwa na za juu sana ambazo wengine wanachukua, ambazo zinawaletea matokeo makubwa na mafanikio makubwa pia.
Kama unataka kufanikiwa, unahitaji kuchukua hatua kubwa sana, hatua ambazo kwa wengine zinaonekana ni hatari, lakini wewe unapaswa kuzichukua na kuzichukua kwa umakini ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
SOMA; UKURASA WA 979; Kubali, Kisha Chukua Hatua.
Kuwinda wanyama ni kitu hatari na kinachohitaji kuchukua hatua kubwa na kutumia akili pia, simba anaweza hilo, anaweza kumkimbiza mnyama kwa muda mrefu bila ya kuchoka, na hata anapomkamata, inamchukua nguvu na muda kuweza kumdhibiti. Lakini kubeba mizigo au kula nyasi siyo hatua kubwa, hakuna hatari yoyote, na ndiyo maana punda anaishia kuwa kawaida, na simba anakuwa na mafanikio.
Kila siku ya maisha yako, kumbuka mifano hii miwili, simba na punda, na jiulize je kwa hatua unazochukua, unakuwa simba au unakuwa punda? Jisukume kuchukua hatua za kisimba, ili uweze kufanikiwa zaidi. Na kataa kabisa kuwa punda. Kila unapofanya kitu cha kawaida, ambacho kila mtu anaweza kufanya na amezoea kufanya, hata kama utafanya kwa nguvu kiasi gani, umechagua kuwa punda, na punda hawana mafanikio.
Kuwa simba, chukua hatua kubwa, chukua hatua hatari, fanya mambo makubwa na ya tofauti, ambayo hayajazoeleka na wengine wanayaogopa, huko ndipo mafanikio yamejificha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog