Zamani, wakati hakukuwa na fursa rahisi za kujifunza na kupata maarifa na taarifa, walioweza kukariri vitu vingi ndiyo walionekana kuwa na akili. Na ndiyo maana mfumo mzima wa elimu umejengwa kwenye kukariri, kwamba yule anayeweza kukariri kwa wingi na kujibu maswali ya mtihani ndiye aliyefaulu.
Hili lilikuwa na mantiki kwa sababu ukishakuwa kwenye kazi yako, unapaswa kukumbuka yale muhimu kwa urahisi, kwa sababu kama umesahau, ilikubidi uende maktaba kutatufa kitabu na kusoma.
Chukua mfano ni daktari, na unamtibu mgonjwa, umeona dawa fulani ndiyo itamfaa, lakini hukumbuki dozi yake kwa usahihi. Kama ni mwaka 1990, ingekubidi uende maktaba, utafute kitabu cha madawa, uitafute dawa hiyo na kujua dozi yake sahihi. Unaona kwa nini ilikuwa muhimu kukariri, kwa sababu kulikoa muda na kurahisisha ufanyaji wa kazi.
Lakini mwaka 2018, unamtibu mgonjwa na umesahau dozi kamili ya dawa, unaingia kwenye mtandao wa google, unaandika jina la dawa na kuuliza dozi yake na chini ya sekunde moja, majibu yanakuja ya dawa hiyo, dozi sahihi na mengine unayotaka kujua kuhusu dawa hiyo.
Sasa huo ni mfano mmoja kwenye udaktari, lakini ndivyo mambo yalivyo kwenye kila taaluma, kwamba ujanja siyo kukariri tena, kwa sababu ndani ya sekunde moja, unaweza kupata jibu la kitu chochote ulichosahau.
Sasa kumekuwa na watu wanaosema kuna haja gani ya kuwa na taaluma fulani wakati kila mtu anaweza kugoogle? Na hapa ndipo kinakuja kitu kinachowatofautisha watu, kitu hicho ni namna ya kufikiri. Daktari na mgonjwa wanaweza kugoogle kitu kimoja, wakasoma taarifa moja, lakini ikawa na manufaa zaidi kwa daktari kuliko kwa mgonjwa. Kwa sababu daktari anaweza kufikiri na kuchakata taarifa hiyo kwa tofauti kabisa na anavyofanya mgonjwa.
Hivyo basi, kumbe kinachotuwezesha kuwa tofauti zama hizi siyo kukariri, bali kufikiri. Hivyo eneo moja la kuweka nguvu zako ni kujijengea uwezo wa kufikiri kwa usahihi, na ukishaweza kufikiri, utaweza kutumia vyema maarifa na taarifa nyingi zinazopatikana kufanya maamuzi sahihi.
Kama huwezi kufikiri kwa usahihi, maarifa na taarifa nyingi zinazopatikana zitakuwa usumbufu kwako na zitakupoteza kabisa.
Jifunze jinsi ya kufikiri kwa usahihi, na utaweza kufanya maamuzi sahihi kila wakati.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,