Kuna mashindano mengi huwa yanaendeshwa kuibua vipaji vya wasanii, yaani kupata wasanii wapya ambao kwa namna fulani hawapati nafasi ya kuonekana. Lakini wasanii wote wakubwa unaowajua, hawajaibuliwa na mashindani ya aina hiyo.

Kuna mashindano mbalimbali ya kibiashara huwa yanafanyika, kuibua mawazo ya biashara ambayo watu wanayo na kuwapa nafasi ya kuyatekeleza. Lakini wafanyabiashara wakubwa na wenye mafanikio hawajaibuliwa na mashindano ya aina hiyo.

Siyo kwamba mashindano ya aina hiyo na vitu vingine vyenye lengo kama hilo havifanyi kazi, vinafanya kwa kiwango fulani, lakini havina nguvu ya kutengeneza mafanikio makubwa kwa walio wengi.

Sababu ni nini hasa?

Sababu ni nguvu ambayo mtu anapaswa kuwa nayo ili aweze kufanikiwa.

Mafanikio makubwa siyo lele mama, yanahitaji mtu aweze kulipa gharama hasa, awe tayari kujitoa kweli kweli na hata anaposhindwa asikate tamaa.

Wale ambao wanavutiwa kufanya kitu kwa sababu wameona kuna shindano, wanakuwa wamevutiwa na zawadi au manufaa ya kushiriki shindano husika. Hivyo hata kama watashinda shindano hilo, nguvu ya kuendelea kupambana na magumu hawatakuwa nayo.

Wale ambao wanafikia mafanikio makubwa kwenye kile wanachokifanya, ni wale ambao wamejitoa kweli kukifanya, wale ambao hawajioni wakiishi bila ya kufanya kitu hicho. Maisha yao ni kitu hicho na hivyo kama wapo hai watakifanya.

Wasanii wanaofanikiwa ni wale wanaoyaona maisha yao ni sanaa, hawasubiri mpaka mashindano yatokee ndiyo wajitokeze kama wasanii, kwa maisha yao yote wanatumia kila fursa kuishi usanii wao.

Kadhalika wafanyabiashara wanaofanikiwa ni wale ambao hawayaoni maisha yao yakienda bila kufanya biashara, wao ni biashara na biashara ni wao. Hicho ndiyo kitu pekee kinawafanya wawe hapa duniani, hivyo hawasubiri mpaka waambiwe kuna shindano la mawazo ya kibiashara au kuna fursa fulani, wao wanafanya hata bila ya kuwepo kwa vitu hivyo, kwa sababu ni maisha yao.

Hivyo ndivyo inavyokwenda kwenye kila eneo la maisha, uandishi na hata huduma nyingine, wanaofanikiwa ni wale walioyatoa maisha yao kwenye kile wanachofanya, ambao hawajioni wakiweza kuishi bila ya kufanya kitu hicho.

Je wewe ni kitu gani ambacho huwezi kuishi bila ya kukifanya, kipi ambacho husubiri mpaka usukumwe au kushawishisha kukifanya. Hicho ndiyo kitu kilichobeba mafanikio yako makubwa. Kitambue vizuri na jipange kukifanya kwa namna ambayo kitawanufaisha wengine na wao kuwa tayari kukulipa kwa namna unavyowasaidia.

Kila mtu kuna kitu ambacho hawezi kuishi bila ya kufanya, kitu ambacho kwa wengine kinaonekana ni kazi kubwa ila kwake ni kama mchezo. Hicho ndiyo kimebeba mafanikio ya kila mtu. Wachache wanaojitambua kwenye hilo ndiyo wanapata mafanikio makubwa.

Jitambue kwenye hilo, na chukua hatua sahihi ili kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha