Kila mmoja wetu ana sauti fulani iliyopo ndani yake.
Sauti ambayo mara nyingi huwa ina wasiwasi na mashaka, inaona ugumu na kushindwa kwenye kila jambo. Sauti hii huwa haiamini kwenye uwezo mkubwa ulionao.
Hii ni sauti unayopaswa kuwa nayo makini sana, kwa sababu usipojua udhaifu wake, itakuwa kikwazo kwako kupiga hatua.
Fikiria umesoma mahali kuhusu tabia za watu wenye mafanikio, umetoka ukiwa na hamasa kwamba unakwenda kutekeleza tabia hizo. Wakati wa utekelezaji unapofika sauti hiyo ya ndani yako inakujia. Inakuambia acha kujidanganya, huwezi kufika ngazi walizofika hao wengine, hali yako hairuhusu, mazingira yako siyo kama yao na ushahidi mwingine mwingi ambao sauti hii itakupa.
Unachopaswa kujua ni kwamba kila mmoja wetu huwa ana sauti ya aina hii. Wale unaowaona wanapiga hatua siyo kwamba hawana hii sauti, bali wamejua jinsi ya kuidhibiti isiwe na madhara kwao.
Kitu kingine cha kujua ni kwamba hakuna mtu mwingine anayesikia sauti ya ndani yako. Japo sauti hiyo itakuaminisha kwamba kila mtu anafuatilia na hivyo ukishindwa watakucheka, huo ni uongo. Kila mtu anapambana na yake, hakuna anayesumbuka na mambo yako.
Kwa kujua haya sasa, kila unapopanga kufanya kitu halafu sauti hii inakujia, iambie nimekusikia, lakini sitafuata hicho unachotaka, mimi ni zaidi ya wewe, wewe ni sauti tu, mimi ni nafsi inayotawala kila kilicho ndani ya mwili huu, ikiwa ni pamoja na wewe kama sauti.
Ukishaiambia hivyo, fanya kile ulichopanga kufanya, ukirudia hivi mara kadhaa, sauti hiyo inakosa nguvu kabisa na utakuwa huru kupanga na kufanya mambo yako bila ya kujali au kuhofia chochote.
Mchawi wako wa kwanza ni wewe mwenyewe, adui yako ni wewe, anayekuangusha ni wewe, kwa sababu umeipa sauti ya ndani yako nafasi kubwa ya kukutawala, ni wakati wa kubadili hilo sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha, ni kweli sauti yangu naisikia Mimi mwenyewe na nimepata mbinu ya iuidhibiti.
LikeLike
Asante sana kocha, ni kweli sauti yangu naisikia Mimi mwenyewe na nimepata mbinu ya kuidhibiti.
LikeLike