Huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga.
Mwanzo wa kufanya kitu chochote huwa ni mgumu, lakini baadaye huwa tunajikuta tunafanya bila hata ya kufikiri.
Chukua mfano wakati unajifunza kuendesha chombo chochote kile, iwe ni baiskeli, pikipiki au gari. Mwanzoni ulikuwa unafikiria kila unachofanya, lakini baada ya kuzoea unajikuta unaendesha huku ukifikiria mambo mengine kabisa.
Kwenye kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, nimelijadili hili kwa kina sana, jinsi akili zetu zinavyotengeneza mazoea.
Mazoea haya yana faida na hasara.
Upande wa faida ni yanaipa akili yetu uhuru, badala ya kurudia kuwaza mambo yale yale, inayafanya kuwa tabia na hivyo kuipa akili nafasi ya kuwaza mambo mengine.
Upande wa hasara ni kufanya vitu kwa viwango vya chini kwa sababu ya mazoea, kwa kuwa mtu hafikirii basi anakuwa hana ubunifu.
Leo nakwenda kukushirikisha zoezi ambalo ukilifanya utajenga tabia yenye manufaa kwako, ili kuondokana na tabia ya kuahirisha mambo.
Kila mmoja wetu kuna kitu huwa anatamani sana kukifanya lakini hakifanyi. Anaweza kuwa anasingizia ni muda hana au hajawa tayari. Sababu huwa hazikosekani.
Zoezi unalokwenda kujifunza hapa linavunja kila sababu na kukujengea mfumo mzuri wa kufanya yale muhimu.
Zoezi hilo ni kuchagua kitu kimoja utakachofanya kila siku kwa siku 100 bila kuacha hata siku moja.
Hiyo pekee ndiyo sheria ya zoezi hilo, kufanya kitu kwa siku 100 bila kuacha.
Ni kitu gani unafanya na kwa kiwango gani unachagua mwenyewe, ila ukishachagua unafanya kweli, SABABU HAZINA NAFASI.
Ukiweza kufanya zoezi hili, ukafanya kitu kwa siku 100 bila kuacha hata siku moja, utakuwa umejijengea tabia yenye manufaa sana.

Unaweza kufanya chochote unachotaka kwenye maisha yako katika zoezi hili, mifano ni;
1. Kusoma kurasa unazojipangia za kitabu kila siku.
2. Kuandika idadi ya maneno unayojipangia kila siku.
3. Kufanya mazoezi kwa kiwango unachojipangia kila siku.
4. Kuweka akiba kwa kiwango unachojipangia kila siku.
5. Kuboresha kazi au biashara yako kila siku.
Na mengine mengi unayopanga kufanya.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA tumeanza changamoto hii, ambapo watu wengi wamechagua vitu vya kufanya kwa siku hizi 100 na kwa pamoja tupo kwenye mchaka mchaka mkubwa.
Uzuri wa wanaoifanya changamoto hii kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni kusukumwa na wengi, kwa kuwa mtu anakuwa ameahidi kwa wengi ataifanya changamoto, anasukumwa kuifanya ili asiwaonekane ni mtu asiyetimiza ahadi zake.
Nikushauri na wewe uifanye changamoto hii, uchague kitu kimoja cha kufanya kila siku kwa siku 100 bila kuacha na ukiweza kupata watu wa kufanya nao pamoja, itakusukuma zaidi kuendelea kufanya kila siku kama ulivyojipangia.
Kwa wale ambao wangependa niwasimamie kwa karibu kwa siku hizo 100 ili waweze kujisukuma bila kuacha, natoa nafasi chache kwa wale waliojitoa kweli.
Kama unataka nikusimamie kwa karibu kwenye changamoto ya siku 100 za kufanya bila kuacha, niandikie ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717396253, ujumbe uwe na maneno NAOMBA KUSIMAMIWA KWA SIKU 100.
Nikutakie kila la kheri kwenye zoezi hili la siku 100 za kujenga tabia bora, ndani yako tayari una uwezo mkubwa, hapo ulipo tayari umezungukwa na rasilimali zote muhimu, ni wewe uamue kufanya makubwa na uyafanye kweli ili ufanikiwe.
Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania