Mpendwa rafiki yangu,

Mara nyingi imekuwa ni kawaida yetu sisi binadamu kutumia hisia zaidi kuliko akili. Na hata tafiti zinaonesha kwamba maamuzi mengi yanayofanya kila siku yanaongozwa na hisia na siyo kutumia akili. Watu wanaotumia akili ni wa chache sana.

Na hili ukiliangalia ni kweli, katika maisha yetu majanga mengi yanayotokea ni kwa sababu ya kushindwa kufanya maamuzi kwa kutumia akili. Pale tunapofanya maamuzi tukiwa na hisia yoyote ile akili zetu huwa zinakuwa chini sana na hisia zinakuwa juu.

Hisia zikiwa juu na akili inakuwa chini. Ndiyo maana unakuta mara nyingi mtu anakosea pale anapofanya maamuzi kwa kutumia hisia.

Kinachotokea katika maisha yetu baada ya kuruhusu hisia zitutawale ni majuto. Ukiangalia watu wengi waliongozwa na hisia kufanya jambo fulani sasa hivi huwa wanajuta sana kwa mateso wanayopata. Siku zote hisia huwa haimwachi mtu salama lazima tu itakugharimu kwa namna yoyote ile kwenye maisha yako.

Jaribu kuangalia hata wale wanaobaka, ni kwa sababu ya kukubali kuongozwa na hisia mpaka wanakubali kufanya kile ambacho hisia inataka kwa muda ule, vipi kuhusu mateso wanayopata kwa sasa wakiwa katika kifungo?  Ule uhuru wao wote wameupoteza na kwa sasa wanajuta na kusema laiti ningelijua.

Huenda ulimwadhibu mtoto ukiwa na hasira, baada ya hasira kuishi unaanza kujuta na kujilaumu kwanini umefanya kile ulicho. Baada ya hisia kuwa chini na fikra kuwa juu ndiyo tunaanza kuona ukweli kwamba kile tulichofanya siyo sahihi kabisa.

Na huwa tunajikuta tunahatia ndani yetu, ile hatia inatuambia kabisa tulichofanya sasa siyo sahihi kwenye maisha yetu, huwa inatusuta kwa kile tulichofanya.

SOMA; Sifa Nne Za Kuangalia Wakati Wa Kuchagua Kazi Au Biashara Ili Iwe Na Maana Kwako Na Uweze Kufikia Mafanikio Makubwa.

Hatua ya kuchukua leo, kwa kuwa tumeona hisia ni hasara, tunapaswa kufanya maamuzi ya kutulia pale unapokuwa na hisia yoyote ile, jicheleweshe kuchukua hatua na baada ya kujichelewa utakuja kujiona ni mshindi sana.

Kwahiyo, hatuwezi kuzuia hisia zisitokee bali tunaweza kuzitawala hisia ili zisilete madhara kwenye maisaha yetu. Badala ya kukubali kuongozwa na hisia sisi tunakataa kuongozwa na hisia.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana