Rafiki yangu mpendwa,
Zipo njia nyingi za kupata thamani zaidi unapohudhuria semina ya kushiriki moja kwa moja, ambazo huwezi kupata kwa kujisomea mwenyewe au kushiriki semina kwa njia ya mtandao.
Ukiacha yale masomo utakayojifunza kwenye semina, kuna vitu vingine vikubwa unaweza kunufaika navyo pia. Moja ya vitu hivyo ni kukuza mtandao wako zaidi. Mtandao wako ni muhimu sana kwa mafanikio yako. Wanasema ukubwa wa mtandao wako, yaani wale wanaokujua na unaowajua ndiyo sawa na ukubwa wa mafanikio yako.
Hivyo unapopata nafasi ya kushiriki semina yoyote ya moja kwa moja, hakikisha unawajua watu wapya, ambao ulikuwa hujuani nao.
Na ili uweze kunufaika na kukuza zaidi mtandao wako kwenye semina unayoshiriki, yapo mambo kumi uhimu sana ya kuzingatia.

Hapa nakwenda kukushirikisha mambo hayo ili uweze kunufaika sana na semina unazoshiriki;
- Kuwa na mpango wa kukuza mtandao wako.
Unapoenda kwenye semina ya kushiriki moja kwa moja, kuwa na mpango wa watu wa aina gani unataka kujuana nao. Pia jua ni vitu gani unataka kujifunza kutoka kwa wale unaotaka kujuana nao. Ukienda ukiwa na mpango wa aina hii inakuwa rahisi kwako kuliko ukienda bila mpango wowote.
- Kuna na kianzilishi sahihi cha mazungumzo.
Watu wengi huwa hawana kianzilishi sahihi cha mazungumzo, kinachotokea ni wanapopata nafasi ya kuzungumza na wengine, wanakosa kabisa cha kuzungumza au wanaanzisha mazungumzo ambayo wengine wanashindwa kuyaelewa. Unaposhiriki kwenye semina, kuwa na kianzilishi sahihi cha mazungumzo, na mara nyingi penda kujua kuhusu mtu, anafanya nini na unawezaje kunufaika na anachofanya. Pia kuwa tayari kujieleza kwa mwingine.
- Kuwa mtu mwenye kufikika.
Unaposhiriki kwenye semina, mara zote kuwa wazi kwa kukuza mtandao wako zaidi. Hakikisha inakuwa rahisi kwa kila mtu kukufikia. Muda wa mapumziko panga kujuana na watu mbalimbali na usitumie muda wako mwingi kwenye simu au vitu vingine. Unapokuwa bize na simu muda wote, watu wanachukulia kwamba huna muda na wao na hivyo kukuepuka.
- Usibague nani wa kuongea naye na nani wa kuacha.
Unaposhiriki semina ya moja kwa moja, usiwe na ubaguzi ni watu wa aina gani unataka kuongea nao na kutengeneza nao mahusiano, na muhimu zaidi usilenge wale ambao ni maarufu pekee kwako. Kuwa tayari kuongea na kila mtu, kwa sababu kuna kitu cha kujifunza kutoka kwa kila mtu. Na kwa wale ambao hutegemei makubwa, ndiyo unajifunza mengi na kupata fursa kubwa zaidi.
- Kuna na kadi yako ya biashara.
Kadi yako ya biashara ni njia rahisi ya kujitambulisha kwa wengine na hata kuwaachia alama ya mawasiliano na wewe zaidi kwa baadaye. Hivyo unaposhiriki semina ya moja kwa moja, hakikisha unakuwa na kadi zako za kibiashara (business cards) ambazo zinakutambulisha vizuri wewe ni nani na unafanya nini.
- Kuwa mtu wa kusikiliza zaidi ya kuongea.
Mtu ambaye kila wakati ni yeye tu anaongea na hasikilizi, huwa havutii watu wengi. Na kumbuka unapoongea hakuna kitu kipya unachojifunza. Hivyo ili kunufaika zaidi na semina ya moja kwa moja, pamoja na kukuza mtandao wako, kuwa msikilizaji zaidi ya muongeaji. Anayesikiliza anamvutia kila mtu.
- Eleza ni kipi wengine wanaweza kunufaika nacho kutoka kwako.
Unapokuwa kwenye mazungumzo na wengine, usiishie tu kueleza nini unataka kutoka kwa wengine, bali pia waeleze wengine nini wanaweza kunufaika nacho kutoka kwako. Hii itawafanya watu waone thamani zaidi kwako na kuwa tayari kukutafuta zaidi, kwa sababu wanajua watanufaika zaidi.
- Jua watu wengi kwenye semina wapo kwenye hali uliyopo wewe.
Kinachowafanya mkutane kwenye semina ni kitu kimoja, wote mnakuwa na kiu ya kujifunza na kuweza kupiga hatua zaidi. Pia unakuta wote mna changamoto zinazofanana. Kwa kujua hili, ni rahisi kwako kutengeneza mahusiano yenye faida kwa kila mmoja wenu katika kupiga hatua zaidi na hata kutatua changamoto ambazo wote mnapitia.
- Jichanganye na watu tofauti tofauti.
Sisi binadamu huwa tunapenda kukaa na wale watu ambao tayari tumeshazoeana nao. Hili pia hutokea kwenye mikutano, hata kama hujuani na mtu kabisa, wale wa kwanza unaojuana nao mapema, unajikuta ndiyo unakaa na hao hao muda wote. Usifanye kosa hili, jichanganye na watu wengi uwezavyo, zungumza na watu mbalimbali. Hakuna atakayekushangaa, kwa sababu kila mtu anataka kujuana na watu wengi zaidi.
- Usisahau kuwa mfuatiliaji baada ya semina.
Watu wengi hupoteza kabisa mawasiliano na wale ambao wamekutana nao kwenye semina. Hawawasiliani nao kwa muda mrefu mpaka watu hao wanawasahau kabisa. Kuwa mfuatiliaji baada ya semina, pale ambapo unahitaji kufanya hivyo. Endelea kuboresha mahusiano uliyoanzisha, kwa sababu mahusiano yoyote yanaimarishwa au kuuvunjwa na mawasiliano. Wasiliana kwa salamu mara kwa mara, na unapokuwa na kitu kinachoweza kumfaa mtu mpe taarifa. Hakikisha mawasiliano yako ni ya kuongeza thamani na siyo ya usumbufu.
Rafiki, hizo ndizo njia kumi za kunufaika zaidi pale unaposhiriki semina ya moja kwa moja. Njia hizi zinakuwezesha kukuza mtandao wako zaidi na kujuana na wengi zaidi. Kumbuka ni kupitia wengine ndiyo unapata mawazo bora, fursa mbalimbali na hata kujifunza zaidi.
KARIBU KWENYE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.
Rafiki, tarehe 03/11/2018 ndiyo siku ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, semina hii itafanyika kwenye moja ya hoteli zilizopo jijini dar es salaam.
Itakuwa ni semina ya siku nzima, kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa moja jioni. Yatakuwa ni masaa 12 ya kujifunza, kujuana na wengine, kuhamasika na kuweka mkakati wa kwenda kufanyia kazi kwa mwaka mzima.
Ada ya kushiriki semina hii ni tshs 100,000/= (laki moja) ada ambayo itajumuisha huduma zote za siku ya semina, kuanzia chai, chakula cha mchana, vitafunwa vya jioni, vijitabu vya kuandikia na kalamu.
Ili kupata nafasi ya kushiriki semina hii, unapaswa kulipa ada yako kabla ya tarehe 31/10/2018, ambayo ndiyo tarehe ya mwisho ya kulipia ada.
Pia nafasi za kushiriki semina hii ni 100 pekee, na zilizobaki ni chache sana. hivyo kama hutaki kukosa nafasi hii, lipa ada yako mapema ili tuweze kuwa pamoja kwenye semina hii.
Nakusubiri kwa hamu sana rafiki yangu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, kwa sababu yapo mengi mazuri nimekuandalia kwa mafanikio yako kwa mwaka 2018/2019.
Namba za kufanya malipo ili kushiriki semina hii ni MPESA- 0755 953 887 au TIGO PESA/AIRTEL MONEY – 0717 396 253. Majina ya namba hizo ni AMANI MAKIRITA. Ukituma fedha tuma na ujumbe wa kueleza umefanya malipo ya semina, ukiambatana na jina lako na namba yako ya simu kwa ajili ya kupewa taarifa zaidi za semina.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL