Siku kama ya leo, yaani tarehe moja ya mwezi wa kwanza, miaka mitano iliyopita, niliandika ukurasa wa kwanza kwenye makala hizi za kurasa za maisha ya mafanikio. (Soma; Kurasa 365 Za Mwaka 2015, Fursa Muhimu Kwako Kujifunza. na KURASA YA 01; Maisha Unayoishi Ni Yako.)

Sikukaa chini na kusema nitaandika kurasa hizi kwa miaka mitano au kumi au ishirini ijayo, bali nilijiambia kila siku ambayo ninaamka na kuwa hai, basi nitaandika makala fupi ya kurasa.

Na nimekuwa natekeleza hilo kila siku, mara nyingi asubuhi ninapoamka na pale ninapokuwa kwenye mazingira magumu, basi wakati mwingine wowote kwa siku, lakini kwa miaka mitano sijaruhusu hata siku moja ipite sijaandika makala hizi fupi za kurasa.

Wakati mwingine makala zinakuwa fupi sana, wakati mwingine zinakuwa ndefu sana, lakini lengo kuu ni kuandika kitu kila siku, kuyaweka mawazo yangu na yale niliyojifunza kwenye ujumbe mfupi ambao mtu anaweza kujifunza na kuondoka na hatua za kuchukua.

Hivi ndivyo unavyoweza kufanyia kazi lengo na mpango wowote unaojiwekea, usiangalie unafika wapi, bali wewe angalia unafanya nini kila siku, kisha fanya hivyo.

Wote tunajua na imesemwa sana, safari ya maili elfu inaanza na hatua moja. Na wale wanaofika kwenye kilele cha mlima hawakuamka na kujikuta hapo, bali walipiga hatua moja baada ya nyingine mpaka wakafika kwenye kilele.

Usifikiri wewe ni wa tofauti, usifikiri umekutana na siri ambayo wengine hawajaijua, kwamba utaweza kufanikiwa kwa miujiza, jiepushe na fikra hizo, ondokana na wenye ushawishi huo.

Weka lengo laki kubwa, kisha weka mchakato wa hatua ambacho utakwenda kuzifanya kila siku ili kufikia lengo, na kisha kila siku chukua hatua ulizopanga kuchukua.

Kuna ugumu wowote hapo rafiki yangu? Hakuna. Lakini sisi wenyewe tumekuwa tunachagua kuyafanya mambo kuwa magumu, pale tunapoanza kutafuta njia rahisi na ya mkato ya kupata kile tunachotaka. Njia hiyo huwa haipo na hivyo tunapoteza muda na nguvu kwa yasiyo na umuhimu.

Nikutakie heri ya mwaka mpya 2020, tulianza pamoja safari hii ya kurasa 2015 na naendelea kukuahidi kwamba kila siku ninayoamka na kuwa hai, nitaandika makala fupi ya kurasa, kwa ajili yangu na kwa ajili yako rafiki. Makala hizi zitaendelea kuwa za kutukumbusha yale muhimu kuhusu mafanikio, kuturekebisha pale tunapotetereka na kutuongoza kuweza kufanya makubwa sana.

Weka lengo, weka mchakato, chukua hatua kila siku, hivyo ndivyo mafanikio yanavyofikiwa, na ninaamini utafanya hivyo rafiki ili tuendelee kuwa pamoja na wote tufanikiwe zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha