Upo usemi kwamba mwanafunzi anapokuwa tayari, mwalimu huonekana. Usemi huu una maana kubwa kwamba walimu tayari wapo, ila wanafunzi ndiyo hawajawa tayari. Ina maana yule anayesema hapati wa kumfundisha, hajawa tayari kujifunza.
Sasa nataka tutumie kauli hiyo kwa namna nyingine, kwa upande wa kazi na biashara tunazofanya.
Tunapaswa kuutumia usemi huo kwamba wateja tayari wapo, kinachohitajika ni mwenye kile wanachotaka kuonekana. Hii ina maana kwamba wewe hutengenezi wateja, bali unawaonesha upo, na kuwapa kile ambacho wanakitaka.
Kutumia kauli hii itakuwa na msaada mkubwa kwetu, kwani tutaacha kusumbuka na kutengeneza wateja au kutafuta wateja na badala yake kuweka juhudi kwenye kuonekana na watu sahihi. Unafanya hivyo kwa kueleza manufaa ya bidhaa au huduma unayotoa kwa wale wenye uhitaji.
Mahitaji ya watu ni yale yale, kinachohitajika ni wewe kuweza kuwashawishi unachowauzia kinakidhi mahitaji yao. Ukiendesha biashara yako kwa namna hii, haitakuumiza kichwa, maana utajua watu gani unaowalenga na jinsi ya kuwafikia.
Kauli hii pia ina manufaa kwenye uongozi, wafuasi tayari wapo, wanachohitaji ni mtu wa kuwaongoza. Hivyo popote ulipo, angalia watu wanataka kuongozwa kwenye nini, kisha simama kama kiongozi na wale wanaotaka kuongozwa kwenye eneo hilo watakufuata. Viongozi huwa hawatengenezi wafuasi, bali wanawafanya wafuasi wawaone ni watu sahihi kwao.
Kwa kutokujua misingi sahihi huwa tunahangaika na mambo yasiyo na tija, lakini kwa kujua msingi sahihi kama huu, unaweka juhudi zako eneo sahihi na zinazalisha matokeo ambayo ni makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha kwa maarifa haya , kazi kwangu kuyafanyia kazi
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Ahsante sana
LikeLike
Karibu
LikeLike