Mpendwa rafiki yangu,

Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni matunda ya ndoa pia.

Watoto wametofautiana kwa vingi, huwezi kukuta watoto wamefanana kwa kila kitu hata mapacga wa kufanana hawajafanana kwa kila kitu. Kila mtu ana upekee wake.

Ndiyo maana wazazi wanaalikwa kuwapokea watoto jinsi walivyo. Kila mmoja ana udhaifu wake na hivyo unaalikwa kuwapokea watoto uliopewa bila kuwabagua.

Epuka kuwagawa watoto kwa njia za waziwazi kabisa, hii inaleta mpasuko katika familia. Upendeleo katika familia unaleta mpasuko na kuzaa chuki, tukishakuwa na chuki, basi inakwenda kuzaa mauti.

Ukiwa mzazi, kuwa mtu wa haki maana wote ni wa kwako na kila mmoja mpe haki yake bila upendeleo. Toa upendo kwa watoto wote ulionao na kila mtoto mpe muda na jua udhaifu na uimara wake na msaidie katika makuzi yake mbalimbali.

Hakuna sehemu ambayo mtoto anajisikia mahali salama na ulinzi kama anavyokuwa na mzazi wake. Jaribu kuwa mpole na usiwe mkali maana ukali utamfanya mtoto kushindwa kukuambia vitu vingi kwa sababu ya ukali wako hata kama anapitia magumu.

Leo tunakwenda kujifunza namna ya kugundua uwezo wa mtoto wako uko wapi.

Sisi binadamu tumegawanyika katika makundi mawili. Hata watoto wetu nao wako katika makundi hayo hivyo ukishawajua itakusaidia sana katika malezi ya mtoto wako.

Kuna watu ambao huwa wanauwezo mkubwa sana wa kufanya mambo asubuhi au mchana na kuna watu ambao wanakuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo yao usiku.

Natumaini hata hili umeshaliona kwako, wako wale ambao wakisoma au kuandika usiku wa manane akili zao ndiyo zinakuwa fiti sana na wako ambao wao usiku wanakuwa hawana ufanisi ila mchana.

Sasa utawezaje kugundua uwezo wako mtoto wako kama uko usiku au mchana. Mtoto anayeweza kuamka mapema asubuhi yeye mwenyewe bila kulazimishwa huyo uwezo wako wa kutenda miujiza uko asubuhi. Na tabia zake huwa anakua anapenda sana kuwahi kulala na kuwahi kuamka hawezi kukaa usiku muda mrefu.

Wako watoto ambao asubuhi kuwahi kuamka inakuwa changamoto kwao. Wanachukua muda mrefu kuamka asubuhi na wanachukua muda mrefu kulala usiku. Wanaweza kukaa muda mrefu usiku na wakawa hawana hata usingizi na mwingine hata muda huo ndiyo anachukua daftari au kitabu anasoma. Hapa utagundua kuwa mtoto wa namna hii uwezo wake uko usiku ndiyo anakuwa na ufanisi mkubwa.

Kazi yako kubwa ni kukaa na watoto wako, kuwachunguza ni muda gani wanakuwa na ufanisi zaidi na watumie vizuri kadiri ya muda wao wa ufanisi. Kuna mtoto mwingine hawezi kusoma usiku akili yake inakuwa imechoka, na kuna wengine wanaweza kukesha usiku na wanakuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo kuliko muda mwingine wowote ule.

Hata wewe ulivyokuwa unasoma umeliona hili, kuna wale ambao walikuwa wanakesha usiku asubuhi wanalala tu na kuna wale ambao usiku wanalala tu na asubuhi wanasoma sana.

Hata katika utendaji wetu wa kazi, wako ambao wakifanya kazi zao usiku wanakuwa na nguvu za ajabu za kufanya miujiza, sasa ukishagundua mtoto wako ni wa wakati gani msaidie kumuongoza na kukazia ule muda ambao anapenda kufanya mambo yake.

Usilazimishe watoto wafanane hata siku moja. Wape nafasi ya kukosea ili wajifunze na wawe huru kufanya kile wanachopenda usiwalazimishe wafanye vile unavyotaka wewe wape nafasi ya kuchagua. Kwa mfano, hata katika uvaaji wa nguo, muulize unapenda kuvaa nguo gani leo, rangi nk, anapochagua mwenyewe anajihisi vizuri na anaweza kufanya maamuzi yeye mwenyewe.

Tumezoea kuwafanyia watoto maamuzi kwenye kila kitu hivyo kwa sasa pendelea kumuuliza na awe anafanya maamuzi mwenyewe, kwa mfano, kabla hujampeleka hata shule muulize anapenda kusoma shule gani na kwanini, muda mwingine unaweza kumpeleka mtoto shule unayoipenda wewe mzazi na mtoto akaichukia hii itampelekea hata kufeli darasani. Licha ya kumpa uhuru wa kuchagua na kufanya maamuzi , bado unatakiwa kupima kile anachochagua kama ni sahihi au siyo sahihi na kumpa faida na hasara ya kile alichochagua.

Hatua ya kuchukua leo; mgundue mtoto wako uwezo wake uko usiku, asubuhi au mchana.
Ukishajua yeye ni wa muda gani itamsaidia kutumia muda huo kufanya vizuri na kuong

eza ufanisi kwenye kile anachofanya.

Hivyo basi, ni muhimu kupata muda wa kumchunguza mtoto wako kwenye kile anachopenda kufanya. Ukiwa mfuatiliaji mzuri kwa mtoto au watoto wako utajikuta unajifunza mengi hii ni pamoja na kujua uimara na udhaifu wao uko wapi.

Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.

Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://www.mtaalamu.net/kessydeo , vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana