Ipo kauli ya kihenga inayosema kwamba tunavuka daraja pale tunapolifikia.
Ni kauli fupi lakini yenye ujumbe mkubwa mno kuhusu maisha.
Mara nyingi huwa tunahangaika na mambo ambayo siyo tu hayapo karibu, bali pia hatuna cha kufanya kuhusu mambo hayo kwa wakati tunasumbuka nayo.
Chukua mfano wa ujenzi, kama unajenga nyumba na ndiyo unaanza kujenga msingi, hutasumbuka sana na taa za aina gani utaweka au rangi gani utapiga kwenye nyumba hiyo.
Hayo ni mambo muhimu, lakini muda wake bado, kwa sasa kuna mengine muhimu zaidi yako mbele yako, kuhakikisha msingi ni imara na ujenzi unakwenda kwa wakati.
Hivyo ndivyo inapaswa kuwa kwenye kila eneo la maisha yetu, kuna mengi tunahangaika nayo ambayo yanatupotezea tu muda. Na hayo ndiyo huwa yanatupa msongo mkubwa, kwani hatuna cha kufanya katika mambo hayo.
Endesha maisha yako kwa utofauti, chagua kuhangaika na yale yaliyo mbele yako kwa wakati husika, yale unayoweza kuchukua hatua kuyaathiri.
Hii haimaanishi upuuze ya baadaye, yape uzito yanayostahili, lakini usiyaruhusu yaingilie kukamilisha yaliyo mbele yako sasa.
Jua kuna daraja mbele, lakini usifikirie sana utalivukaje wakati bado hujalifikia. Kwa sasa fikiria jinsi ya kwenda na njia uliyonayo kwa usalama. Unaweza kusumbuka na daraja ambalo hujalifikia, ukakosa umakini na ukapata ajali inayokuzuia hata usilifikie daraja.
Ni mazoea yetu binadamu kufikiria zaidi yale yajayo, kwa kuwa hatuna uhakika nayo na tunapenda sana uhakika. Lakini huko ni kujidanganya, hata uyafikirie kiasi gani, hilo halitakupa uhakika. Kazana na yaliyo mbele yako sasa na utaweza kufanya makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,