Mpendwa rafiki yangu,
Kuna mambo mazuri ya kujifunza sana kutoka katika familia za kiyahudi, ni familia ambazo wazazi wanazingatia sana malezi ya watoto.
Mpaka sasa bado mzazi anawajibika kumtunza mtoto wake wa kike aje kuolewa akiwa bikira, na wanaume nao wanaelekezwa ni familia gani ni salama kuoa. Watoto wanafundishwa mambo mazuri ambayo wakiingia katika familia zao wanakwenda kuyaiishi vizuri.
Katika mahusiano ya leo wale ambao wako katika mahusiano aidha ni wachumba au ndoa wamekuwa ni watu ambao wamejistahilisha kuwa bidhaa ya kuonjwa na kila mtu anayetaka kuonja.
Usikubali kuwa bidhaa ya kuonjwa hata siku moja, hutoweza kuiridhisha dunia, chagua mtu mmoja funga naye ndoa na tulia naye na usiwe mtu wa kuonjesha mwili wako kama bidhaa ya karanga.
Kwa mfano, ukiwa unauza karanga, watu watakuambia tuonjeshe , wako ambao wataonja karanga zako na kusema karanga hizi hazina chumvi, wengine watasema karanga zako hazijakauka vizuri zina maji yaani yako mengi utakayopata.
Mfano huu ni nimeutoa ni kwa dunia ya sasa ambayo watu wengi wanaendeshwa na hisia za mwili ambapo wanaufanya mwili kuwa kama bidhaa ya karanga na siyo hekalu la Mungu.
Wako ambao hawajaingia katika maisha ya ndoa lakini wamekuwa ni watu wa kuonjesha karanga zao na wanafikiri kadiri wanavyoonjesha ndiyo karanga zao zitapendwa kumbe ndiyo kushuka thamani. Wewe unafikiri kama kila mtu ameshaonja karanga zako katika mtaa unaokaa unafikiri utakuwa na njia gani ya kuwashawishi watu kama karanga zako ni za namna gani wakati kila mtu alionja na kujua ladha ya karanga zako?
Usipoteze hadhi yako ya kuufanya mwili wako kuwa kama bidhaa ya karanga.
Jitunze, jiheshimu na watu wanapenda wale wanaojiheshimu na kujitunza.
Wako ambao wameingia maisha ya ndoa lakini hawajatulia katika ndoa zao bado wanaendelea kuhangaika na visima vya watu badala ya kunywa maji ya visima vyao wenyewe. Maji ya kisima chako ndiyo mazuri na uhakika ni mazuri je maji ya visima vya watu wengine huna uhakika kama ni visafi kwa sababu hujui ni wangapi wameshachota maji.
Nini cha kujifunza hapa na kuondoka nacho katika makala ya leo?
Hatua ya kuchukua leo; usikubali kuwa bidhaa ya kuonjwa kama karanga, mwili wako ni hekalu la Mungu na siyo choo ambapo kila takataka hutupwa huko.
Jifunze kujitunza na usiendeshwe na hisia za mwili kwani wewe ni binadamu unao uwezo wa kujidhibiti.
Wazazi, wajibikeni katika malezi ya watoto na wala msibinafsishe majukumu yenu ya kifamilia kwa watu wengine.
Wanandoa tulieni katika ndoa zenu, ishini ahadi za uaminifu kama mlivyokula kiapo na siyo kuonjesha mwili wako kama bidhaa ya karanga.
Kwahiyo,wazazi ni muhimu kuwatunza watoto wenu katika malezi bora ili wafikie miito yao na ili mzazi uyatimize yote hayo yakupasa uwe na utii, uvumilivu , upendo na kupenda majukumu yako ya kibaba au ya kimama.
Kila kitu kinawezekana kama kila mmoja akiwajibika katika nafasi yake kwenye familia.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.
Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana