Hata kama utakuwa mwema kwa kila mtu na kuwasaidia wengi uwezavyo,

Hata kama utajali mambo yako na kutokujihusisha na yale yasiyokuhusu,

Hata kama utawapa watu kila wanachotaka kutoka kwako,

Bado kuna watu ambao watafurahia kifo chako.

Siku utakayokufa, japo wengi watakulilia, lakini kuna ambao watafutahia wewe umekufa.

Japo siyo wote watakaofanya hivyo kwa nia mbaya, wengine inawabidi tu kufurahia kwa ndani, hata kama hawaoneshi kwa nje.

Labda ni mtu anayetaka kupata kazi unayofanya, au mshindani wako kwenye biashara uliyopo. Inaweza kuwa pia mtu ambaye mlikwazana siku za nyuma sana na umeshasahau. Lakini pia, atakayeuza jeneza utakalozikwa nalo, atafurahia kifo chako.

Kujua ukweli huu, unatusaidia sana kuacha kujidanganya kuhusu maisha, lakini pia kukabiliana na watu kama walivyo.

Badala ya kutaka kila mtu akuchukulie kama unavyotaka wewe, waache watu wakuchukulie kama wanavyotaka wenyewe. Wajibu wako ni kufanya kile ambacho ni sahihi, na siyo kuwafanya watu wakuchukulie utakavyo wewe.

Waelewe watu, ielewe asili yetu binadamu na hutakuja kuumia. Kwa sababu hiki tulichojifunza kwamba kitatokea ukifa, jua kwamba kitatokea mara nyingi kabla hujafa.

Mfano kwenye kila jambo gumu utakalopitia, kwa kila tatizo utakalokutana nalo, kwa kila changamoto, kuna wengi watafurahia. Hata uwe mwema kiasi gani, bado kuna wengi watafurahia matatizo yako, hata wale ambao ulikuwa unawasaidia sana kabla hujawa na tatizo.

Elewa hili na ishi maisha yako bila ya kuruhusu uvurugwe na yeyote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha