2273; Marudio…

Kumbuka wimbo ambao unaupenda sana, umeusikiliza au kuuangalia mara ngapi?
Kumbuka chakula unachokipenda sana, umekila mara ngapi kwenye maisha yako?
Kumbuka somo ambalo umewahi kufaulu kuliko mengine ulipokuwa shuleni, ulilisoma mara ngapi?
Yale yote muhimu na unayoyapenda, umekuwa unayarudia rudia kila mara.
Mziki unaoupenda huwa unausikiliza au kuuangalia kila mara, bila ya kuchoka.
Chakula unachopenda huwa unakila mara kwa mara na hukichoki.
Na somo ulilolipenda zaidi shuleni, ulikuwa unarudia kulisoma zaidi kuliko masomo mengine na ukalifaulu ziadi.
Sasa inapokuja kwenye mafanikio, kwa nini hutaki kutumia kanuni hiyo muhimu kufanikiwa?
Kwa nini unataka ufanye kitu mara moja tu uwe umefanikiwa?
Kwa nini unataka usome kitabu mara moja tu uwe umekielewa?
Kwa nini unataka uwaambie watu kitu mara moja wakuelewe na kukubaliana na wewe?
Hivyo sivyo maisha yalivyo, chochote unachohitaji kifanikiwa kwenye maisha yako, kinahitaji marudio yasiyo na mwisho.
Kazi au biashara yako, lazima urudie kuifanya wakati wote ili kupata na kudumu kwenye mafanikio.
Vitabu unavyosoma, lazima uchague ambavyo utavirudia mara kwa mara ili uvielewe na kuviishi ka wakati.
Na hata wale unaotaka kuwashawishi wafanye kitu fulani, iwe ni kukubaliana na wewe au kununua unachouza, lazima urudie mara kwa mara ndiyo wasukumwe kuchukua hatua.
Hakuna utakachofanya mara moja kikakutosha, bali kila unachofanya unahitaji marudio yasiyo na ukomo ndiyo ufikie mafanikio makubwa.
Tunaishi kwenye zama za kelele na usumbufu mkubwa, ambapo kila mtu hana muda na amevurugwa, usipotumia marudio, hutaweza kufanya makubwa, kujifunza na kuwashawishi wengine.
Angalia matangazo ya makampuni makubwa ya simu au vinywaji, huwa yanarudiwa kila siku na kila mara, hata kama umeshalisikia tangazo linarudiwa tena na tena na tena. Makampuni hayo yanajua bila marudio hakuna matokeo.
Je ni marudio gani unatengeneza kwenye maisha yako?
Vitu gani unapanga kufanya kila siku ya maisha yako?
Vitabu gani umechagua kurudia kuvisoma mara kwa mara?
Ujumbe gani umechagua kujiambia mara kwa mara ili ukusukume kufanikiwa?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini na mara kwa mara nitakuwa narudia kukukumbusha usisahau.
Kocha.